SHAHIDI wa nane wa upande wa mashtaka, katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge Morogoro na dereva teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam, inayo mkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe ametoa ushahidi wake jana na kusema alikuwa na marehemu hao kabla ya kuuawa.
Shahidi huyo, Rajabu Juma Saidi ambaye ni fundi wa magari katika Gereji ya Yamungu Mengi, iliyoko Ilala, Dar es Salaam ambako kabla ya kuuawa wafanyabiashara hao, walipeleka gari lao kutengenezwa.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Angaza Mwipopo, shahidi huyo aliiambia mahakama hiyo, kuwa kabla ya wafanyabiashara hao kuuawa alishinda nao kwenye gereji yake ambako alikuwa akiwatengenezea gari lao.
Alisema awali, ndugu wa wafanyabiashara hao aitwaye Vasco alifika kwenye gereji yetu, akiwa na gari kwa ajili ya kulifanyia matengenezo na baadaye wafanyabiashara hao walifika wakiwa na gari ndogo aina ya Toyota Mark II.
Alisema baadaye Vasco alitumwa kwenda kununua vipuri mjini na kuwaacha ndugu zake hao katika gereji hiyo na aliporudi aliwasimulia habari za tukio la ujambazi ambalo lilikuwa limetokea usiku wa siku iliyopita.
“Watu wote tulichangia mada kuhusu taarifa za tukio hilo la ujambazi na ndipo Jongo (Ndugu wa Vasco na mmiliki wa gari hilo aliyeuawa), akasema kwa jinsi hali ya ujambazi ilivyo mbaya hivi sasa mtu ukiwa na pesa inabidi kuwa makini sana,” alieleza Saidi.
Alidai baadaye wakati akiendelea na matengenezo ya gari hilo, Jongo aliuliza mahali ambako angeweza kupata soda na bila kuchelewa Saidi aliwapeleka kwenye baa ya Bonga iliyoko Ilala Sharifu Shamba na baada ya kunywa soda walirudi kwenye gereji hiyo na mchana aliwapeleka kula katika Mgahawa wa Yamungu Mengi.
Alidai kuwa majira ya alasiri, Jongo na wenzake waliondoka kuelekea Bonga baa na kumwacha Saidi na Vasco akiendelea na matengenezo ya gari hilo, na kumuagiza kuwa gari likiwa tayari awataarifu.
“Tulipomaliza tulikwenda hadi Bonga baa na kumtaarifu kuwa gari liko tayari, akatuambia twende tukalijaribu sehemu zenye milima. Nilimwambia inabidi twende naye akalione, lakini akasema wao wanataka kwenda Sinza kupeleka pesa kwa mke wa rafiki yao ambaye yuko Mahenge,”alieleza Saidi.
Alidai kuwa baada ya hapo waliagana na Jongo na wao (Saidi na Vasco) walienda kulijaribu gari hilo katika milima ya Kisarawe na baada ya kuthibitisha kuwa lilikuwa sawa, alimpigia Jongo simu, lakini haikuwa na majibu na hata alipowapigia wenzake simu zao zilikuwa hazijibiwi.
Saidi alidai kwamba waliendelea kulijaribu gari hilo hadi Chanika na kwamba wakiwa huko, Vasco alipigiwa simu na Ngonyani kutoka Mahenge akimtaarifu kuwa ndugu zake wamekamatwa na polisi.
“Kesho yake asubuhi Januari 15, 2006 Vasco alikuja akaniambia kuwa amehangaika kuwatafuta ndugu zake katika vituo mbalimbali, lakini hakuwapata. Hivyo aliondoka lakini mchana akanipigia simu kuwa amepata taarifa ndugu zake wameuawa na kwamba alikuwa anaenda kuangalia miili yao Muhimbili. Baadaye mchana akanipigia simu kuwa naye (Vasco) amekamatwa,” Saidi aliieleza mahakama .
Baada ya kutoa maelezo hayo walisimama mawakili wa upande wa utetezi wakaanza kumuhoji maswali shahidi huyo.
Wakili wa kwanza alikuwa ni Moses Maira anayemtetea mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo, ACP Abdallah Zombe na baadhi ya mahojiano yao yalikuwa hivi:
Wakili Maira: Shahidi maelezo uliyoyatoa hapa ndiyo uliyoyaandika hata katika ‘statement’ yako kule makao makuu ya polisi au kuna mengine umeyasahau?
Saidi: Ndiyo hayo.
Maira: Mbona ulimwambia polisi kuwa Vasco alikueleza kuwa kaka yake ana pesa nyingi sana?
Saidi: Mimi hapa nilikuwa najibu maswali kama nilivyoulizwa.
Maira: Kuna lingine umesahau au hadi nikukumbushe?
Saidi: Itakuwa ni vema zaidi ukinikumbushia unalolijua wewe.
Maira: Vasco alipompigia simu, kaka yake alikwambia kwa nini haipatikani?
Saidi: Alisema inawezekana chaji imekatika.
Maira: Mbona hukulisema hilo hapa?
Saidi: Kwa sababu sikuulizwa, alijibu Saidi na kufanya baadhi ya wasikilizaji kutikisa vichwa huku wakicheka chini chini
Maira: Maelezo yako ya kule polisi, ulisema Vasco alikwambia kama ndugu zake wameenda Sinza walikuwa wameenda kwa mke wa nani?
Saidi: Wa mwenye teksi;
Maira: Ulijua mwenye teksi ni nani?
Saidi: Vasco alisema ni yule aliyeko Mahenge (Ngonyani shahidi namba Moja)
Maira: Kwa hiyo yule Ngonyani aliyekuja hapa kutoa ushahidi ndiye mwenye teksii?
Saidi: Hilo sijui.
Baada ya wakili Maira alisimama wakili Majura Magafu na Wakili Denis Myovela ambaye alimuuliza Saidi kuwa ni watu wangapi waliokwenda gereji.
Saidi: Walienda watu wengi tu, sasa sijui unauliza watu wa namna gani, maana hujaainisha swali lako.
Myovela: Waliohusiana na gari la Jongo.
Saidi: Kwanza walikuja wawili na baadaye wanne.
Awali shahidi namba saba, Hadija Mohamed Chwaka ambaye ni jirani wa shahidi namba mbili, Benadetha Felix Lyimo, mke wa shahidi namba moja (Ngonyani) alieleza jinsi alivyoshuhudia wafanyabiashara hao wakikamatwa na askari polisi na kuondoka nao kusikojulikana.
Alisema siku hiyo akiwa barazani kwake wafanyabiashara hao walifika na baada ya kusalimiana na Benadetha waliondoka na baadaye lilifika gari la polisi likiwa na askari waliovaa sare, wengine kiraia na baadhi wakiwa na silaha.
Alisema waliwazuia wafanyabiashara hao na kuwaamuru kushuka katika gari na kuwapekua huku wakiwatuhumu kuwa ni majambazi.
Alidai askari hao walichukua begi la wafanyabiashara hao lililokuwa na pesa na kuwachukua wafanyabiashara hao na kuondoka nao kusikojulikana.
Kabla ya kuchukua begi hilo, askari mmoja wa kike aliomba mkoba wa fedha wautunze kwenye gari dogo walilokuja nalo, lakini askari mwingine alisema bora akae nao kwani utatumika kama kidhibiti.
Katika hatua nyingine, watu wengi wanaendelea kufurika kusikiliza kesi hiyo ambayo inaendelea kuvuta hisia za watu.
No comments:
Post a Comment