Zombe akiingia katika basi la Magereza kuelekea ukonga huku akipiga mkwara mpigapicha!
MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara ACP Abdallah Zombe amewafokea waendesha mashtaka kwa madai kwamba wanachelewesha kesi yake.
Zombe alitoa tuhuma hizo jana wakati wa kusikiliza kesi yake inayoendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Mbali na malalamiko hayo, pia aliilaumu mahakama hiyo kuwa haimtendei haki, kwa kukubali kusikiliza mashtaka yake kinyume cha sheria.
Alifafanua kuwa alipokamatwa awali, alishtakiwa na kufikishwa mahakamani bila kupewa nafasi ya kutoa maelezo kuhusiana na mashtaka hayo.
Zombe alitoa malalamiko hayo baada ya mawakili wa utetezi kupinga shahidi namba 11, D8790, Koplo John kutoka Kituo Kikuu cha Polisi kutoa ushahidi wake kutokana na kutokidhi masharti ya kisheria ya kutoa ushahidi.
Jaji Salum Masatti anayesikiliza kesi hiyo alilazimika kuiahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, baada ya kiongozi wa waendesha mashtaka, Wakili wa Kujitegemea (PP), Revocatus Mtaki kuieleza mahakama kuwa hapakuwa na shahidi mwingine aliyeandaliwa baada ya Koplo John kumaliza kutoa ushahidi wake jana.
Wakili Majura Magafu alisimama na kuieleza mahakama kuwa upande wa utetezi haukuwa na jina la shahidi huyo katika orodha ya mashahidi wa kesi hiyo.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Angaza Mwipopo, alimtaka Jaji aendelee kusikiliza kesi hiyo, endapo upande wa utetezi utaridhia kwa kuwa maelezo ya shahidi yalikuwepo.
Baada ya mawakili wa upande wa utetezi kupitia vifungu kadhaa vya sheria juu ya utoaji wa ushahidi, kwa nyakati tofauti walisema kwa kuwa maelezo ya shahidi huyo hayakusomwa wala shahidi huyo kutajwa kama shahidi, hawezi kuruhusiwa kutoa ushahidi.
Kutokana na maelezo ya upande wa utetezi, Jaji Masatti alikubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuamua kuahirisha kesi hiyo.
Kabla ya Jaji Masatti kuahirisha kesi hiyo, Zombe alinyoosha mkono na kuanza kuufokea upande wa mashtaka kwamba haujaandaa mashahidi wengi na kwamba hali hiyo inamnyima haki.
“Mheshimiwa Jaji mimi ninadhani mahakamani ni ndipo mahali ambako haki inatendeka. Mashahidi ambao ni askari wako wengi tu zaidi ya 30 na hawako mbali kiasi kwamba ukifungua tu mlango wa ofisi yako utapaona makao makuu walipo. Leo hii kesi kubwa kama hii, ambayo inavuta hisia za watu wengi inakosa mashahidi,” alisema Zombe kwa hasira.
Alidai kuwa mpaka sasa yeye si mshtakiwa, bali amefikishwa katika mahakama hiyo, kwa nia mbaya kwa kuwa alikamatwa na kupelekwa mahakamani bila kuandika maelezo yake.
Zombe alidai kikatiba ni makosa na ni marufuku kumkamata mtu bila kufuata sheria na kwamba hajui ni kwa nini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na askari polisi walimkamata na hatimaye kumfikisha katika mahakama hiyo bila kupewa nafasi ya kuandika maelezo yake na badala yake alishitakiwa moja kwa moja.
Zombe aliyasema hayo huku akikariri kifungu cha maandiko Matakatifu katika Biblia Takatifu akisema, katika Injili ya Yohana sura ya Saba, mstari wa 51 (Yoh.7:51) kinaeleza kuwa, huwezi kumhukumu mtu kabla hujampa nafasi ya kumsikiliza kwa kile alichokitenda.
Akitafsiri kifungu hicho cha Biblia, Zombe alisisitiza kuwa yeye si mshtakiwa na kuwa hajapewa nafasi ya kuandikisha maelezo yake.
“Akawaambia Nikodemu je, Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikiliza kwanza na kujua atendalo?” Zombe alisema akinukuu kifungu hicho cha Biblia na kuvuta hisia za watu waliokuwa wakifuatilia kwa makini mwenendo wa kesi hiyo.
Pia aliilaumu mahakama kwa kukaa kimya baada ya kufikishwa katika mahakama hiyo kinyume cha sheria, ingawa katiba iko wazi katika suala hilo.
"Katiba inasema ni lazima mtu asikilizwe kwanza, lakini mimi sijapewa nafasi hiyo. Na sasa hivi kila mahali ukipita ni Zombe, Zombe tu, nimekuwa kama wimbo,” alifoka.
Baada ya Zombe kufoka, Mwendesha Mashtaka Kiongozi, Mtaki alisimama na kuiambia mahakama kuwa, Zombe hakupaswa kufoka mahakamani na kwamba alipaswa kuwasilisha hoja yake kupitia kwa mawakili aliowaajiri.
Mtaki alipinga hoja ya Zombe kwamba hakusikilizwa na kufafanua kuwa haikuwa ya msingi, kwa sababu yuko mahakamani ambako anaweza kusikilizwa na uamuzi kutolewa juu ya mashtaka yake na kwamba asiporidhika, anaruhusiwa kukata rufaa na kuongeza kuwa kitendo cha kutokuandika maelezo yake, hakizuii Jamhuri kumshtaki.
Kuhusu hoja ya mashahidi, Mtaki alisema upande wake hauna shida na kwamba kama mahakama itaridhia wako tayari kwenda kuwaandaa mashahidi kwa ajili ya kutoa ushahidi wao muda wowote.
Licha ya maelezo hayo, Zombe aliendelea kufoka na kudai kuwa PP huyo, anafanya hivyo kwa sababu ametoka Arusha, hivyo anapata posho (night allowance).
PP Mtaki alisimama tena na kukanusha kuwa yeye hapati posho na akamtaka Zombe akanushe kauli hiyo.
Kutokana majibishano hayo, wakili wa Zombe, Jerome Msemwa alisimama na kumwomba radhi Mtaki kwa niaba ya mteja wake. Alikiri kuwa mteja wake alipaswa kuwasilisha hoja zake kupitia kwake, hata hivyo alisisitiza kuwa hoja alizozitoa Zombe zinapaswa kutiliwa maanani.
Baada ya malumbano hayo, Jaji Masatti alimshauri Zombe afungue kesi ya kikatiba kama anadhani haki zake zimevunjwa na kusema kuwa kesi hiyo, itaendelea kusikilizwa na alimwambia mshitakiwa ana nafasi ya kukata rufaa.
Mara baada ya Jaji kuahirisha kesi hiyo, Naibu Kiongozi wa waendesha mashtaka hao, Jasson Kaishozi aliendelea kumfokea Zombe wakati akitolewa kizimbani na askari, kutokana na kitendo chake cha kufoka katika mahakama hiyo na kumtuhumu PP Mtaki kuwa anapata posho.
“Huyu asitake kuleta uhuni hapa, hapa hakuna cha UACP wala nini, hata ufanye nini hapa wewe (Zombe) ni mshitakiwa tu,” alifoka Kaishozi huku akitulizwa na askari mmoja wa Jeshi la Polisi akimsihi aachane na Zombe.
Naye PP Alexander Mzikila akiwa nje ya mahakama hiyo, alisema si kosa kwa mtuhumiwa Zombe kuwasilisha hoja zake na kwamba ingekuwa vizuri zaidi kupitisha hoja hizo kwa mawakili wake.
Katika hatua nyingine, nje ya mahakama, wakili mmoja ambaye anawatetea baadhi ya watuhumiwa katika kesi hiyo, alisema madai ya Zombe kuwa hakuandika maelezo hayana msingi ingawa kwa upande mwingine yanaweza kuwa na masilahi kwake.
Januari 14, mwaka 2006 katika Msitu wa Pande ulioko Mbezi Luis wilayani Kinondoni waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini na wakazi wa Wilaya ya Mahenge mkaoni Morogoro, Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo pamoja na dereva teksi wa Manzese, jijini Dar es Salaam Juma Ndugu.
No comments:
Post a Comment