PINDA SEMA PESA ZA EPA LAZIMA ZIRUDI BOT
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema mabilioni yaliyoibwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya Benki Kuu (BoT), yalitoka katika taasisi hiyo, hivyo lazima zirudi.
Kauli ya Pinda imekuja wakati kukiwa na mjadala kuhusu nani hasa mmiliki wa fedha hizo, kufuatia Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kusema fedha hizo si za BoT wala serikali bali ni za wafanyabiashara.
Akifanya majumuisho ya hotuba yake mjini Dodoma jana, Pinda alisema anajua shauku iliyopo ni kubwa kwani wananchi wengi wanataka kujua fedha hizo ni za nani na mwisho wake ni upi, lakini kubwa ni kwamba fedha hizo lazima zirudishwe kwa gharama yoyote.
"Hili suala la EPA najua lina mvuto mkubwa mimi najua kwa nini, lakini ndugu zangu kwa kuwa fedha hizo zilikuwa Benki Kuu hakuna haja ya kugombana tufanye subira, mwisho wa safari ni lazima zirudi," alisema Waziri Mkuu Pinda.
Alisema kuwa wanachokifuatilia ni jinsi fedha hizo zilivyotolewa BoT, zilitolewa na nani, kwenda wapi na kufanya nini.
Akizungumzia juu ya tume ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete na kupewa jukumu la kuhakikisha fedha hizo zinarudishwa na kupewa muda wa miezi sita, alisema hata yeye hajui kinachoendelea katika tume hiyo.
"Ukiniuliza hata mimi sijui rafiki yangu katika tume hiyo wamefikia wapi? Hapa ndugu yangu Mwanyika hata nikimuuliza haniambii, badala yake anasema subiri," alisema Pinda na kuwataka Watanzania wawe na subira, kwani anaamini fedha hizo zitarudishwa.
Kwa muda wa wiki mbili wadau mbalimbali wakiwemo wasomi na wanasiasa wameibuka na kupinga kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mkulo aliyoitoa bungeni kuwa pesa za EPA si za umma na kwamba pesa hizo ni za wafanyabiashara.
Kauli hiyo pia iliwaweka njiapanda baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ambao walipoulizwa na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti walishindwa kutoa majibu sahihi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo, alisema kauli ya Waziri Mkulo, imemwacha gizani huku CAG, Utouh akitaka suala hilo aachiwe mwenyewe Mkulo alitolee ufafanuzi kwa kuwa anavyoelewa yeye fedha za EPA ni mkusanyiko wa fedha nyingi ingawa hakuzichanganua.
Kauli hiyo tata ya Mkulo inapingana na Taarifa ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa kupita kwa Luhanjo Januari 9 mwaka huu kuwa fedha hizo ni za umma na kutaka hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kuhusika na upotevu huo na kuhakikisha kuwa zinarejeshwa.
Katika taarifa hiyo, Luhanjo alitoa takwimu za deni hilo kuwa lilianzia mwaka 1999, lilikuwa ni dola za Marekani 623 milioni, ambazo kati ya hizo, dola 325 milioni zilikuwa deni la msingi na dola 298 ni riba na baadaye deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.
Hata hivyo, alisema chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.
Utaratibu huo ulileta matatizo ambayo yalibainika katika Ukaguzi wa Hesabu za BoT za mwaka 2005/06, ambao ulifanyika Agosti, 2005.
EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo awali ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT, kwa madhumuni ya kulipa wafanyabiashara ambao waliingiza bidhaa nchini, kwa sababu wakati huo serikali ilikuwa inakabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni.
Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa BoT, na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha kampuni ya Ernst &Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG, mapema Desemba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment