Friday, June 06, 2008

ZOMBE LEO

Silaha zilizotumika zawasilishwa kortini Silaha zilizotumika katika mauaji ya wafanyabiashara zikiwa mahakamani jana kama kielelezo.

BUNDUKI mbili zinazodaiwa kutumiwa na polisi wanaotuhumiwa kuwaua wafanyabiashara wa Mahenge zimewasilishwa mahakamani .
Silaha hizo zilizokabidhiwa jana katika mahakama hiyo, zote ni bunduki aina ya SMG namba 13059192 na 3N0199P.
Shahidi namba 22 katika kesi hiyo, Mrakibu wa Polisi, Juma Bwire kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Kitengo cha Uchunguzi wa Silaha, aliieleza mahakama kuwa baada ya silaha hizo kutumika, zilipelekwa kwake zikiwa pamoja na maganda tisa ya risasi.
Shahidi wa 15 katika kesi hiyo, Koplo Xaver Kajera ambaye ni mtunza ghala la silaha Kituo cha Polisi cha Oysterbay, alidai mahakamani hapo kuwa bunduki moja alikabidhiwa Koplo Saad na nyingine alikabidhiwa Koplo Rashid ambaye pia ni mmoja wa washitakiwa katika kesi hiyo.
Koplo Kajela alidai bunduki namba 3N0199P alikabidhiwa Koplo Saad na namba 13059192 alipewa Konstebo Rashid.
Shahidi huyo alidai kuwa siku iliyofuata baada ya siku waliyokabidhiwa, walirejesha silaha hizo na kwamba Koplo Saad alirejesha bunduki aliyokabidhiwa ikiwa na risasi 21 zikiwa zimepungua risasi tisa na Rashid alirejesha risasi zote 30.
Koplo Kajela alidai askari wengine aliowakabidhi silaha hizo kuwa ni D.9321 Konstebo Rashid Lema mshitakiwa wa 11, D.4656 Koplo Rajabu Hamis Bakari mshitakiwa namba 12 ambao wako katika kesi hiyo.
Akitoa ushahidi wake katika mahakama hiyo jana, SP Bwire alidai kuwa Januari 25, 2006 alipokea silaha hizo pamoja na maganda tisa ya risasi kama vielelezo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Alidai alipokea silaha hizo pamoja na barua ya maombi ya kufanya uchunguzi kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, SP Christopher Bageni ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo.
Bwire alidai dhumuni la uchunguzi huo, ilikuwa ni kubaini maganda tisa ya risasi zilizofyatuliwa kutoka katika bunduki gani kati ya mbili alizokabidhiwa.
Alidai mahakamani hapo kuwa silaha hizo alipokea zikiwa katika hali nzuri na kwamba hazikuwa zimechakaa.
“Baada ya uchunguzi nilibaini kuwa maganda matano yalikuwa yametumika katika silaha SMG namba 3N0199P na maganda manne yalitumika katika silaha SMG namba 13059192,” alisema Bwire.
Alidai kuwa Machi 9, 2006 alipelekewa maganda mengine mawili ya risasi ili ayafanyie uchunguzi kubaini kama yalitumika katika silaha za awali alizopelekewa.
Bwire katika ushahidi wake aliieleza mahakama kuwa si rahisi kutambua kama silaha hizo zilitumika mahali pengine baada ya tukio la Januari 14, Mwaka 2006.
Naye shahidi namba 21 katika kesi hiyo, Sajenti Hassan ambaye ni mtunza ghala la silaha katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, alidai katika mahakama hiyo kuwa, Januari 14, Mwaka 2006 alimkabidhi D. 2300 Koplo Abenet Saro bastola moja namba 212115 ikiwa na risasi nane ambaye ni mshitakiwa wa 10.
Alidai siku iliyofuata Koplo Saro alirejesha silaha hiyo ikiwa salama pamoja na risasi zote nane na kwamba hakuna risasi hata moja ambayo ilikuwa imetumika.
Shahidi huyo pia alidai anamfahamu mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, ASP Ahmed Makelle ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi kituoni hapo, lakini akadai kuwa siku hiyo hakumpa silaha yoyote.
Alidai katika kipindi hicho, ASP Makelle alikuwa na silaha aina ya bastola namba 16013916 na risasi nane, ambayo alikabidhiwa na D. 8348 PC Emmanuel tangu Juni 8, 2005.
Sajenti Hassan alidai ASP Makelle alirejesha bastola hiyo Januari 25, 2006 ikiwa salama na risasi zote.
Baadhi ya mahojiano kati ya shahidi na mawakili yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Majura Magafu: Shahidi je, kulikuwa na kosa lolote kwa ASP Makelle kukaa na silaha hiyo kwa kipindi chote hicho?
Sajenti Hassan: Hapakuwa na kosa kwa kuwa yeye kama Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi anaweza kukaa na silaha kwa muda wowote kwa ajili ya kuangalia hali ya usalama.
Magafu: Kwa hiyo wajibu wake akishaitumia silaha ndio anatoa ripoti?
Sajenti Hassan: Ndio.
Wakili Msafiri: Umesema askari akitumia silaha hufungua taarifa ya matumizi ya silaha husika, jalada hilo linaitwaje?
Sajenti Hassan: Linaitwa kufyatua risasi.
Mzee wa Baraza Kimolo: Siku hiyo uligawa silaha ngapi?
Sajenti Hassan: Sihala nne.
Kimolo: Je, zilirudi salama?
Sajenti Hassan: Ndio silaha zote zilirudi salama.
Kimolo: Kama mtunza ghala la silaha huwa unapeleka taarifa ya matumizi ya silaha kwa uongozi wa juu?
Sajenti Hassan: Ndio kila baada ya miezi mitatu au miezi sita.
Kimolo: Je, huwa kwa maandishi?
Sajenti Hassan: Ndio.
Kimolo: Umesema Makelle alipewa silaha tangu Juni 8, 2005 akarudisha Januari 25, 2006, je imo katika kumbukumbu zako?
Sajenti Hassan: Ndio.
Mzee wa Baraza Mosi: Umesema Makelle alikaa na silaha hiyo kwa muda wote huo, nani alimpa kibali hicho?
Sajenti Hassan: Yeye ni bosi hahitaji kupata kibali.
Mosi: Nani alimwambia airejeshe silaha hiyo tarehe hiyo?
Sajenti Hassan: Aliirejesha kwa sababu alikuwa anataka kwenda kusoma nchini Misri.




















2 comments:

Pope said...

Kazi Ipo!!

Anonymous said...

Nimekuwa nikifuatlia kesi hii kwa muda lakini nadhani Zombe atafungwa kutokana na kukosa wakili madhubuti. Mpaka sasa upande wa mashitaka umeshindwa kutoa ushahidi unaonyesha ya kuwa ni kweli risasi zilizotumika zimetoka kwenye ile bunduki .

Pili kitendo cha dookta kusema ya kuwa wale watu waliwekwa chini na kupigwa risasi inaonyesha dhahiri alikuwa na preconceived ushahidi . Jee vipi kama mpigaji aliamua kuwa piga risasi hao watu wote katika sehemu moja tuu , namaanisha endeo fulani la mwili tuu. Nadhani wale waliona kesi mbali mbali za maserial killer watakubalina na mimi .

T