Wednesday, June 04, 2008

ZOMBE

Zombe adaiwa kuongoza polisi wavaa kininja

Kipande hiki nilishindwa kukiweka kutokan na sababu za kiufundi

SHAHIDI wa 12 katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro, Zainabu Hashimu Masogoa jana amedai kuwa askari polisi waliwavamia waombolezaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakiwa wamevaa kininja na kuleta hofu kwa waombolezaji hao.
Masogoa alisema hayo jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi mbele ya Jaji Salum Masatti wa mahakama hiyo anayesikiliza kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2006, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Abdallah Zombe na wenzake 12.
Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anmgaza Mwipopo, Masogoa alidai siku ya Jumatano ya Januari 18, mwaka 2006 alikuwa ni miongoni mwa waombelezaji waliofika katika hospitalini hiyo kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu hao kabla ya kusafirishwa kwenda Mahenge kwa ajili ya mazishi.
Alidai mara baada ya kumaliza kuuandaa mwili wa dereva teksi Juma Ndugu na kuupeleka msikitini katika hospitali hiyo kwa ajili ya kufanyiwa ibada, ghafla gari la Polisi aina ya Land Rover Defender lilifika likiwa na askari polisi huku likiendeshwa kwa kasi.
Masogoa alidai askari hao walikuwa wakiongozwa na Zombe ambaye alikuwa amevaa sare za kazi huku askari wake wakiwa wamevaa soksi usoni, ili kuficha nyuso zao na kuacha sehemu ya macho tu, huku wakiwa na bunduki ambazo walikuwa wamezishikilia tayari kwa kuanza kazi.
Alidai walipofika, walishuka kwa harakaharaka na kuwaamuru watu wapishe, jambo ambalo liliwatisha watu na kulazimika kukimbia pembeni ili kuwapisha.
Alidai baada ya kuwapisha, askari hao walikwenda moja kwa moja hadi msikitini ambako ibada ya kumuaga marehemu ilikuwa ikifanyika.
“Wakati askari hao wakiingia msikitini, Zombe alikwenda kusimama katika mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti akawa anazungumza na watu fulani,” alidai Zainabu na kubainisha kuwa hakujua walichokuwa wakizungumza.
Baadaye akijibu swali kutoka kwa wakili Majura Magafu, ambaye alitaka kujua kama kulikuwa na madhara yoyote baada ya Zombe kufika katika eneo la msikiti huo, shahidi huyo alidai askari hao hawakuwafanyia fujo waombolezaji bali kutokana na staili yao, walitishika.
“Japo hakuna jambo baya lolote walilolifanya kwa waombolezaji, ujio wao ulitutisha kwa sababu walikuwa wamevalia kijambazi. Walificha sura zao kwa maana kwamba wasitambulike, hivyo wangeweza kumdhuru mtu bila kutambulika,”alisisitiza shahidi huyo.
Awali Masogoa ambaye ni Mhudumu katika Hoteli ya Bondeni iliyoko Magomeni ambako marehemu walifikia, aliieleza mahakama kuwa aliwapokea marehemu hao Januari 12, mwaka 2006 na kuwakabidhi vyumba na kwamba aliwaona tena Januari 14, mwaka 2006 asubuhi na aliondoka kuendelea na kazi na kuwaacha wakinywa chai.
Alidai kuwa Januari 15, 2006 alipata simu kutoka Mahenge kwa Alex Ngonyani (shahidi namba moja) kwamba wageni wake walikamatwa na polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi Urafiki.
“Nilimpigia simu Afande Mbaraka wa kituo cha polisi Magomeni baada ya kupata namba ya simu yake kwa mke wake ambaye anafanya kazi pale hotelini, nikamweleza habari hizo akaniambia nisubiri afuatilie,” alisema Masogoa.
Aliongeza kuwa baadaye Afande Mbaraka alimpigia simu mdogo wake aitwaye Zubeda na kumwambia kuwa wageni wake walikuwa wameuawa.
Kwa upande wake shahidi wa 11 katika kesi hiyo, Jafar Amir Jafar, alikana kuwa wafanyabiashara hao hawakuwahi kumvamia na wala kupora dukani kwake.
Akitoa ushahidi katika kesi hiyo huku akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Alexander Mzikilz, Jafar ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki duka la vito vya thamani, alidai majambazi waliomvamia na kumpora anawafahamu na kwamba siyo aliowaona hospitali ya Muhimbili.
Alidai kuwa majambazi waliomvania aliwakariri vizuri kabisa sura zao, kwa kuwa alikaa nao kwa muda mrefu na kubainisha kuwa mmoja alikuwa ni mwanaume mrefu mnene mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde.
Jafar alidai kuwa Januari 14,2006 akiwa dukani kwake na wenzake wawili, Mohamed Yakub na Mzee Ali, alifika mteja mmoja na kutaka kubadilisha mkufu wake.
Alidai mteja huyo alikuwa akiwasiliana kwa lugha ya Kiingereza, baadaye alichagua mkufu mwingine na baada ya kuelewana bei aliomba apunguziwe lakini baada ya muda mfupi waliingia watu wengine wawili, mmoja mwanaume na mwingine mwanamke.
Alidai baada ya dakika chache mwanamke alitoka na kumwambia mwanaume kuwa anakwenda kununua dawa.
“Yule mwanamke alipotoka tu,yule mteja mwanaume alichomoa bastola na kumlenga Mohamed Yakubu na wakati huohuo yule mteja wa kwanza alinirukia pale kaunta, lakini hawakumjeruhi Yakubu,” alidai.
Jafar alidai baada ya majambazi hao kuwaweka chini ya ulinzi walichukua bastola yake na kisha kuanza kukusanya vitu mbalimbali na kwamba wakati wakikusanya vitu hivyo, walisikia mlio wa risasi nje ya duka hilo.
Alidai baada yakusikia mlio huo, majambazi walimlazimisha awafungulie mlango mwingine wa kutokea nje kwa mbele na kwamba walimtishia kwamba akikataa watatoka nje na mtoto wake, hivyo akalazimika kuwafungulia mlango huo.
“Baadaye tulipotoka nje tulikuta mlinzi wangu ndio amepigwa risasi hivyo tukamchukua na kumpeleka hospitali,”alisema Jafar na kuongeza kuwa walipata habari kuwa majambazi hao, walikuwa wengi na kwamba walikuwa na magari mengi tu waliyokuwa wameyaegesha maeneo tofautitofauti.
Alidai kuwa siku mbili baadaye, alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Msimbazi kuwa kuna majambazi wameuawa na kwamba, aende Muhimbili kuwatambua kama ndio waliomvamia na kumpora dukani kwake.
“Tulikwenda Muhimbili, sisi wote mimi, Mohamed Yakub na Mzee Ali na tukakuta miili ya watu wanne. Wale watu tulitambua kuwa siyo majambazi waliotuvamia,” alisisitiza Jafar.
Baada ya kutoa maelezo hayo, mashahidi hao waliulizwa maswali mbalimbali na mawakili wa upande wa utetezi na baadhi ya mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Magafu: Shahidi ulisema wakati ukiwa ndani ulisikia risasi zikilia huko nje je, hii inaashiria nini?
Shahidi wa 11, Jafar: Kulikuwa na majambazi wengine nje.
Majura: Wewe hukuwatia machoni, je yuko jambazi yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na ukamtambua ni miongoni mwa waliokuvamia?
Jafar: Tulishakwenda mara mbili Kituo cha Polisi Msimbazi lakini wote waliokuwa wamekamatwa walikuwa siyo.
Majura: Umesema ulikwenda Muhimbili kutambua maiti zile baada ya siku mbili je, unakubaliana na mimi kwamba mtu anakuwa mochwari hasa hizi za kwetu na baadaye anabadilika?
Jafar: Ndio, lakini hao sisi tuliwaona ‘face to face’, hivyo tuliwatambua kuwa siyo waliohusika.
Wakili Rongino Myovela: Shahidi umesema wewe ulikuwa ndani na yaliyoendelea nje hukuyaelewa je, nikisema baada ya tukio hilo polisi waliokuwa doria walifukuzana na majambazi hao huku wakirushiana risasi unalijua hilo?
Jafar: Silijui.
Wakili Moses Maira: Shahidi umesema Zombe alikuja mochwari na askari je, kabla ya hapo Mochwari ulikuwa umemuona?
Shahidi namba 12, Zainabu: Nilimuona kwenye TV (Runinga) akitangaza kuwa wameua majambazi.
Maira: Mbona kuna mambo umeyasema hapa, lakini katika statement yako (maelezo ya maandishi) uliyoitoa polisi hukuyasema?
Zainabu: Hata bungeni huwa kuna maswali ya nyongeza.

Naye Shahidi wa 14 Costantine ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa siku ya tukio washitakiwa saba katika kesi hiyo walikuwa kwenye doria.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa alistaafu jeshi la polisi Julai mwaka jana akiwa Msaidizi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alidai kuwa siku hiyo ya Januari 14, mwaka 2006, washitakwa saba katika kesi hiyo wakiwa askari wa kituo cha polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walikwenda kwenye doria na kwamba zilitolewa silaha tatu zikiwemo bastola (risasi 8), SMG (risasi 30) na SMG nyingine (risasi 30).

Washitakiwa waliokuwa kwenye doria siku hiyo ni Coplo Festus, Coplo Nyangehera, PC Michael, Coplo Felix, Coplo Emanuel, PC Noel na Station Sajent James.

Alidai siku iliyofuata asubuhi alipokea silaha zote na kuzirudisha katika ghala huku zikiwa na risasi zote zilizokuwa zimetolewa.

“Asubuhi nilipofika kazini nilikuta askari waliokuwa doria usiku, wako kwa mkuu wa kituo na niliwasikia wakisema kwamba walipambana na majambazi usiku na wakawa wamewaua,” alieleza Costantine.

Shahidi huyo alidai kuwa hakukuwa na askari yeyote aliyekuwa amejeruhi katika mapambano hayo.

Naye Shahidi wa 13 katika kesi hiyo ambaye ni Afisa wa Jeshi la Polisi PC John ameieleza mahakama kuwa, siku ya tukio akiwa kazini alimsikia mwenzake aliyekuwa naye akipokea taarifa kutoka kwa maaskari waliokuwa maeneo mbalimbali ya Jiji kwamba, maeneo ya Samnujoma kumetokea tukio la ujambazi.

Kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2006 kwa mara ya kwanza, Zombe na wenzake 12 walifikishwa mahakamani Septemba 28, mwaka juzi mbele ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Laurian Kalegeya ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Zombe alipandishwa katika mahakama hiyo, kwa mara ya kwanza Juni 9, saa 4:00 asubuhi na Juni 15 mchana alifutiwa shtaka la mauaji lililokuwa likimkabili peke yake mbele ya Kaimu Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Addy Lyamuya na kuunganishwa na wenzake 12 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi.

Ilidaiwa katika mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja Januari 14, katika Msitu wa Pande ulioko Mbezi Luis wilayani Kinondoni waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini na wakazi wa wilaya ya Mahenge mkaoni Morogoro, Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo pamoja na dereva teksi wa Manzese Juma Ndugu.

No comments: