Friday, July 04, 2008

MSIMAMO

Tanzania haitambui urais wa mugabe!!!!

TANZANIA imesema haimtambui Robert Mugabe kama Rais halali wa Zimbabwe kwa kuwa amechaguliwa katika uchaguzi uliokiuka vigezo vyote vya demokrasia.
Msimamo huo wa Tanzania, ambao ni wa kwanza kutolewa tangu uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe urudiwe Juni 27, mwaka huu na kumrejesha Mugabe madarakani, ulitangazwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Waziri Membe aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya wizara hiyo, jijini Dar es Salaam kuwa msimamo huo umefikiwa kwa vile ushindi wa sasa wa Mugabe ni sawa na kufunga goli la kuotea katika mpira wa miguu.
“Uchaguzi wa Zimbabwe ni sawa na mchezo wa mpira. Goli la Mugabe limekuwa offside (la kuotea),” alisema Membe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU).
Alisema ukiukwaji wa vigezo vya demokrasia katika uchaguzi wa rais wa Zimbabwe, ulibainishwa na ripoti ya waangalizi zaidi ya 413 walioshuhudia uchaguzi huo.
Membe alisema baadhi ya waangalizi, wanatoka Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Bunge la Afrika, wote waliridhika kuwa uchaguzi huo ulipoteza sifa ya kuwa huru na wa haki.
Alisema katika uchaguzi huo baadhi ya vyama (isipokuwa Zanu-PF cha Mugabe) havikuruhusiwa kufanya kampeni na baadhi ya wagombea walinyimwa fursa ya kutumia vyombo vya habari.

2 comments:

Simon Kitururu said...

Itanishangaza nikisikia nchi nyingi za kiafrika zikikiri msimamo huu waziwazi!Hata JK alikuwa anakwepa kutamka wazi hili jambo !

Anonymous said...

Kwanza unakaa kimya na kuiacha Zimbabwe ifanye uchaguzi katika mazingira ya kutatanisha kabisa na ukijua wazi Mugabe anajitafutia uhalali tu wa kuhesabika kwamba kachaguliwa kihalali na wazimbabwe walio wengi na ukisha kuwa na uhakika kwamba ni Mugabe ndiye aliye tangazwa mshindi na Rais wa Zimbabwe ndipo wewe sasa unapo jitokeza na kutoa Tamko rasmi kwamba 'Hatuitambui serikali ya Mugabe kwa sababu uchaguzi haukuwa huru na wa haki'!That is Political Abracadabra at its Best!Congratulations whoever it is for the intelligent and genious creativity in political abstract thinking!Siasa za Bongo hizo...