Thursday, September 11, 2008

NAPE AVUKA KIGINGI CHA KWANZA
MWENYEKITI wa CCM, Jakaya Kikwete jana alimpa ruksa mwanasiasa kinda wa chama hicho, Nape Moses Nnauye kukata rufaa iwapo anaona hakuridhika na uamuzi wa kumvua uanachama wa Umoja wa Vijana wa chama hicho, UVCCM, akitofautiana na katibu wake, Yusuf Makamba, ambaye alisema kijana huyo hawezi kukata rufaa katika chombo chochote.
Kikwete, akitoa taarifa fupi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) jana, pia alisema chama hicho tawala kitaendelea kumtambua Nape kama mjumbe wake, mwanachama na kutambua nyadhifa zake zote ndani ya CCM, tofauti na mapendekezo ya Baraza Kuu la UVCCM lililotaka mtoto huyo wa mwanasiasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho, marehemu Moses Nnauye, avuliwe nyadhifa zake zote.
Baraza hilo, ambalo lilimjumuisha Makamba, ambaye ni mtendaji mkuu wa CCM na mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru, ambaye ni Kaimu Kamanda wa Vijana Tanzania Bara, lilimvua Nape uanachama na kupendekeza avuliwe nyadhifa nyingine zote ndani ya CCM, kwa madai kuwa alisema uongo alipotoa tuhuma nzito kuwa mkataba wa uwekezaji wa jengo la Makao Makuu ya UVCCM unanuka rushwa.
Lakini jana, kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha NEC kilichofanyika mjini Dodoma, Kikwete, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliuambia mkutano huo kuwa Halmashauri Kuu inamtambua Nape kama mjumbe halali, mwanachama wa CCM na pia inatambua nyadhifa zake zote ndani ya chama na kwamba, kijana huyo machachari anayo haki ya kukata rufaa kupinga maamuzi ya Baraza Kuu la UVCCM.
"Hiyo ilikuwa ni taarifa fupi ya mwenyekiti mwenyewe," alisema mtoaji habari wetu. "Aliichomeka hoja hiyo na kuweka bayana kuwa, NEC inamtambua Nape kama mjumbe, nyadhifa zake na uanachama wake. Baada ya kauli hiyo, wajumbe walipiga makofi na kuunga mkono."
Chanzo hicho kutoka NEC kilifafanua zaidi kuwa, mwenyekiti alisema maamuzi ya Baraza Kuu la UVCCM ni ya vijana wenyewe na kwamba kama Nape akiamua kukata rufaa, anaruhusiwa kufanya hivyo kwa kufuata ngazi husika, kwa mujibu wa taratibu za chama na jumuiya.
Kwa mujibu wa taarifa hizo za kuaminika, Kikwete aliweka bayana kwamba maamuzi ya Baraza Kuu la UVCCM ni ya vijana wenyewe na chama hakiwezi kuingilia wala kuhusishwa nayo.
Alipoulizwa kuhusu msimamo huo wa NEC, Nape alisema alikuwa mwenye furaha na akarudia kauli yake kuwa ana imani na vikao vya juu vya CCM.
"Nimepokea habari hizi kwa furaha kubwa na nina matumaini makubwa na imani na vikao vya juu vya chama," alisema.
"Ushindi uliopatikana katika hatua hii si wangu binafsi, bali ni ushindi wa wale wote wanaopenda kusema ukweli na kuusimamia.
"Nawataka wale wote wanaoniunga mkono, wasikate tamaa kwa sababu safari inaendelea na inanionyesha kwamba, kuna mwelekeo wa mafanikio.
"Kwa matokeo haya angalau ninaweza kusema kwamba ukweli umeshinda na hii inatupa changamoto wote kwamba mtu unaposimamia ukweli, basi daima uwongo unajitenga."
Ushindi wa Nape pia ulijidhihirisha katika uamuzi mwingine wa Kamati Kuu, iliyokutana juzi na kuamua kutoupitisha Mkataba wa uendeshaji wa jengo la Makao Makuu ya UVCCM ikitaka uangaliwe upya.
Makamba, ambaye aliingia kwenye Baraza Kuu la UVCCM kwa wadhifa wake wa Katibu Mkuu wa chama, amekuwa akiwaambia waandishi kuwa uamuzi wa kumvua Nape uanachama ni wa mwisho na kwamba, kijana huyo hawezi kukata rufaa popote pale mbinguni na duniani.
Mara kadhaa amekuwa akiripotiwa kueleza kuwa kitendo cha Nape kukikosoa chama nje ni cha utovu wa nidhamu na kuwajibu wale waliokuwa wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu kuwa, demokrasia haikutendeka kwa kusema demokrasia haiendani ni utovu wa nidhamu.
Lakini maamuzi hayo yalipingwa na makada waandamizi wa CCM, wakiwemo mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa David Msuya na Frederick Sumaye, ambao walisema waziwazi kuwa Baraza Kuu liliamua kwa jazba.
Awali, suala la Nape halikuwa ajenda kwenye kikao hicho cha NEC na kwa maana hiyo halikuweza kujadiliwa kutokana na kutokuwepo rasmi. Ajenda zilizokuwepo zilikuwa ni uchaguzi wa Tarime.

1 comment:

Anonymous said...

HONGERA NAPE MNAUYE.
SIKU ZOTE UKWELI UTABAKI KUWA UKWELI.

RAIS AMEUTAMBUA UKWELI!!!

BIG UP MHE.JAKAYA MRISHO KIKWETE

Habari za leo watanzania wezangu. Mimi kama kada wa CCM nimefurahishwa sana na muono wa mbali wa Rais wetu pendwa wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua nyasifa zote alizokuwanazo huyu mwanasiasa kijana na machachari Nape Mnauye.Kwa kweli hili pia limedhihirisha kuwa Kikwete bado yuko makini mno ktk maamuzi yake yote ambayo yeye huyachukua kwa kuyamini kuwa ni sahihi.

Unajua Rais wetu ameona mbali sana kiasi cha kutokukumbatia zaidi maamuzi ya baraza kuu la UVCCM ambalo mimi naweza sema kuwa sijui lilikuwa linakitakia nini chama hapo siku za usoni.

Ujumbe wangu kupitia makala hii ni kuwa,wazee wasitumie zaidi madaraka yao kunyamazisha mawazo ya vijana walio na muono unaokwenda na wakati na badala yake ni bora wawe wanangalia umuhimu na uwepo wa vijana ambao ni wazalendo na hujenga hoja zikakubalika kwa watu.Inashangaza kuona kuwa ni kipindi kirefu kwa chama kupitia UVCMM kilimwamini Nape Mnauye na kumpa nyazifa nyingi ktk chama halafu leo kinasema yeye ni wendawazimu.Wanasahau wendawazimu waliopo YAANI MAFISADI AMBAO WAMELIINGIZIA NA BADO WANAEDELEA HASARA KUBWA TAIFA LETU.Mimi ningependa kuchangia kwa kusema kuwa kwa hatua ya nchi iliyopo sasa inahitaji viongozi makini ambao ninyi mmewaita ni wendawazimu kama kina Nape Mnauye ambao hufichua maovu na kubuni majawabu sahihi ya nini kifanyike kutatua matatizo yaliyopo.Yaani haitakiwi kabisa kuendeleza usiri ambao mtu akiubainisha mnasema eti amesema uongo,kwa hiyo mnamuazibu.Tukikumbatia hili chama na nchi kitazidi kubomoka kila siku kwa kuendeleza uwepo wa makundi.Nimeyasema haya baada ya kufuatilia kwa ukaribu na kwa makini hoja na maelezo aliyoyanena kijana mwenzetu Nape Mnauye kuhusu ufisadi katika UVCCM.Cha msingi kilichokuwa kikitakiwa kama baraza la Uvccm ni kuangalia kwa umakini kuhusu hoja hiyo na kuchunguza kwa kufuatilia kwa ukaribu zaidi kuhusu ufisadi huo badala ya kukurupuka na kutangaza ktk vyombo vya habari kuwa Nape amechukuliwa hatua kadha wa kadha.Kwa kufanaya hivyo ni kutounga jitihada za Raisi ktk kupambana na ufisadi.Hala hala watanzania tunatakiwa kuunga mkono juhudi za Rais za kuhakikisha kuwa tunauondoa ufisadi ktk chama na sio kuwaondoa watu wanaofichua siri za ufisadi ktk chama au nchi.Jambo hili ndilo Rais wetu anapigania kila siku kuhakikisha anaondoa ufisadi ktk chama ili kuwafanya wananchi wazidishe imani naye na kumpatia kipindi kingine cha miaka mitano Rais wetu mpendwa.Kwa muono wangu kauli zilizotolewa na kina Makamba na kina Nchimbi nimeziona kama zilikuwa zinataka kuvuruga zaidi chama na pengine kuharibu jitihada za Serikali ktk malengo yake ya baadae. Pia nikijaribu kufikiria kauli ya Nchimbi kwa undani kuwa ktk umoja wa vijana kuna wendawezamu,hii haingii akilini kabisa.Kwa sababu Nchimbi kama mwana MWANACHAMA WA UVCCM anatakiwa aangalie mbele na nyuma kwa kutilia mkazo usemi unao sema kuwa ujana ni maji ya moto.Hii ikimaanisha kuwa ujana ni sehemu ya wenda wazimu uliona na muono/malengo ya mafanikio hapo baadae.Nchimbi amesahau kuwa uwendawazimu alionao Nape ni ule wa uwezo uwezo wake wa kujenga hoja zinazo washawishi wananchi katika mambo ya maendeleo.Hasa ukizingatia kuwa mambo hayawezi kwenda pasipo uwepo wa watu wanao weza jenga hoja.Kwa kweli hii ilinisononesha sana tena sana ,eti kwa wenda wazimu huu walio uona wao ndio unapendekeza avuliwe uanachama .Kwa kweli naweza sema kuwa Mhe. Nchimbi hatutakii mema sisi vijana na UVCCM kwa ujumla tena inaonesha kuwa kama mwanasiasa uwezo wake wa kujenga hoja anatakiwa aungalie zaidi .Nilidhani angejenga hoja kuwa kwa nini wanapendekeza Nape avuliwe uanachama na sio kufuata morali za wajumbe wachache waliohudhuria kikao kile.

Big up Rais Kikwete kwa kufutilia mbali mapendekezo ya baraza lile.Hii ni changamoto kwao kwa siku nyingine kuwa wawe makini ktk maamuzi yao.Sio kuwaonea tu watu walio na uzalendo na nchi yetu.

Wako,
Mdau -SWEDEN