Friday, September 05, 2008

ZOMBE LEO


Washtakiwa wakitoka mahakamani kurejea rumandebaada ya kesi kuisha.


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam jana ilielezwa kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi, alimuita mshtakiwa wa 12, Koplo Rajabu Bakari katika kesi hiyo na kumpangia maelezo kwenye karatasi ili akayaeleze kwenye tume ya Jaji Kipenka iliyoundwa na rais kuchunguza tukio la mauaji hayo.
Shahidi wa 31 katika kesi hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Omar Amir Omar (48), aliieleza mahakama kuwa, yeye alikuwa mmoja wa watu walioteuliwa kupeleleza tukio hilo na kwamba aliwahoji washtakiwa wanne.
ASP Omar ambaye anafanya kazi Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Koplo Emmanuel Mabula (mshtakiwa wa 7), Koplo Felix Cedrick (mshtakiwa wa 8), Koplo Rashidi Lema (mshtakiwa wa 11) na Koplo Rajabu Bakari (mshtakiwa wa 12).
Alidai kuwa, wakati anamhoji Koplo Rajabu Bakari alimweleza kuwa, siku ya tukio alipangiwa kufanya doria eneo la Mwananyamala na kwamba, wakati anarudi ofisini katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, majira ya jioni alikutana Bageni ambaye alimweleza waende Sam Nujoma kwenye tukio la ujambazi la Kampuni ya Bidco.
Alidai walifika Sam Nujoma saa 12.30 jioni na kwamba aliiona pick-up ya Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa na watu wanne waliokuwa wamelazwa chini.
Shahidi huyo alidai kuwa, wakati mshtakiwa huyo wakiwa katika eneo hilo la Sam Nujoma, Bageni aliwahoji watu wanne ambao walikuwa ni wafanyakazi wa Kampuni ya Bidco; na kwamba baada ya kumaliza askari waliokuwa kwenye gari la Chuo Kikuu walishuka na kuingia kwenye gari aina ya ‘Defender’.
ASP Omar ambaye anashughulikia upelelezi wa kesi zinazohusiana na makosa ya jinai,
alidai baada ya kuingia kwenye gari, Bageni aliamuru gari ielekee upande wa Ubungo na kwamba walienda hadi kwenye Msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis wilayani Kinondoni, kulikotokea mauaji hayo.
Alidai wakati wakiwa barabarani, Bageni alikuwa akizungumza kwa simu yake huku akijibu; ‘Ndio afande’.
Alidai walipofika katika msitu huo yeye (mshtakiwa wa 12) alikuwa akiongea na ‘redio call’ kuhusu tukio la ujambazi lililotokea Kijitonyama na kwamba alishtuka baada ya kusikia mlio wa risasi, lakini hakushiriki katika kuwaua wafanyabiashara hao.
Alidai baada ya tukio hilo, maiti zilipakiwa kwenye ‘defender’ na kupelekwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alidai walipofika katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, Makelle na Bageni walishuka na kuingia ofisini huku akiwa amebeba mkoba mweusi na kwamba baada ya muda Zombe naye alifika na kuingia katika ofisi hiyo.
Shahidi huyo, alidai mshtakiwa alimweleza kuwa siku tatu baada ya tukio hilo kutokea aliitwa kwenye tume ya Jaji Kipenka iliyoundwa na rais kuchunguza mauaji hayo.
Alidai kabla hajaenda katika tume hiyo, Zombe alimuita ofisini kwake na kumpa maelezo kwenye karatasi ya jinsi atakavyokuwa akiijibu tume hiyo, wakati akihojiwa.
Baadhi ya mahojiano baina ya wakili wa serikali Angaza Mwipopo na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Mwipopo: Machi 3, mwaka 2006 ulifanya nini?
Shahidi: Nilimhoji mshtakiwa wa 12 Koplo Rajabu Bakari.
Wakili: Ulichukua muda gani?
Shahidi: Si zaidi ya saa 2.30.
Wakili: Alikueleza nini?
Shahidi: Alinieleza kuhusu tukio la mauaji lililotokea Msitu wa Pande na lile la kwenda kufyatua risasi katika machimbo ya mchanga yaliyoko Bunju.
Wakili: Ulifahamu ni lini Bakari alifikishwa mahakamani?
Shahidi: Sikumbuki kwa sababu baada ya kumaliza kuchukua maelezo yake niliendelea na shughuli zangu nyingine.
Wakili: Machi 6, mwaka 2006 ulikuwa wapi?
Shahidi: Nilikuwa ofisini.
Wakili: Je, kitu gani kilitokea?
Shahidi: Mama Mkumbi ambaye alikuwa kiongozi wa timu yetu alitueleza kuwa ataletwa mshtakiwa wa 11 ili tuweze kumhoji.
Wakili: Je, aliletwa?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Je, kitu gani kiliendelea?
Shahidi: Alianza kuhojiwa na akasema amekuja ili aweze kutueleza ukweli wa tukio zima lilivyotokea.
Wakili: Ni ukweli upi
Shahidi: Ukweli juu ya tukio la mauaji ya wafanyabiashara lilivyotokea.
Baada ya mahojiano hayo wakili Mwipopo aliiomba mahakama ikubali kupokea maelezo ya washtakiwa wa 11 na 12 ili yawe kielelezo katika kesi hiyo, lakini mvutano mkali uliibuka baina ya mawakili wa upande wa utetezi na mahakama.
Jaji Kiongozi Salum Masatti alimuuliza Wakili Denis Msafiri wa upande wa utetezi kama analo pingamizi kuhusiana na maelezo ya mshtakiwa wa 11 kutolewa kama kielelezo na wakili huyo alimwonyesha mshtakiwa ambaye aliyakubali na kusema kuwa hana pingamizi.
Hata hivyo, Wakili Majura Magafu alipinga maelezo hayo kutolewa katika mahakama hiyo, kwa madai kuwa yana mapungufu kisheria.
“Sisi tunapinga kupokewa kwa maelezo hayo mahakamani kwa sababu hayajitoshelezi na yanaweza kuleta maswali mengine kwamba mtu huyu alikuwa amepangwa kwa ajili ya kuwamaliza wenzake,” alisema Wakili Majura.
Naye Wakili Dieneus Ishengoma alipinga maelezo ya mshtakiwa wa 12 kupokewa katika mahakama hiyo, kwa madai kuwa yanawagusa washtakiwa wengine.
“Mtukufu Jaji kwa mujibu wa kifungu cha 33, kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya ushahidi maelezo haya ni kama ungamo, sisi tunapinga kupokewa kwa sababu kuna mapungufu wakati wa kuandika maelezo haya,” alisema Wakili Ishengoma.
Wakili wa Serikali Mwipopo akijibu hoja za mawakili hao wa upande wa utetezi alidai kuwa hoja zao si za msingi kwani hata washtakiwa wenyewe wameyakubali maelezo yao.
“Hoja zao si za msingi wanaona ushahidi unaanza kuwa mzito, wanaanza kuhangaika,” alisema Wakili Mwipopo ambaye anaiwakilisha Serikali.
Jaji Masatti baada ya kusikiliza hoja zote alitupilia mbali hoja za mawakili hao wa upande wa utetezi na maelezo hayo yalipokewa katika mahakama hiyo kama kielelezo.

“Ni mtuhumiwa pekee anayejua ukweli na kisheria maelezo ya mshtakiwa hayawezi kugusa washtakiwa wengine kama hakuna ushahidi mwingine unaounga mkono maelezo hayo,” alisema Jaji Masatti.
Awali, ilidaiwa katika mahakama hiyo, kuwa washtakiwa hao kwa pamoja Januari 14, mwaka 2006 katika Msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis wilayani Kinondoni waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini ambao walikuwa wakazi wa Mahenge mkoani Morogoro pamoja na dereva wa teksi, mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Wafanyabiashara hao ni Ephraim Sabinus Chigumbi, Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo, Mathias Lunkombe na dereva wa teksi Juma Ndugu.
Watuhumiwa wengine mbali ya Zombe ni SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, F.5912 PC Noel Leonard, WP 4593 PC Jane Andrew, D6440CPL Emmanuel Mabula, E6712 CPL Felix Cedrick, D8289 PC Michael Sonza, D 2300CPL Ebeneth Saro, d9312D/C Rashid Lema, D4656 C/CPL Rajab Bakari na D.1367 D/CPL Festus Gwabisabi.
.......E&P....2008/09/04

No comments: