Saturday, September 06, 2008

ZOMBE LEO

Ushahidi wa picha dhidi ya Zombe watupwa Wananchi wakitoka kusikiliza kesi ya polisi kuua wafanyabiashara jana.

MAHAKAMA Kuu imekataa kupokea kielelezo cha picha ili kitumike katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa Mahenge, mkoani Morogoro na dereva teksi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, (ACP) Abdallah Zombe na wenzake 12.
Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya shahidi wa 32 katika kesi hiyo, Sajini Moja Kabenga (38), ambaye anafanya kazi katika kitengo cha picha kilichoko Makao Makuu ya Upelelezi kuanza kutoa ushahidi wake.
Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa alikuwa ni mmoja wa watu waliokwenda katika msitu wa Pande ulioko Mbezi Loius, na Bunju kwenye mashimo ya mchanga, wilayani Kinondoni na kwamba alipiga picha za mnato kwenye maeneo hayo.
Shahidi huyo, akihojiwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali Mugaya Mutaki, alieleza mahakama hiyo kuwa alipiga picha eneo linalodaiwa kutokea mauaji ya wafanyabiashara wanne na dereva teksi na kuchora ramani ya eneo hilo.
Shahidi huyo alidai pia kuwa alipiga picha za maganda mawili ya risasi yaliyookotwa katika msitu wa Pande.
Pia shahidi huyo aliwaacha hoi watu waliokuwepo katika mahakama hiyo, baada ya kuieleza mahakama kuwa hana utaalamu wa kuchora ramani na kwamba alishtukizwa achore baada ya kwenda kwenye eneo husika.
“Mimi hata bunduki siwezi kuitumia japokuwa nilipata mafunzo na bunduki yangu kwa sasa ni kamera na hata utaalamu wa kuchora ramani sina,”alisema Sajini Kabenga na kuzua kicheko katika mahakama hiyo.
Wakili wa serikali Mutaki aliiomba mahakama ipokee vielelezo vya picha na ramani ili vitumike katika kesi hiyo, lakini upande wa utetezi ulipinga kwa madai kuwa vilikuwa na mapungufu.
“Sisi tunapinga picha hizo na ramani visipokelewe mahakamani kama vielelezo katika kesi hii kwa sababu upande wa mashitaka haukuwahi kutueleza kama kutakuwa na vielelezo kama hivyo katika kesi hii,” alisema wakili Majura Magafu.
Akijibu hoja hiyo, wakili wa serikali Mutaki alisema kutokana na kifungu namba 246 kifungu kidogo cha sheria za jinai si lazima kuorodheshwa kila kitu kitakachowasilishwa mahakamani.
Wakili Magafu alisema kuwa kifungu hicho hakiishii kusema maneno tu, bali kinaeleza kwamba vitu vinavyotarajiwa kuwasilishwa mahakamani kama vidhibiti lazima vitajwe.
Jaji Kiongozi Salum Masatti baada ya kusikiliza hoja zote, alikubali kielelezo cha ramani kipokelewe kuwa kidhibiti katika kesi hiyo, lakini alikataa kielelezo cha picha.
Sehemu ya mahojiano baina ya mawakili Mutaki, Jerome Nsemwa, Gaudiosus Ishengoma, Magafu na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Mutaki: Ulipiga picha za namna gani?
Shahidi: Picha za mnato.
Wakili: Ulipiga sehemu zipi?
Shahidi: Nilipiga picha sehemu zote ambazo mshitakiwa wa 11 Rashidi Lema alikuwa akizionyesha kule tulikokwenda na kuchora ramani.
Wakili: Ulipata picha ngapi?
Shahidi: Picha 24.
Wakili: Baada ya kumaliza ulifanya nini?
Shahidi: Niliandika maelezo na mkanda wa picha nilimkabidhi kiongozi wangu.
Wakili Jerome Nsemwa: Katika upigaji picha, uliwahi kukutana na mshitakiwa wa kwanza?
Shahidi: Hapana.
Wakili Gaudiosus Ishengoma: Katika msitu wa Pande kulikuwa na umbali gain kutoka barabarani hadikulikolazwa miili ya marehemu?
Shahidi: Ni kama hatua moja.
Wakili: Je wewe ni mtaalamu wa kuchora ramani?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Utakubali kwamba hii ramani yako haitupi uhalisi wa yale yaliyotokea katika msitu wa Pande?
Shahidi: Hilo siwezi kulijibu.
Wakili: Utakubali kwamba kukosa kwako uzoefu hata hiyo, ramani ina mapungufu?Shahidi: Siyo kwamba sikuwa na udhoefu yaani sijui kabisa.
Wakili Majura Magafu: Katika msafara wenu wapiga picha mlikuwa wangapi?
Shahidi: Tulikuwa wawili mimi na Sajini Elly aliyekuwa akipiga picha za video.
Wakili: Nani alikuambia uchore ramani?
Shahidi: Sajini Elly.
Wakili: Kitu gani kilikufanya usimwambie Sajini Elly kwamba hujui kuchora ramani?
Shahidi: Kwasababu ni bosi wangu hivyo lazima nitekeleze amri.
Wakili: Je, hiyo ndiyo amri ya polisi?
Shahidi: Ndiyo, unatekeleza amri ya bosi wako.
Wakili: Kwa hiyo hata bosi wako akikuambia kitu ambacho kiko nje ya taaluma yako huwezi kumshauri?
Shahidi: Nilimshauri akasema nichore.
Wakili: Je, uliwaeleza wakubwa wako wengine, uliokuwa nao siku hiyo?
Shahidi: Sikuwaeleza kwasababu nilikuwa natekeleza amri halali.
Wakili: Utakubaliana nami kwamba taratibu za kijeshi zinakutaka utekeleze amri halali, je hiyo ilikuwa amri halali?
Shahidi: Ndiyo ilikuwa amri halali.
Mshauri wa baraza Magreth Mosi: Je, jukumu la kuchora ramani uliwahi kuambiwa kabla au ulishtukizwa kwenye tukio?
Shahidi: Nilishtukizwa pale pale kwenye tukio.
Mshauri: Eneo la msitu wa Pande udongo wake ukoje?
Shahidi: Sijui.
Jaji Kiongozi Masatti baada ya kusikiliza hoja zote aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 22 mwaka huu mashahidi wa upande wa mashitaka watakapoendelea kutoa ushahidi.
Katika tukio jingine nje ya Mahakama baadhi ya ndugu wa Zombe waliwajia juu waandishi wa habari wakihoji kwanini ndugu yao anaandikwa kila siku na kupigwa picha.
Tukio hilo lilitokea jana nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam baada ya gari lililokuwa limewabeba washitakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo kuondoka katika mahakama hiyo.
Baadhi ya ndugu hao, walisikika wakisema kuwa wamechoshwa na tabia ya baadhi ya waandishi kumuandika ndugu yao kila siku na kwamba kila mtu anakosea kama binadamu.
“Hawa waandishi wa habari wabaya sana kila siku Zombe tu wakati kama ni kukosea kila mtu anakosea,” walilalamika ndugu hao, kwa nyakati tofauti.
Huku wakionekana kuwa na jazba ndugu hao, walisikika wakilalamika kuwa hata picha za ndugu yao zimekuwa zikitawala kwenye vyombo vya habari kuliko za washitakiwa wengine.

No comments: