Tuesday, February 17, 2009

KESI YA ZOMBE


Makelle ambebesha lawama Zombe

MSHITAKIWA wa tatu katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro na dereva teksi wa Manzese, Ahmed Makelle ameileza Mahakama Kuu kuwa mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi mkoani Dar es salaam, ndiye aliyembambikia kesi hiyo.
Makelle, ambaye ni mrakibu msaidizi wa polisi, ASP, na ambaye pia ni shahidi wa tatu wa upande wa utetezi katika kesi hiyo, alitoa shutuma hizo dhidi ya kamishna huyo msaidizi wa polisi jana wakati akihitimisha ushahidi wake mahakamani hapo kwa kuhojiwa na mawakili wa serikali na mawakili wa washitakiwa wengine.
Baada ya Makelle kumaliza kutoa ushahidi wake jana, mwanamke pekee kwenye kesi hiyo, Jane Andrew, ambaye ni mshtakiwa wa nne, leo ataanza kutoa maelezo yake akiongozwa na mawakili wa upande wa utetezi.
Jana wakati wa kuhitimisha ushahidi wake, Makelle alisema Zombe, ambaye pia alikuwa akikaimu nafasi ya kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, RPC, wakati wa mauaji hayo, alipeleka taarifa ya uongo kwenye Tume ya Rais ya kuchunguza vifo hivyo iliyokuwa chini ya Jiji Mussa Kipenka.
Makelle alisema taarifa aliyoipeleka Zombe si ile aliyoitoa yeye kwenye chumba cha mawasiliano (control room) kuhusu tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha wa kampuni ya Bidco na kwamba taarifa ya Zombe imesababisa yeye ashtakiwe.
Baada ya kumhoji jinsi alivyopata taarifa na kwenda hadi eneo la tukio, Wakili Mtaki alihamia kwenye kielelezo ambacho alimtaka Makelle akitambue na kuendelea na mahojiano kama ifuatavyo:
Mtaki: Kuna kielelezo hapa mahakamani,…
Jaji: Kabla hujaenda huko hebu shahidi kwanza atusaidie, ulisema uliona begi, lilikuwa ni begi gani?
Makelle: Lilikuwa begi dogo hivi.
Jaji: Briefcase?
Makelle: Hapana haikuwa briefcase lakini ni begi ambalo unaweza kuweka document (nyaraka).
Jaji: Lakini lenye zipu
Makelle: Ndio.
Jaji: Lilikuwa la rangi gani?
Makelle: Rangi sijui ya kahawia nyeusi yaani kama kahawia nyeusi ila inaelekea kwenye nyeusi.
Mtaki: Hapa kuna kuna kielelezo hiki hapa hebu kiangalie na uiambie mahakama ni nini (anasema Mtaki na kumkabidhi Makelle faili).
Makelle: Ni maelezo ya ACP. Zombe kuhusiana na tukio la Bidco (alisema Makelle baada ya kuliangalia na kisha kuanza kuisoma taarifa hiyo).
Taarifa hiyo ambayo sehemu yake inasomeka kuwa akiwa ofisini akiendelea na kazi huku radio call yake ikiwa hewani alimsikia Makelle kwenye call sign moja, tano, nane akisema kuwa wamepambana na majambazi wamewajeruhi na kwamba wamepata bastola moja na fedha taslimu Sh.5 milioni.
Mtaki: Maelezo haya ni sahihi?
Makelle: Usahihi unategemea na aliyeyaeleza hayo maelezo. Mimi siwezi kujua.
Mtaki: Kama mwandishi ndo anajua unasema alikusingizia?
Makelle: Tena sana tu.
Mtaki: Una sababu yoyote mshtakiwa wa kwanza akusingizie?
Makelle: Kama RCO wangu sikuwa na tatizo naye, sasa sijui kwa nini aliamua kuandika maelezo kama hayo.
Mtaki: Kwa kuwa umekubali kuwa ulitangaza redioni na kwamba uliyosema si haya ni nini uliyotangaza?
Makelle: Mimi nilisema watu wanne wamekamatwa na askari wa Chuo Kikuu na pesa zinazokadiriwa kuwa Sh.5 mil na bastola na nimewaagiza wawapeleke kituoni kwao kwa mahojiano. Mtukufu Jaji hayo ndio nilijulisha control room.
Mtaki: Hebu tusaidie kituo cha Polisi Urafiki kiko katika wilaya gani ya Kipolisi?

Makelle: Mtukufu Jaji kiko katika wilaya ya Magomeni.

Mtaki: Na Chuo Kikuu?

Makelle: Kiko Kinondoni.

Mtaki: Eneo walilokamatwa hao suspect liko Magomeni au Kinondoni?

Makelle: Liko Kinondoni.

Mtaki: Katika ushahidi wako juzi ulisema vielelezo vya bastola na pesa vilikuwa katika kituo cha Urafiki, hebu ieleze mahakama vipi vielelezo vya Kinondoni vije Urafiki na watuhumiwa waende Chuo Kikuu ambako ni Kinondoni

Makelle: Mheshimiwa Jaji mimi sijui ni kwa nini ilikuwa hivyo.

Mtaki: Tukio la Bidco ulilishuhudia kwa namna yoyote?

Makelle: Nilijulishwa tu kuwa nifuatilie.

Mtaki: Pale Ubungo Terminal ulikaa muda gani?

Makelle: Sikukaa, lengo lilikuwa ni kuwadrop tu askari wangu.

Mtaki: Ulisema kutoka hapo ulikwenda kwenye kituo kidogo cha polisi karibu na Usafirishaji Mabibo, je, hapo ulikwenda kufanya nini?

Makelle: Kuangalia kazi za kawaida.

Mtaki: Ulikaa muda gani?

Makelle: Sikukaa, nilisimama nikaongea nao tu nikaondoka.

Mataki Ulifika Urafiki saa ngapi?

Makelle: Kati ya saa 1.30 na saa2.00

Mtaki: Ulikuta taarifa gani?

Makelle: Niliteremka nikamkuta OCD kisha nikaingia ofisini baada ya kumsalimia.

Mtaki: Ile gari ya polisi iliyoondoka na watuhumiwa uliikuta pale Urafiki?

Makelle: Hapana sikuikuta.

Mtaki: Kesho yake uliona nini?

Makelle: Niliona ile gari saloon

Mtaki: Ambayo niliiona kwenye tukio?

Makelle: Ndio ilikuwa kwenye parking.

Jaji: Gari ya nani?

Makelle: Gari ya wale suspect ambayo niliiona kule Sinza.

Mtaki: Labda tusaidie ASP Makelle hii gari ilikamatwa kwenye tukio la Kinondoni vipi nayo iletwe Urafiki?

Makelle: Mimi sijui maana hata faili sikuletewa kwa hiyo sijui ni kwa nini OCS alikubali kuvipokea.

Mtaki: Mshtakiwa wa kwanza alifika pale muda gani?

Makelle: Kama dakika 40 hivi baada yangu.

Mtaki: Alikuja kwa nini?

Makelle: Siju nilimuona tu wakiongozana ofisini kwa OCS.

Mtaki: Nani na nani?

OCD, mshtakiwa wa kwanza na SP Mkumbo.

Mtaki: Nilikuuliza mshitakiwa wa kwanza.

Makelle: Samahani Mheshimiwa Jaji nilichanganya alifikia kama dakika 40.

Mataki: Mshitakiwa wa pili naye alifika ?

Makelle: Yah alianza kufika yeye.

Mtaki: Ulijua mshtakiwa wa pili alikuja kufanya nini?

Makelle: Nilijua alikuja kuchukua vielelezo.

Mtaki: Ni kwa nini alikataa kupokea?

Makelle: Alidai pesa alizotumwa na OCD Matage zilikuwa ni pungufu.

Mtaki: ASP Makelle uliweza kujua kiasi cha pesa za tukio la Sinza?

Makelle: Sikuzitambua kwani hapakuwa na discussion.

Mtaki: Haikukugusa akilini kuwa kule Sinza zilitajwa Sh.5mil. na pale zikatajwa Sh.5mil.

Makelle: Nilihisi hivyo.

Mtaki: Hivi zilikuwa kwenye nini?
Makelle: Hizi zilikuwa kwenye begi.
Mtaki: Hilo begi linafanana na uliloliona Sinza?
Makelle: Lilikuwa linafanana.
Mtaki: Kama lilifanana haikugusa akili
Makelle: Ndo maana nilisema nilihisi, lakini kwa sababu nilitoa maelekezo na sikusikia malekezo mengine kwa sababu Dar kulikuwa na matukio mengi.
Mtaki: Umeieleza mahakama kuwa Sinza askari walitaka kukukabidhi pesa za watuhumiwa ukakataa, sasa hapa Urafiki ulikutana na begi hilo je kulikuwa na askari yeyote aliyezileta?
Makelle: Hapana hawakuwepo waliondoka nazo.
Mtaki: Mkutano wenu pale Urafiki ulichukua muda gani?
Makelle: Haikuchukua muda kwani baada ya mshtakiwa wa kwanza kukasirika na kutoa agizo kwa OCD Matage zipatikane zilizopungua aliondoka na zilizobaki alipewa mshitakiwa wa pili akaondoka nazo nami nikaendelea na kazi zangu.
Mtaki: Mshtakiwa wa kwanza alifanya juhudi zozote za kujua watuhumiwa wako wapi?
Makelle: Hapana yeye alichouliza ni pesa tu.
Mtaki: Kuna maelezo yanasemekana ni yako, je uliandika maalezo yoyote?
Makelle: Wapi?
Mtaki: Kwenye timu ya Mgawe.
Makelle: Hapana.
Mtaki: Haya maelezo ni yako? aliuliza huku akimpa file akalisoma.
Makelle: Si yangu (alijibu baada ya kuyaangalia).
Mtaki: Mama Mkumbi ni afisa wako mkubwa uliwahi kuwa na ugomvi naye?
Makelle : Hapana.
Mtaki: Na Mgawe je?
Makelle: Yeye ndoo alikuwa bosi wangu na sikuwahi kuwa na ugomvi naye.
Wakili wa Zombe, Jerome Msemwa: Hapa kuna barua ambayo uliiandika ukiwa gerezani kwenda kwa DPP
Makelle: Sijawahi kuandika barua.
Msemwa: Uliwahi kushikwa na simu gerezani?
Makelle: Kushikwa vipi nikiwa nimeiba?


Msemwa: Uliwahi kushikwa na simu yenye vocha ya Sh235,000 ?
Mkalle: Sijawahi
Wakili Gaudioz Ishengoma: Shahidi unakumbuka wakati mshtakiwa wa kwanza akitoa ushahidi hapa alikutaja kama mmoja wa watu walioandika barua kutoka gerezani kwenda kwa DPP?
Makelle
: Alinitaja ndio.
Ishengoma: Hii ni barua inasemekana ni yako imeandikwa na nani (alimkabidhi faili)
Makelle: Imeandikwa na Ahmed Makelle.
Ishengoma: Imeandikwa tarehe ngapi?
Makelle: Imeandikwa tarehe 9 /6/2006.
Ishengoma: Ilifika kwa DPP lini?
Makelle: Tarehe 12/6/2006


Ishengoma: Kwa hiyo nitakuwa sahihi kusema kwamba haya mliyomwandikia DPP ndio yaliyomfanya mshtakiwa wa kwanza ashtakiwe?
Jaji: Huo ni uamuzi wa DPP yeye mshitakiwa wa kwanza anaamini hivyo sasa unataka na yeye(Makelle) aamini hivyo swali lako ni nini?
Ishengoma: Mshtakiwa wa kwanza anaamini kuwa haya ndio yaliyochangia yeye ashtakiwe.
Jaji: Hiyo ni imani yake.
Ishengoma: Sambamba na haya anayoyaamini ni na ushahidi ulioutoa hapa, wewe unasemaje?
Makelle: Ushahidi uko wazi, silaha za urafiki hazikutumika kwa hiyo inaonekana huyo mtu (Zombe) kaniletea mzigo mbaya sana. Kanibambikia kesi kwani yeye ndio alipeleka information makao makuu na ndiye alikwenda Tume ya Kipenka na ndo kaandika kitu cha uwongo.
Ishengoma : Huyu?
Makelle: Eh huyo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi itakapoendelea tena leo mahakamani hapo.

No comments: