Tuesday, March 31, 2009

AJALI YA TRENI


Majeruhi wa ajali ya treni mkoani Dodoma wakipatiwa matibabu baada yakuhamishiwa hospitali ya General ya mkoa wa Dodoma jana.

POLISI mkoani Dodoma inawashikilia watu sita ili kwa tuhuma za uzembe na kusababisha ajali ya treni iliyoua watu saba na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 10:45 alfajiri katika kitongoji cha Pandambili katika Kijiji cha Msagali wilayani Mpwapwa umbali wa kilomita chache kutoka ilipotokea ajali kubwa ya treni mwaka 2002 na kupoteza maisha ya zaidi ya watu 200.
Akizungumza ofisini kwake mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni mkuu wa mkoa William Lukuvi alisema kuwa watu hao wanashikiliwa kutokana na uchunguzi wa awali kubaini kuwa ajali hiyo haikuwa ya bahati mbaya bali ilitokea kutokana na uzembe wa wafanyakazi wa TRL wakiwemo madereva.
Lukuvi alisema wamebaini kuwa treni ya mizigo haikuwa na hitilafu yoyote ambayo ingelazimisha kusimama katika eneo lolote na kwamba katika mahojiano na baadhi ya watu wanaoishi katika maeneo hayo ilibainika kuwa treni hiyo ilisimama ili kupakua mizigo ya wizi ikiwemo mafuta.
Alisema kuwa wananchi waliofika katika eneo la tukio walieleza kuwa mahali hapo pamekuwa ni kituo kikuu cha kufanya biashara za magendo kati ya wafanyakazi wa treni za mizigo na baadhi ya vijana ambao wanaendesha maisha yao kwa kutegemea zaidi biashara hizo.
Kwa mujibu wa Lukuvi kumekuwa na tatizo kubwa la wafanyakazi kutokuwa waaminifu na kwamba uongozi wa TRL wameshindwa kabisa kutumia njia za kisasa ili kuweza kuwabaini wabaya wao ambao wamekuwa wakilisababishia shirika hilo hasara ya mabilioni ya fedha.
Alisema wanaoshikiliwa na polisi ni pamoja na madereva wa treni zote mbili zilizosababisha ajali hiyo ,wasaidizi wao na wakuu wa stesheni za Gulwe na Igandu.

No comments: