Thursday, March 12, 2009

ALIYEMZABUA MWINYI

Kijana Ibrahim Said (26) atararajiwa kufika mahakamani leo kwa kumpiga kibao Rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amedaiwa kusema; kwa kitendo alichofanya, amefikisha ujumbe wake wa kuchukizwa na maelezo ya kuruhusu matumizi ya kondomu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, mtuhumiwa huyo anadaiwa kusema kuwa anajutia kitendo hicho kwani hakukusudia kumpiga Mzee Mwinyi kwani anampenda.
Kamanda Suleiman Kova aliwaeleza waandishi wa habari jana kuhusiana na tukio la Mzee Mwingi (maarufu kama Mzee Ruksa) kupigwa kibao na kijana huyo juzi akiwa anahutubia Baraza la Maulid wakati wa kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililohudhuriwa na waumini wengi wa dini ya Kiislam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Kamanda Kova alisema mahojiano na mtuhumiwa huyo aliyafanya mwenyewe juzi usiku na kumweleza kuwa hakuwa na nia ya kumdhuru, bali alitafuta kioja cha kufanya ili ujumbe wake wa kutaka viongozi wa dini wasisitize matumizi ya kondomu kwa waumini wao pamoja na kutoshabikia umoja katika kusherehekea sikukuu za Idd, Maulid, Pasaka na Krismasi.
“Mtuhumiwa huyo alisema viongozi mbalimbali wa dini waache kusisitiza matumizi ya kondomu kwani si njia sahihi na ni batili na potofu katika maadili ya kidini,” alisema Kova.
Hata hivyo watu mbalimbali walipinga kitendo cha kijana huyo kumpiga mzee Mwinyi kutokana na umaarufu wake na hata maadili aliyoonyesha wakati wa uongozi wake, ingawa baadhi walidai kuwa alikosea kusema juu ya kondomu kwenye hadhara ya waumini wa dini ya kiisilamu ambayo inakataza watu kufanya uzinzi.
Kamanda Kova alifahamisha kwamba, alipomhoji zaidi mtuhumiwa huyo kwa nini hakutafuta njia nyingine ya kufikisha ujumbe wake tofauti na kumchapa kibao; alisema alifanya hivyo kwa kuwa Mwinyi ni kiongozi anayependwa na kuheshimika zaidi hivyo kuamini kuwa kwa kufanya hivyo ujumbe wake utafika.
Akimnukuu kijana huyo Kova alisema: “Najuta kutenda kosa hilo kwa kuwa nampenda Rais Mwinyi, lakini ni njia sahihi ya kufikisha ujumbe huo,” alisema.

No comments: