Tuesday, March 03, 2009

JK AJA JUU




RAIS Jakaya Kikwete amesema ana majina ya watu wa kitengo cha maktaba cha Bandari ya Dar es salaam wanaofanya ufisadi unaolikosesha taifa mamilioni ya fedha na kuahidi kuyakabidhi kwa wahusika ili washughulikiwe.
Kikwete alisema hayo jana baada ya kufanya ziara ya kushitukiza kwenye Bandari ya Dar es salaam kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Januari 15 mwaka huu kwa wakuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA).
Alisema kitengo cha maktaba kimekuwa kikifanya mchezo mchafu bandarini hapo kwa kushirikiana na wasafirishaji na kwamba, vibarua vya watu wa kitengo hicho viko hatarini.
“Waambieni watu wa kitengo cha maktaba kuwa mchezo wao unajulikana na orodha ya majina yao inajulikana, lakini bado kuwaumbua tu,” alisema Kikwete baada ya kumaliza ziara yake.
“Ndugu zangu sitawataja hadharani wala kwenye magazeti, bali nitakachofanya nitawaletea orodha ya majina, muwafukuze kazi. Kama wameshindwa kazi tutaleta watu wengine ambao wako tayari kufanya kazi kwa uaminifu.”
Alisema watu hao wamekuwa wakiwasiliana na wasafirishaji na kufanya ujanja wakati wa kujaza fomu za makontena yanayoingia nchini kwa kuandika mizigo tofauti na ile iliyomo ndani ya makontena hayo, ili yasipitishwe katika mashine ya uchunguzi (scanner) na hivyo kukwepa kulipa kodi kubwa.
Alisema mchezo huo hufanywa kwa makusudi ili kuwalaghai watu wa kitengo cha T. Scaner kutochunguza mizigo hiyo kwa mashine yao wakiamini kuwa hayana mzigo wa maana.
“Fomu imeandikwa ndani kuna mitumba, lakini kontena likikaguliwa unakuta magari ya kifahari. Kazi hii inawatajirisha wao na kulitia umasikini taifa letu,” alisema Kikwete.
“Tunahitaji scanner za kisasa ambazo zitakuwa na uwezo wa kuona hata chupa iliyomo ndani ya kontena.
“Lakini nashangaa mambo haya nayajua mimi, ninyi hamna habari. Sijui mnafanyaje kazi lakini fanyeni kazi kwa bidii na msifanyie mazoea.”
Ujanja wa kupitisha mizigo kwa njia ambayo hailipishwi ushuru unaolingana na thamani halisi, imesababisha kuwepo kwa mawakala wengi ambao husaidia mipango ya kutoa mizogo bandarini na kujipatia fedha nyingi ambazo zilitakiwa kuingia kwenye makasha ya serikali.
Utitiri wa makampuni ya uwakala huo ulipungua baada ya serikali ya awamu ya tatu kuanzisha utaratibu uliozitaka kampuni hizo kuweka dhamana ya Sh10 milioni kabla ya kuruhusiwa kufanya biashara, lakini sasa yamerudi kwa nguvu kubwa.
Kuhusu msongamano wa meli za mizigo, makontena na magari bandarini, Rais Kikwete alimuweka kiti moto mkurugenzi wa TPA, Efraem Mgawe kwa kumuhoji maswali ya papo kwa papo.
Mgawe alithibitisha kuwa tatizo la msongamano halijaondoka na kuchukua ahadi ya kulishughulikia kabla ya ziara nyingine ya rais ndani ya miezi miwili.
Rais alitaka kujua idadi ya kontena na magari ambayo yapo bandarini na ni kwa muda gani yamekaa hapo, swali ambalo Mgawe alionekana kutokuwa na jibu lake.

2 comments:

Anonymous said...

MZEE WA SUMO NA WANANCHI KWA UJUMLA MH.RAIS ALIPOSEMA WATU WA MAKTABA AKUMAANISHA WAFANYAKAZI WA BANDARI SABABU KWANZA BANDARINI AKUNA MAKTABA,HAPA MH.JK ALIWALENGA WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA TISCAN ILIYOPO KTK MAJENGO YA MAKTABA GHOLOFA YA PILI,HAWA TISCAN WAMEPEWA TENDA NA SERIKARI YA KUFANYA MAKADILIO YA KODI NA KUKAGUA MIZIGO KWA KUTUMIA MASHINE MAARUM ZA MIONZI SCANER,SASA BAADHI YA WAFANYAKAZI WA HII KAMPUNI UFANYA MAELEWANO NA BAADHI YA IMPORTES WAKUBWA NA KUZIHUJUMU FOMU ZA MAKADILIO YA USHURU ZINAZOITWA PCVR KWA MAELEWANO YA PESA KATI YA MILION 4-5 KWA FOMU MOJA NA HAWA IMPORTES ULIPIA USHURU MDOGO KWA KUONESHA KIWANGO KIDOGO CHA THAMANI ZA BIDHAA,HUU NI MCHEZO MCHAFU ULIOANZA MUDA MREFU SANA TRA WALIUFUMBIA MACHO TUASHUKURU KAMA MZEE WETU JK YAMEMFIKIA NA NI VYEMA WAFANYAKAZI HAO WAKAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUUJUMU UCHUMI WA NCHI HII MASIKINI KWA MFANO RAISI NI KWAMBA KAMA MZIGO ULITAKIWA KIRIPIWA MILIONI 18 MTU ANAWEZA KURIPIA MILIONI 6 NA SELIKARI KUKOSA MILIONI 12 SABABU YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE AMBAO KWA SDASA NI MATAJIRI WAKUBWA BY MDAU.

Anonymous said...

bandari uozo umezidi..ona sasa vipusa hivi hawakuviona>????

au scanner yao mbofu mbofuuuuuuuuuuuuuuuu

http://www.saigon-gpdaily.com.vn/National/2009/3/69066/