Thursday, June 18, 2009

SERIKALI YAUFYATA MISAMAHA


SERIKALI imeondoa pendekezo lake la kufuta msamaha wa kodi kwa bidhaa zote zinazonunuliwa na masharika ya dini na taasisi zake kama ilivyotangazwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo wakati akisoma bajeti ya serikali kwa mwaka 2009/10. Taarifa hiyo imetolewa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa madhehebu ya dini yenye nguvu na ushawishi kwa Watanzania usiku wa kuamkia jana. Akitangaza uamuzi huo mjini hapa jana kwa waandishi wa habari, Pinda alisema serikali imekubaliana na mawazo ya viongozi hao na kwamba, katika mkutano huo serikali imekubali iwepo mbinu na mkakati sahihi kati ya pande mbili hizo ili kudhibiti uvujaji wa mapato kwa wachache wanaotumia vibaya misamaha hiyo. “Nimewaiteni, kuzungumzia hili jambo la msamaha wa kodi kwa madhehebu ya dini, jana (juzi) tulikuwa na mkutano na viongozi wa dini kujadili juu ya msamaha wa kodi,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: “Walikwepo maaskofu kama Mokiwa (Valentino), ndugu yangu Mwamasika na mashehe wawili, tumewaeleza maoni yetu nao wakaeleza ya kwao, tukakubaliana nao kwani tunafahamu na kuthamini sana msaada wa wenzetu katika huduma za afya, elimu, maji na nyingine”. Waziri Mkuu aliongeza kwamba, baada ya mazungumzo hayo walikubaliana kwamba, misamaha katika mambo yote ikiwemo vifaa vya ujenzi wa nyumba za ibada, magari ya viongozi wa dini, huduma za madhehebu na nyingine iendelee kama kawaida. Alifafanua kwamba, baada ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam jana, alikubaliana na uamuzi huo wa mkutano wa pande zote mbili. Pinda alipoulizwa uko wapi msimamo wa serikali kutokana na uamuzi huo ambao unaonekana kugeuza maamuzi ya wataalamu, alisema: “Ahaa…wao ni viongozi, na sisi ni serikali”. “Serikali inapaswa kusikiliza raia, huu ndiyo utawala bora, si kwamba kuna udhaifu wowote, …wakati mwingine tungeweza kusema tuendelee na msimamo, lakini tumeangalia hawa ni wenzetu na wadau muhimu kimaendeleo,” alisisitiza Waziri Mkuu. Pinda alisema uamuzi huo wa serikali pia umeangalia kwa mapana haki za raia wengine wakiwemo malaika watoto wa nchi hii ambao wanaweza kuathirika kwa namna moja au nyingine kutokana na baadhi ya watu kutumia misamaha vibaya.

No comments: