Friday, May 30, 2008

UBORESHAJI WA SHERIA YA NDOA, MIRATHI NA URITHI
NA SHERIA MBALIMBALI ZA WATOTO


WAZIRI wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe amesema baada ya kuyatafakari mapendekezo ya Tume ya Kurekebisha Sheria na yale ya wadau mbalimbali juu ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria zinazogusa Mirathi na Urithi, Serikali imeamua kuandaa Waraka wa Serikali kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya namna bora ya kuboresha Sheria ya Ndoa na Sheria zinazosimamia Mirathi na Urithi.

Uamuzi huu umetokana na ukweli kwamba maeneo haya yanahusu mahusiano ya Kijamii na Kiutamaduni ikiwemo mila, desturi na imani za watu kwa upande mmoja na maendeleo ya Kijamii katika dunia ya sasa kwa upande mwingine. Ni masuala nyeti na muhimu na hivyo kuhitaji maoni yanayowakilisha mila, imani, desturi na jamii zote katika mchakato wa kuboresha sheria hizi.

Mchakato wa kuziboresha sheria hizi ulianza kwa Serikali kuiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya utafiti kuhusu Sheria zote zinazogusa maeneo haya matatu (Ndoa, Urithi na Mirathi) kutokana na sheria hizi kuwa na upungufu. Tume ilifanya utafiti na kutoa mapendekezo yake ambayo Serikali imeyatafakari na kuyatolea uamuzi.

Ikumbukwe kuwa tangu ilipopata Uhuru kutoka kwa Wakoloni mwaka 1961, Tanzania imekua ikifanya maboresho ya mfumo wa Sheria kwa lengo la kuboresha upatikanaji haki kwa Wananchi wote. Maboresho haya yamejumuisha kubadilisha vifungu vya Katiba na kurekebisha na kufuta Sheria mbalimbali kutokana na mabadiliko makubwa tunayoyashuhudia katika nyanja za Kisiasa, Kiuchumi, Kiutamaduni na Kijamii.

Vilevile, maboresho hayo yamejumuisha kuingiza Haki za Binadamu katika Katiba ya Nchi mwaka 1985 pamoja na kuridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayohusu Haki za Binadamu.

WAKATI HUOHUO, Serikali imeamua kuwa sheria zote zinazogusa watoto zifanyiwe marekebisho ya kawaida kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Kurekebisha Sheria na wadau mbalimbali kuhusu sheria husika badala ya kutunga sheria moja mpya inayowalinda watoto.

Hatua hii inafuatia Serikali kuzipitia kwa kina sheria zote zinazolinda maslahi na haki za watoto na kuona kuwa ingawa ni kweli kuwa sheria zinazogusa maslahi na haki za watoto zipo nyingi, lakini kila moja ya sheria hizi ni muhimu katika eneo lake na hivyo si vyema kuzifuta na kutunga moja. Badala yake, imeonekana ni bora maboresho yanayopendekezwa na Tume ya Kurekebisha Sheria na yale ya wadau yafanywe katika sheria zilizopo kwa nia ya kuziboresha ili hatimaye maslahi na haki za watoto zilindwe na kuboreshwa zaidi.

Sheria za Ndoa, Urithi na Mirathi zinagusa pia haki na maslahi ya watoto. Hivyo mchakato wa kuboresha sheria zinazowagusa watoto utaanza baada ya Serikali kukusanya maoni kuhusu sheria za Ndoa, Urithi na Mirathi kupitia Waraka wa Serikali.

Waraka huu wa Serikali unatarajiwa kutolewa katika mwaka ujao wa fedha ili kuipa Serikali fursa ya kuandaa bajeti kwa ajili ya zoezi hilo.

Baadhi ya sheria zinazofanyiwa maboresho zimedumu kwa miongo kadhaa na hivyo kuwa na upungufu. Serikali imedhamiria kuziboresha sheria mbalimbali zilizo na upungufu kwa lengo la kuuboresha mfumo wa upatikanaji haki na hivyo kuwaondolea kero wananchi.


Imetolewa na Wizara ya Katiba na Sheria,
S.L.P 9050,
Dar Es Salaam

Mei 26, 2008

No comments: