Tuesday, June 10, 2008

KASEJA

Kaseja akianguka saini mbele ya Madega.

JUMA Kaseja amesaini mkataba wa mwaka mmoja Yanga wenye thamani ya Sh milioni 57 kwa gharama zote ambao unamlazimisha Kocha wa Yanga, Dusan Kondic kumpanga mechi zote.
Mkataba huo wa mwaka moja ambao Mwanaspoti ilibahatika kuuona una masharti kadhaa na mmojawapo ni kumfanya Kaseja kuwa kipa namba moja katika klabu hiyo ya Jangwani.
Hiyo ina maana kwamba, Kondic hawezi kuwa na chaguo jingine zaidi ya kumpanga Kaseja kama inavyoonyeshwa katika mkataba huo.
Lakini pia hiyo ina maana kuwa kipa Ivo Mapunda sasa atakuwa hana nafasi tena ya kudaka isipokuwa tu kama Kaseja atakuwa ni majeruhi.
Kuna madai kuwa Ivo atachukuliwa na kocha wake wa zamani, Sredojevic Milutin 'Micho' katika kikosi chake cha St George cha Ethiopia.
Mkataba huo ambao una vipengele vizuri kadhaa kwa Kaseja unaonyesha kuwa utakwisha mara tu baada ya Ligi Kuu Bara mwaka 2008/09 kumalizika Mei mwakani.
"Kaseja alikuwa mjanja sana, alitubana sana, hakutaka kuweka mkataba wa miaka miwili kama tulivyotaka, alikuwa akisoma kila kipengele, ameweka masharti mengi kama makipa wa Ulaya," kilisema chanzo kutoka Yanga.
Kaseja alipokea kitita cha dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 36 za Tanzania na ndipo akakubali kusaini mkataba huo wa mwaka mmoja.
Licha ya hilo, Kaseja atalipwa mshahara wa Sh milioni moja kila mwezi hivyo kwa mwaka mmoja ambao atakuwa Yanga atalipwa jumla ya Sh milioni 12.
Kipa huyo bora nchini licha ya kutokuwamo kwenye kikosi cha Marcio Maximo, atalipwa Sh milioni 3.6 za nyumba kwa mwaka ikiwa ni Sh 300,000 kwa mwezi.
"Tayari amechukua Sh milioni 1.8 kwa ajili ya nyumba, nyingine atazichukua baadaye," kilisema chanzo cha habari kutoka Yanga.
Inadaiwa kuwa Kaseja alipangiwa usafiri wa Sh milioni tano kwa mwaka, lakini akataka apewe fedha hizo na ameahidiwa kupewa haraka iwezekanavyo.
Gharama zote za Yanga kumsajili Kaseja, kuanzia mkataba, mshahara wake wa miezi 12, gharama za nyumba na usafiri zinafikia jumla ya Sh milioni 57.
Kipa huyo, ambaye amewahi kuchezea Moro United kwa sasa ndiye mchezaji ghali zaidi wa Tanzania kuwahi kusajiliwa nchini pengine tangu Uhuru mwaka 1961.
mwisho

No comments: