Tuesday, June 10, 2008
ZOMBE LEO
Polisi adai Zombe aliwapongeza wauaji
*Shahidi asema yeye ndiye alitakiwa kuuawa kwa kuwa ni jambazi
SHAHIDI wa 24 katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi, amedai mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Abdallah Zombe aliagiza askari waliowaua wafanyabiashara hao wapandishwe vyeo, wakati shahidi mwingine ameibuka na kudai wafanyabiashara hao hawakuwa na kosa badala yake alistahili kuuawa yeye.
Shahidi wa 24 katika kesi hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Sebastian Masinde ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alidai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana kwamba siku moja baada ya mauaji ya wafanyabiashara hao aliagizwa na Zombe awapeleke askari hao, ofisini kwa Zombe ili awape mkono wa pongezi kwa kazi waliyokuwa wameifanya
“Asubuhi ya Januari 15, mwaka 2006 nilipokuwa nikijiandaa kwenda chuoni nilikokuwa nikisoma nilipata taarifa kwa njia ya ‘Radio Call’ kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Dar es Salaam na Kaimu Kamanda ACP Zombe kuwa niwapeleke vijana wangu ofisini kwake ili awape mkono wa pongezi kwa kuua majambazi na kukamata pesa na silaha,” alidai SSP Masinde.
Alidai taarifa hiyo ya Zombe iliwahusisha wakuu wa vituo vingine ambao askari wao walishiriki katika tukio hilo na kwamba aliwataka Makamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) na wakuu wengine wa vituo vya polisi kutoka sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam, kufika ofisini kwake kwa ajili ya hafla ya kuwapongeza askari hao
SSP Masinde alidai baada ya kupata taarifa hiyo alimuita dereva Koplo Noel ambaye ni mshitakiwa wa nne na kumwagiza awakusanye wenzake wengine na kuingia ndani kwa ajili ya kuwapeleka huko kwa Zombe kupongezwa.
“Niliwapeleka askari wangu wote waliokuwa wameshiriki katika tukio hilo kasoro Koplo James ambaye hakuwepo kazini na kwa sasa sijui aliko,” alieleza SSP Masinde.
Alidai walipofika ofisini kwa Zombe katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central), walimkuta Zombe katika ofisi ya Kamishna Tibaigana akiwa pamoja na maofisa wengine wa Polisi.
“Zombe aliwapongeza vijana wale akisema wamefanya kazi nzuri sana kuwakamata majambazi na pesa pamoja na bastola. Alionyesha pesa zile zikiwa kwenye mfuko pamoja na bastola ile na akaagiza tufanye utaratibu wa kuwapandisha vyeo,” alisisitiza SSP Masinde.
Alipoulizwa na Kiongozi wa waendesha Mashtaka (PP) Revocatus Mtaki ambaye ni Wakili wa Kujitegemea kama walitekeleza agizo hilo, SSP Masinde alisema hawakutekeleza na badala yake waliwaweka katika kumbukumbu wakisubiri taratibu nyingine za kuwapandisha vyeo askari.
Alidai katika utaratibu wa kuwapandisha vyeo askari, huwezi kuandika mara moja tu bali unapaswa kuweka kumbukumbu na kusubiri maagizo kutoka makao makuu.
SSP Masinde aliiambia mahakama kuwa wakati wa tukio hilo alikuwa akisoma katika Chuo cha Polisi Kurasini na kwamba siku ya tukio, Januari 14, mwaka 2006 alikuwa chuoni ambako kulikuwa na kikao cha wanafunzi na walimu (School Baraza).
Alidai baada ya kikao hicho aliondoka kurudi kituoni na alipofika katika kituo hicho, saa 2 za usiku alipata taarifa kutoka kwa Koplo Omar kuwa askari wake walikuwa wamewakamata majambazi wakiwa na pesa Sh5 milioni pamoja na bastola moja.
Aliwataja askari hao ambao siku hiyo walikuwa zamu na ambao walishiriki katika tukio hilo kuwa ni Koplo Moris, Koplo Felix Nyangelela, Koplo Festus ambaye ni mshitakiwa wa 13 na Koplo Michael, Koplo Emmanuel Mabula na Staff Sajenti James ambaye hadi sasa hajulikani aliko.
Alidai askari hao, waliondoka kuelekea eneo la tukio wakiwa na gari aina Isuzu lenye namba za usajili SU 29363.
Pesa hizo zilipelekwa katika Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ASP Ahmed Makelle ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi katika kituo hicho (OC-CID) na ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo.
SSP Masinde alidai katika msafara huo, Koplo Noel na Koplo Festus hawakuwa na silaha kwa kuwa walikuwa madereva na kwamba kazi yao ilikuwa ni kuwasindikiza wenzao.
Alidai wakati akienda kwa Zombe, alimwagiza Mtunza ghala la silaha akague silaha na risasi, lakini aliporudi alipewa taarifa kuwa silaha zote tatu walizokuwa wamepewa askari zikiwemo SMG mbili na risasi 30 kila moja na bastola moja na risasi nane, zote zilirejeshwa salama na kwamba hakuna hata moja iliyokuwa imetumika.
Naye Shahidi wa 25 Shabani Saidi Manyanya aliiambia mahakama hiyo kuwa aliumia sana aliposikia Zombe akitangaza kwenye runinga kwamba askari polisi wamewaua majambazi wanne Sinza, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la uporaji wa pesa za Kampuni ya Bidco.
Manyanya alidai katika mahakama hiyo kuwa kilichosababisha hadi aumie ni kuuawa kwa wafanyabiashara hao na kwamba walionewa kwa kuwa siyo wao waliokuwa wamehusika katika tukio hilo la uporaji lililotokea katika barabara ya Sam Nujoma, bali yeye na wenzake ndiyo waliohusika katika uporaji huo.
Manyanya alidai alipaswa auawe yeye na wenzake kwa kuwa wao ndio waliofanya uporaji huo si wafanyabiashara hao ambao hawakuwa na hatia yoyote.
Manyanya alidai kutokana na kuumia kupita kiasi baada ya wafanyabiashara hao kuuawa, alikwenda kutoa maelezo yake katika Tume ya Rais ya Kuchunguza mauaji hayo iliyoongozwa na Jaji Kipenka.
Manyanya alidai yeye na wenzake wengine wanne, waliohusika katika uporaji huo kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Akielezea mipango ya uporaji huo, Manyanya ambaye wakati huo alikuwa mkazi wa Mwananyamala alidai siku moja alifuatwa na rafiki yake mmoja, Grayson na kumwambia kuwa kulikuwa pesa za Kampuni ya Bidco ambazo wanapaswa wazipore.
Alidai baada ya kuelezwa hivyo, alimuuliza Grayson nani alimwambia kuhusu kuwepo kwa fedha hizo, naye alimjibu kuwa aliambiwa na Ali (kibarua wa zamani wa kampuni hiyo) na kwamba mpango kamili alikuwa akiujua Mashaka ambaye alikuwa ni dereva wa magari ya kampuni hiyo yanayokusanya mauzo ya bidhaa mbalimbali kutoka maduka ya kampuni hiyo.
Alidai baada ya kupata taarifa hizo aliwaandaa wenzake na kupanga jinsi ya kupora fedha hizo, wakishirikiana na dereva wa Bidco Mashaka, lakini mara ya kwanza na ya pili mpango wao ulishindikana na kwamba walikuja kufanikiwa mara ya tatu.
Manyanya alidai siku ya tatu hakwenda eneo la tukio na badala yake alibaki nyumbani kwake Mwananyamala na wenzake wakaenda kuzivizia pesa hizo.
Alidai walipokwenda kwenye tukio walikodi teksi iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye naye alijulikana kwa jina la Mashaka na kwamba siku hiyo walifanikiwa kupora pesa hizo na bila kutumia silaha yoyote.
Aliongeza kuwa akiwa nyumbani kwake
jioni hiyo wenzake walimwambia tayari wamefanikiwa kupora pesa hizo, lakini wakadai kuwa zilikuwa ni Sh6milioni tu badala ya Sh36 milioni kwa kuwa duka lingine ambako walitarajia kupata makusanyo ya Sh30 milioni lilikuwa limefungwa.
Aliendelea kudai baada ya wenzake kufika waligawana pesa hizo na kupewa Sh 400,000 na jioni hiyo kwenda kujipongeza katika baa moja.
Alidai akiwa katika baa ambayo hakuitaja jina alifuatwa na askari mmoja aliyeitwa Kulwa akamwambia kuwa amesikia wamepora pesa naye alikubali.
Alieleza mahakama kuwa alimfukuza askari huyo huku akimwambia asimletee njaa zake.
Alidai saa 10 usiku alifuatwa na askari wengine aliowatambua kwa majina ya Enjewele na mwenzake kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay wakiwa wamewakamata wenzake aliokuwa ameshiriki nao katika uporaji huo.
Alidai Enjewele alimuuliza kama alikuwa anawafahamu wale aliokuwa nao na Manyanya alisema anawafahamu na kwamba walipora nao fedha hizo huku askari Enjewele akimwambia kuwa alikuwa ametumwa na mamlaka kuchukua fedha hizo.
“Nilikuwa nimezitumia na zimebakia Sh350,000, hivyo nilimpa zote akaniachia na akaniambia inabidi nihame Dar es Salaam na ndipo nilipokwenda Zanzibar,” alidai.
Alidai akiwa Zanzibar aliona kwenye runinga wakitangaza kuwa kuna majambazi wanne wameuawa kwa tuhuma za kupora pesa za Kampuni ya Bidco.
“Iliniuma sana kwani waliouawa siyo waliokuwa wamepora hizo pesa bali ni mimi na wenzangu. Kwa hiyo kama ni kufa mimi ndio nilitakiwa niuawe lakini si wale waliouawa,” alidai Manyanya na kuongeza kuwa alishangaa kusikia kuwa pesa zilizoporwa ni Sh5milioni wakati wao walipora Sh6milioni.
Akijibu maswali kutoka kwa mawakili wa upande wa utetezi, Manyanya alidai amekuwa akifanya kazi hiyo ya wizi kwa muda wa miaka 10 sasa na kwamba hatarajii kuacha hadi atakapokufa jambo ambalo liliwaacha wasikilizaji kuvunjika mbavu.
Yafuatayo ni maswali na majibu kutoka kwa mawakili wa utetezi na shahidi wa 25 Shaban Manyanya.
Maira: Shahidi, leo umetokea wapi kuja hapa mahakamani, nyumbani kwako au gerezani?
Manyanya: Nimetokea nyumbani kwangu.
Maira: Kwa nini siyo gerezani wakati wewe umeiambia mahakama kuwa ni mwizi na ulistahili uwe gerezani?
Manyanya: Kwani polisi hakuna?
Maira: Si ndio waliokuachia?
Manyanya: Waulize wao.
Maira: Umesema wenzako walipokwenda kupora walikuwa na teksi, je kama polisi wa doria, badala ya kufuata teksi ya majambazi wenzako na kwa bahati mbaya wakafuata teksi nyingine wakidhani ndio kundi lako walifanya makosa?
Manyanya: Mimi sikuwepo.
Majura Magafu: Shahidi kutokana na ushahidi wako umekiri kushiriki katika uporaji wa pesa za Bidco kwa kushiriki katika kufanikisha mipango hiyo?
Manyanya: Sawa kabisa.
Majura: Baada ya kuona taarifa za tukio la mauaji kwenye TV, je, ulijitokeza kwenye chombo chochote kama vile polisi kuwa waliouawa walionewa au kwa bahati mbaya au nyie ndio mliopora?
Manyanya: Sikufanya hivyo kwa sababu siwezi kujishtaki.
Majura: Umesema uliogopa kukamatwa, je, leo hii uko hapa na unajitangaza hivyo, huogopi kukamatwa?
Manyanya: Nilikamatwa na walichukua pesa zote.
Majura: Kwa hiyo unadhani kunyang’anywa hizo pesa ndio ulikuwa adhabu yako?
Manyanya: Unavyojua wewe.
Magafu: Nikisema hujawahi kuwa mwizi na kwa tabia ya mwizi hawezi kujitangaza hivi, utasemaje?
Manyanya: Siyo kweli.
Majura: Wizi ulianza lini?
Manyanya: Miaka 10 iliyopita.
Majura: Na mpaka sasa leo hii unaendelea?
Manyanya: Bado naendelea.
Majura: Ni lini unategemea kuacha?
Manyanya: Sitegemei kuacha mpaka kufa kwangu.
Majura: Ulishawahi kupatikana na matatizo ya ugonjwa wa akili?
Manyanya: Sijawahi.
Myovela: Mbali na hizo pesa za Bidco unazodai mlipora, je, ni wizi gani mwingine huwa unaufanya?
Manyanya: Kuwauzia watu madini hewa.
Mshauri Margreth Mosi: Hilo group (kundi ) lenu la wizi linafahamika Oysterbay?
Manyanya: Wanalifahamu sana.
Mosi: Enjewele na wenzake alipokuja kwako uliwapa nini hadi wakakuachia na kuwaambia mtoroke?
Manyanya: Zile pesa walizochukua.
Sehemu ya maswali na majibu kutoka kwa mawakili hao upande wa utetezi na majibu kutoka kwa shahidi wa 24, SSP Masinde.
Wakili Moses Maira: Shahidi, hebu tusaidie, ulipofika ofisini kwa Zombe ulikuta maofisa wangapi?
Shahidi SSP Masinde: Sikumbuki.
Maira: Umesema Zombe alizungumzia suala la Recommendation (kuwapandisha vyeo) je, hiyo imo kwenye PGO? (utaratibu wa maagizo ya utendaji kazi wa jeshi la polisi).
SSP Masinde: Ni maagizo ya mara kwa mara.
Maira: Kwa hiyo Zombe hakuwa nje ya utaratibu kuagiza hivyo?
SSP Masinde: Hakuwa nje ya utaratibu.
Maira: Umesema mkiwa ofisini kwa Zombe, Zombe alionyesha fedha na bastola je, hizo pesa zilikuwa shilingi ngapi?
SSP Masinde: Sijui kwa sababu hazikuhesabiwa ila alisema tu ni Sh 5milioni.
Wakili Gaudioz Ishengoma: Shahidi, umesema taarifa za askari wako kukamata majambazi uliambiwa na Koplo Omary na hukusikia wakati Makelle na Bageni wakiwasiliana, kwani huna ‘Radio Call’?
SSP Masinde: Ninayo lakini nimesema siku hiyo nilikuwa niko shuleni hivyo huko sikuwa nayo.
Wakili Rongino Myovela: Shahidi, umesema Noel na Felix wao huwa ni wasindikizaji tu wa askari wanaopewa silaha kwenda kazini, je, utakubaliana nami kuwa siku hiyo hakuna silaha waliyochukua kwa sababu ni wasindikizaji tu?
SSP Masinde: Ni kweli.
Mshauri wa Mahakana, Nicolas Kimolo: Shahidi, hebu ifahamishe mahakama, ulipopata taarifa kwa Omary kuwa askari wako wamekamata majambazi alikuambia wamewapeleka wapi?
SSPMasinde: Hakusema hilo, na kwa kuwa alikuwepo Mkuu wa Upelelezi (OC-CID) wa Wilaya ya Kinondoni na OC-CID wa Kituo cha Urafiki ambao wote ni viongozi mimi sikutaka kufuatilia zaidi niliwaachia tu wafanye kazi.
Mshauri Margreth Mosi: Je, Zombe alisema majambazi waliokamatwa wako wapi?
SSP Masinde: Hilo hakulisema.
Mosi: Ulipoambiwa kuwa silaha hazikuitumika lakini majambazi wamekamatwa wakiwa na silaha, je, taarifa hizo uliichukuliaje?
SSP Masinde: Niliichukulia kwamba hapakuwa na mapambano ya kurushiana risasi maana kama kungekuwa na kurushiana risasi ingekuwa ni ua nikuue, hivyo risasi zingekuwa zimetumika.
Naye shahidi wa 26 katika kesi hiyo, Ramadhan Said Tupa (32) jana aliieleza Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam jinsi alivyowatuliza polisi na pesa alizopora kwenye tukio la ujambazi.
Shahidi huyo ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo na mkazi wa Mwananyamala kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake alinyoosha kidole na kumwomba jaji amlinde kutokana na ushahidi atakaoutoa.
Alidai katika mahakama hiyo kuwa mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka 2006 akiwa Dar es Salaam alifuatwa na marafiki zake wawili Italaka na Kei na kumweleza kuwa kuna ‘dili’ la pesa.
Alidai baada ya marafiki zake kumweleza ‘dili’ hilo aliwataka aonane na mhusika mkuu ambaye ni dereva wa Kampuni ya Bidco aliyemtaja kwa jina moja la Mashaka.
“Tulikutana na Mashaka Mwananyamala B. Januari 14, mwaka 2006 nikiwa nyumbani nilifuatwa na Italaka na aliniambia mipango iko tayari na tukaenda barabarani kusubiri gari lipite ili tupore pesa,” alidai Tupa.
Tupa alieleza walipora fedha hizo za Bidco katika eneo la barabara ya Sam Nujoma na kwamba zilikuwa kwenye mfuko wa rambo wa rangi ya bluu.
“Lile gari lilipofika pale tulilisimamisha tukamwambia dereva tupe chetu akatoa mfuko wenye hela, sisi huwa hatutumii silaha ya aina yoyote bali ni maneno tu,” alieleza Tupa.
Shahidi huyo aliyeonekana kujiamini wakati wa kutoa ushahidi wake aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya uporaji huo walikwenda baa.
Alidai kuwa baada ya kutoka baa waliondoka kwenda kwa rafiki yao mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Lunje ambako huko walihesabu fedha walizopora na kupata Sh6 milioni.
Alidai waligawana na alipata Sh1.7 milioni na Lunje alipata Sh3 milioni na kwamba waligawana viwango tofauti kutokana na ugumu wa kazi.
Alidai Januari 16, mwaka 2006 majira ya saa 4 asubuhi alikutana na Koplo Joel wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambaye alimuuliza kuhusu wizi huo na kwamba yeye alikataa.
“Baada ya kuona askari wananisumbua Januari 17, mwaka 2006 niliamua kwenda nyumbani kwa mke wa askari Enjewele wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ili kumwomba namba ya mumewe nimpigie tumalizane,” alisema Tupa.
Alidai alipewa namba hiyo ya simu na kumpigia Enjewele na kwamba walikutana usiku wa Januari 17, mwaka 2006 na kumpa Sh 400,000.
Alidai baada ya kumpa fedha hizo, Enjewele alimtaka atoe hela nyingine na kwamba alimuagiza aende Kituo cha Mwananyamala A.
“Nilipofika pale nilivamiwa na askari wawili Hadilu na Mabela wote wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay wakanionyesha kitambulisho na bastola na kunipeleka Kituo cha Polisi cha Mwinyijuma CCM kilichoko Mwananyamala,” alieleza Tupa
Shahidi huyo alidai alipofika katika kituo hicho Hadilu alimwambia kuwa anataka Sh 200,000 na kwamba yeye alimjibu kuwa ameshawapa askari wenzake.
Alidai baada ya kuona wanamsumbua aliagiza mtu aende kumuita dada yake aliyemtaja kwa jina moja la Tausi na kwamba kabla hajafika polisi walimfundisha aseme uongo kwamba amekamatwa kwa wizi wa simu ili dada yake amwekee dhamana.
Alidai dada yake alipofika alitoa Sh 40,000 na kwamba polisi walimwachia.
Shahidi huyo pia aliieleza mahakama kuwa aliamua kwenda kutoa taarifa za uporaji huo kwenye tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kutokana na uchungu alioupata wa kusikia roho za watu ambao hawana hatia wameuawa.
“Niliamua kwenda kule tume kwa sababu wale waliouawa sio majambazi kama kuuawa ilikuwa tuuawe sisi, nilisikia uchungu sana halafu polisi walizidi kunifuata fuata kila siku na kuchukua hela zangu,” alieleza Tupa.
Baadhi ya mahojiano na mawakili yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Nsemwa: Shahidi kutokana na ushahidi ulioutoa hapa utakubaliana nami kuwa wewe ni mwizi?
Shahidi: Ndio.
Nsemwa: Je, unafahamu kama wizi ni kosa la jinai?
Shahidi: Ndio.
Nsemwa: Katika matukio ya uhalifu je, umeiba mara ngapi?
Shahidi: Hili la Bidco ni tukio langu la pili ila nimezoea wizi wa ‘nyatunyatu’ (kibaka).
Nsemwa: Huo wizi wa ‘nyatunyatu’ umekuwa ukiufanya wapi?
Shahidi: Uswahilini.
Wakili Magafu: Je, katika matukio yako ya wizi uliwahi kushikwa na polisi?
Shahidi: Ndio nashikwa halafu tunamalizana.
Magafu: Tangu ulipofanya uporaji wa hela za Bidco uliwahi kufikishwa mahakamani?
Shahidi: Sijawahi.
Magafu: Wewe polisi ni marafiki zako?
Shahidi: Hapana ila nawapenda kama wakiwa wakweli.
Magafu: Uchungu unaousema ni uchungu gani hasa?
Shahidi: Baada ya kusikia Zombe anatangaza kwenye vyombo vya habari kuwa wamewaua majambazi wa Bidco wakati ni uongo nilisikia uchungu sana.
Magafu: Utakubaliana nami kuwa kuombwa ombwa hela na polisi ndiko kumekufanya usikie uchungu na kwenda kutoa taarifa kwenye tume?
Shahidi: Ndio lakini mbali ya hela ni uchungu wa Watanzania wenzangu waliouawa bila hatia.
Kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2006 kwa mara ya kwanza, Zombe na wenzake 12 walifikishwa mahakamani Septemba 28, mwaka juzi mbele ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Laurian Kalegeya ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Kesi hiyo inaendelea tena leo katika mahakama hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Kaka endelea kutuletea kesi hii.Inasisimua sana kusoma ingawa inatia uchungu pia kuona maisha ya watu yalipotea.
Post a Comment