Shahidi adai Bageni ndiye aliyeamuru kuua! Mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya Mauaji, Abdallah akiwasiliana na mawakili wake, Jarome Msemwa Moses Maira jana wakati wa shauri hilo katika Mahakama Kuu.
SHAHIDI wa 27 katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge Morogoro na dereva teksi ameieleza Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kuwa, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Mrakibu wa Polisi (SP), Christopher Bageni, aliamuru askari polisi kuwafyatulia risasi wafanyabiashara wa madini wa Mahenge.
Akitoa ushahidi katika mahakama hiyo jana, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Kitengo cha Upelelezi Makao Makuu ya Polisi, (ACP) Maximinus Michael, alidai kuwa SP Bageni alitoa maagizo hayo baada ya wale wafanyabiashara waliouawa kwa tuhuma za ujambazi na kuwarushia risasi polisi.
Katika mahakama hiyo aliyoongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali (PP), Jasson Kaishozi, ACP Michael alisema, SP Bageni alitoa maelezo hayo mbele ya timu iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza ukweli wa tukio la mauaji hayo na kwamba alikuwa ni mjumbe katika timu hiyo.
ACP Michael aliieleza Mahakama hiyo kuwa, siku tano baada ya mauaji hayo, akiwa ofisini kwake saa 2.00 usiku aliitwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mgawe katika Hotel ya Movenpick.
“Nilipofika SACP Mgawe alinieleza alikuwa ameagizwa na Kamishna wa Mafunzo Tibasana afanye uchunguzi wa tukio la mauaji hayo na kwamba angependa nimsaidie mimi pamoja na ACP Mgasa,” alieleza ACP Michael.
Alidai baada ya siku hiyo, walikwenda ofisini kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, ambaye pia wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa, ACP Abdallah Zombe.
“Tulipofika ofisini kwa ACP Zombe tulimkuta akiwa na ACP Mkumbo, ACP Masawe na SP Bageni. SACP Mgawe alimweleza ACP Zombe kuwa ameagizwa kufanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya Sinza,”alieleza ACP Michael.
Alidai walipomuuliza Zombe kama alikuwa amekwenda kukagua eneo la tukio, alimjibu kwamba hakuwa amekwenda na wakakubaliana waende katika eneo hilo kwa ajili ya kulikagua.
ACP Michael alidai Januari 20, mwaka 2006 ACP Michael, ACP Mgasa na SACP Mgawe walikwenda kwa SP Bageni katika Kituo cha Polisi Oysterbay na kwamba baadaye ACP Zombe naye alifika katika kituo hicho.
Alidai baada ya Zombe kufika, SP Bageni aliingia katika gari la Zombe na kuanza msafara wa kuelekea eneo palipofanyika uporaji wa fedha za Bidco, katika Barabara ya Sam Nujoma.
Alidai wakiwa katika barabara hiyo, SP Bageni alianza kuwapa maelezo ya jinsi tukio hilo lilivyotokea.
ACP Michael alidai wakiwa katika barabara hiyo, SP Bageni aliwaeleza kwamba baada ya tukio hilo kutokea alifika katika eneo la tukio akiwa na timu ya askari wake wa upelelezi na kuwakuta askari polisi wa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa na gari na silaha na wahanga wa Bidco.
ACP Michael alidai SP Bageni aliwaeleza kuwa baada ya kuwahoji wahanga hao, walieleza kuwa majambazi waliopora fedha za Bidco walikuwa na teksi nyeupe na silaha.
Alidai baada ya kuchukua maelezo hayo, SP Bageni aliwataka askari hao kufuatilia katika njia za vichochoro na baadaye walifanikiwa kuyakuta majambazi hayo (wafanyabiashara) katika eneo la Sinza.
ACP Michael alieleza Mahakama Kuu kuwa baada maelezo hayo, SP Bageni aliongoza msafara hadi Sinza mahali ambako ilidaiwa kutokea majibizano kati ya askari na wafanyabiashara hao.
“SP Bageni alitueleza kuwa siku hiyo walipofika eneo la ukuta wa Posta wakiwa umbali wa kama mita 50 waliweza kuona magari mawili yakiwa yameegeshwa moja jeupe na lingine lilikuwa na rangi nyeusi.
ACP Michael alidai Bageni aliwaeleza kwamba baada ya watu waliokuwa kwenye magari hayo, kuliona gari la polisi, gari jeupe liliondoka kwa kasi na jeusi lilishindwa kuondoka na ghafla waliteremka watu wanne, mmoja akiwa na bastola na kuanza kuwarushia risasi askari hao.
“Baada ya majambazi hao kuanza kurusha risasi nikawaamuru askari kujibu mashambulizi na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi wote wakati wakijaribu kupanda ukuta ili watoroke, lakini wote walianguka chini,” alidai ACP Michael baada ya kumkariri SP Bageni.
ACP Michael alidai baada ya mashambulizi hayo, alifika Mrakibu Msaidizi wa Polisi ambaye wakati huo, alikuwa Mkuu wa Upelelezi kituo cha Urafiki, ASP Makelle akiwa na askari wake na moja kwa moja alikwenda kukagua ndani ya gari la wafanyabiashara na kukuta mkoba ambao ndani yake kulikuwa na Sh 5milioni.
“SP Bageni alidai katika eneo la tukio hilo pia aliokota maganda ya risasi za bunduki ya SMG na maganda ya bastola, lakini sikumbuki kama alitaja idadi,” alieleza ACP Michael.
Alidai SP Bageni aliwaeleza baada ya wafanyabiashara hao kujeruhiwa aliwachukua na gari la polisi ili kuwapeleka katika eneo lilipotokea tukio la uporaji wa pesa za Bidco, lakini kabla ya kufika katika eneo hilo, majeruhi walikuwa wamefariki dunia.
ACP Michael alidai SP Bageni aliwaambia baadaye maiti, zilipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
ACP Michael aliieleza mahakama kuwa wakiwa katika eneo la tukio, ACP Mgasa aliokota ganda moja la risasi ya bastola na askari mwingine aliokota ganda lingine na maganda yote kumkabidhi SP Bageni.
ACP Michael aliieleza mahakama hayaamini moja kwa moja maelezo yaliyotolewa na SP Bageni kutokana na hali halisi aliyoikuta eneo la tukio kwamba yalitokea majibizano kati ya askari na wafanyabiashara hao.
Alidai walikagua eneo la ukuta ambako ilidaiwa kufanyika mashambulizi hayo, lakini hakuweza kuona ishara yoyote iliyoonyesha kuwepo kwa mashambuzi ya risasi.
“Mimi nilitarajia kuona damu katika eneo la tukio, lakini sikuona hata tone la damu pale chini wala ukutani. Nilipomuuliza SP Bageni alidai ni kwa sababu jana yake mvua ilikuwa imenyesha,” alidai ACP Michael.
Alidai walipokagua katika ukuta wa Posta ambako ilidaiwa kulikuwa na matundu ya risasi, aliona alama ndogo kama matundu ya risasi na kwamba kama yalikuwa ni ya risasi basi zilikuwa zimepigwa kutokea ubavuni na si wima wima.
Alipoulizwa na PP Kaishozi kama SP Bageni alipokwenda katika eneo hilo, alikuwa na ramani ya eneo hilo.
ACP Michael alidai SP Bageni hakuwa na ramani na kwamba walimwagiza achore ramani.
ACP Michael alidai katika eneo hilo lililodaiwa kutokea majibizano ya risasi, kuna gereji na pembeni kisima cha maji na upande mwingine kulikuwa na wauza matunda.
“Nilikwenda pale gereji na pia katika kisima, nilipowauliza watu kama waliwahi kusikia milio ya risasi, walisema hawajawahi kusikia milio ya risasi katika eneo hilo,”alieleza ACP Michael.
Alidai baadaye walirudi ofisini ili kuendelea na uchunguzi, lakini kabla hawajakamilisha, iliundwa Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Kipenka kuchunguza suala hilo na hivyo wakalazimika kusitisha uchunguzi wao.
Alidai licha ya kusitisha uchunguzi, waliandika taarifa ya walipokuwa wamefikia na kuikabidhi Tume hiyo.
Sehemu ya mahojiano kati ya mawakili wa upande wa utetezi kuhusiana na maelezo ya ushahidi wa ACP Michael yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Gaudioz Ishengoma: Mlikwenda kwa ofisini kwa Zombe, mlimfuata kama RPC au kama RCO?
Shahidi ACP Michael: Wakati huo alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi Mkoa.
Ishengoma: Kwa hiyo lile swali ulilomuuliza la kukagua eneo la tukio ilikuwa ni sahihi kwake?
ACP Michael: Yeye kama RCO (Mkuu wa Upelelezi Mkoa) na RPC alipaswa awe amefanya hivyo kwa tukio kubwa kama lile.
Ishengoma: Lakini si lazima tu afike yeye?
ACP Michael: Ukisoma PGO (Utaratibu wa Utendaji kazi wa Jeshi la Polisi) namba 3, OC-CID, RPC, au RCO, lazima awe amefika kukagua eneo la tukio katika tukio kubwa kama hilo.
Ishengoma: Umesema SP Bageni alikuwa akiwaeleza hayo uliyoyasema hapa, ambayo ninaamini huyaamini yote.
ACP Michael: Yapi?
Ishengoma: Yote aliyokueleza.
ACP Michael: Siyaamini na ndio maana nikatoa mashaka, kwani nilivyotarajia sikuona damu eneo la tukio.
Ishengoma: Je, alipokueleza kuwa aliyeamuru askari warushiane risasi ili kujibu mashambulizi, pia huamini?
ACP Michael: Siamini.
Wakili Majura Magafu: Shahidi, utakubaliana nami kwamba kulikuwa na tukio la uporaji Bidco?
ACP Michael: Nakubali.
Magafu: Je, utakubaliana nami pia kuwa baada ya polisi kupata taarifa za tukio hilo kwenye mawasiliano ya ‘Radio Call’ ilibidi wa-respond kwa sababu wakati huo kulikuwa na matukio ya ujambazi yaliyokithiri na hivyo ilibidi askari wawe makini kuzuia matukio hayo?
ACP Michael: Ni sahihi, waliwajibika kufanya hivyo.
Mshauri Nicolas Kimolo: Shahidi, mlimuuliza SP Bageni wale majeruhi walikuwa katika hali gani?
ACP Michael: Alisema kabla ya kufikishwa katika eneo ambako kulifanyika uporaji ili watu hao waweze kutambuliwa walifariki.
Margreth Mosi: SP Bageni aliwaeleza walijeruhiwa sehemu gani za miili yao?
ACP Michael: Hakusema.
Mosi: Aliwaeleza katika majibizano hayo ya risasi ni askari wangapi waliojeruhiwa?
ACP Michael: Hapana, hakuna askari hata mmoja aliyejeruhiwa.
John Gunzareth: Mliweza kuona matundu pale ukutani na yalikuwa ni ya risasi gani?
ACP Michael: Sisi tulielezwa kuwa ni ya SMG, lakini tulipofika tuliokota maganda ya bastola.
Kesi hiyo imeahirishwa na itaendelea tena leo katika mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment