Friday, June 13, 2008

ZOMBE LEO

Gari iliyodaiwa kutumiwa na majambazi haina matundu ya risasi.
Zombe ataka kesi isiitwe kwa jina lake

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana imeelezwa kuwa teksi inayodaiwa kurushiwa risasi na polisi, wakati wa mapambano yao na wafanyabiashara wa Mahenge, Morogoro halikuwa na matundu yoyote ya risasi.
Katika taarifa ya awali ya jeshi la polisi, ilielezwa kuwa wafanyabiashara hao, waliuawawa na askari polisi baada ya kurishiana risasi wakiwa kwenye gari hiyo (teksi).
Gari hilo aina ya Toyota Mark II yenye namba za usajili T 617 AAS lilifikishwa jana katika mahakama hiyo na kutolewa kama kielelezo wakati kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake 12.
Gari hilo lilitumiwa na wafanyabiashara hao kama teksi wakati wakielekea Sinza kwa mke wa rafiki yao, Methew Ngonyani (shahidi namba moja)
Akitoa ushahidi jana, Meneja wa Ufundi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), Julius Haule (40) ambaye ni mmiliki wa gari hiyo (teksi) na shahidi wa 29 katika kesi hiyo, aliieleza mahakama hiyo kwamba gari hilo, lilikuwa likitumika kwa biashara ya teksi.
Haule alidai gari hilo, alilinunua mwaka 2003 na kwamba mwaka 2005, ilianza kutumika kama teksi.
Alidai alimuajiri marehemu Juma Ndugu kama dereva wa gari hilo na kwamba alikuwa akifanya nalo biashara katika eneo la Sinza Kijiweni.
"Nilimuajiri marehemu Juma kama dereva wa gari yangu kwa ajili ya biashara ya teksi na makubaliano yetu yalikuwa kila Jumapili asubuhi aniletee Sh60,000," alieleza Haule.
Alidai Januari 15, mwaka 2006 alikuwa nyumbani kwake Kinondoni na kwamba siku hiyo dereva wake hakuleta hela kama ilivyokuwa kawaida yake.
"Nilikaa nyumbani kumsubiri na nilipoona kimya ilipofika saa sita mchana niliamua kumpigia simu, lakini ilikuwa haipatikani," alieleza Haule.
Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa baada ya kuona simu ya dereva huyo haipatikani aliamua kwenda Sinza Kijiweni, mahali ambako dereva huyo alikuwa akipaki gari lakini hakumkuta.
Alidai aliwauliza madereva wenzake aliko dereva wake na walimjibu kuwa hawajui chochote na kwamba kutokana na hali hiyo alikwenda nyumbani kwa dereva huyo katika eneo la Manzese Kilimani lakini hakumkuta.
"Nilipokwenda nyumbani kwake niliwauliza pia majirani zake wakasema hawajamuona na wala hawajui lolote na kwakuwa ilikuwa usiku niliamua kurudi nyumbani kwangu," alidai Haule.
Shahidi huyo alidai Januari 17, mwaka 2006 majira ya jioni alipata taarifa kutoka kwa baadhi ya madereva waliokuwa wakifanya kazi na dereva huyo kwamba, gari lake liko Kituo cha Polisi cha Urafiki.
Alidai aliamua kwenda katika kituo cha hicho kwenda kuangalia gari na kwamba alilikuta likiwa salama.
Alidai Machi 3, 2006 alikabidhiwa gari hilo na kuambiwa kuwa asiliuze wala kubadilisha rangi.
Upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa Serikali Angaza Mwipopo uliiomba mahakama kulipokea gari hilo kama kielelezo cha kesi hiyo.
Kabla pande zote hazijakubaliana kupokea kielelezo hicho, Jaji Kiongozi anayesikiliza kesi hiyo, Salum Massati alizitaka pande zote pamoja na washitakiwa kutoka na kwenda kuliangalia gari hilo ili kupata ukweli kama ndio lenyewe kama alivyosema shahidi huyo.
Baada ya kuliangalia gari hilo, pande zote zilikubaliana na mahakama, ikalipokea gari hilo na kuwa moja ya kielelezo katika kesi hiyo.
Jaji Massati alimtaka shahidi huyo kuchukua gari hilo kwa ajili ya usalama zaidi na kwamba halitatakiwa kuuzwa ama kubadilishwa rangi katika kipindi chote cha kesi hiyo.
Baadhi ya mahojiano ya mawakili, wazee wa baraza na shahidi yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Longindo Myovella: Shahidi je, kuna mkataba baina yako na marehemu?
Shahidi: Hakuna.
Myovlla: Kati yako na dereva wako nani alikuwa anakaa na gari?
Shahidi: Yeye dereva.
Myovlla: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba uangalizi wa gari hilo ulikuwa si chini yako?
Shahidi: Sikweli.
Myovlla: Unajua gari lilikuwa likilala wapi?
Shahidi: Sikuwa na haja ya kujua.
Myovlla: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba Januari 13, 14 na 15, 2006 hujui kama gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva wako?
Shahidi: Sijui.
Mzee wa Baraza Kimolo: Ulipokwenda kituo cha polisi cha Urafiki je, walikueleza kwamba dereva wa gari lako alikuwa wapi?
Shahidi: Walinieleza kuwa alikuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Kimolo: Je, ulikwenda Muhimbili kutambua mwili wa dereva wako?
Shahidi: Sikuweza kwenda kutambua.
Mzee Mosi: Nani aliyekupa taarifa kwamba gari lako liko kituo cha polisi cha Urafiki?
Shahidi: Madereva wenzake na baadhi ya majirani.
Mzee Mosi: Tangu huyo dereva aanze kazi kwako kuna siku aliwahi kutotimiza masharti uliyomuwekea?
Shahidi: Hapana.
Katika hatua nyingine, mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya Mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge Morogoro na dereva teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe amekerwa na kitendo cha kesi hiyo kuitwa kwa jina lake.
Kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2006 imesajiliwa katika mahakama hiyo kwa jina la Kesi ya jinai dhidi ya Jamhuri na ACP Abdallah Zombe na wenzake.
Akizungumza jana nje ya mahakama mara baada ya kesi hiyo kuahiriishwa, Zombe alihoji kwa nini watu wanaita kesi hiyo kesi ya Zombe badala ya kuiita kesi ya polisi.
"Kila mahali ni kesi ya Zombe kesi ya Zombe, kwa nini isiitwe kesi ya Polisi? Kwanza ni mema mangapi niliyafanya hapa. Nilikuwa nakosa usingizi kwa ajili ya kupambana na uhalifu na kulinda usalama, kwa nini leo hii hamnitaji kwa mema?" alihoji Zombe wakati akiingia ndani ya basi tayari kwa kurejeshwa mahabusu.
Katika hatua nyingine, watu wengi waliojitokeza katika mahakama hiyo walionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona mshitakiwa huyo wa kwanza wakati alipokuwa akitoka mahakamani.
Wananchi waliofika katika mahakama hiyo, ambao licha ya kumsikia tu kwa jina mshtakiwa huyo hawajawahi kumuona ana kwa ana, hivyo walionesha nia ya kutaka kumuona mshitakiwa huyo.
Mwananchi liliwasikia na kuwashuhudia baadhi ya wananchi hao wakiliuzana Zombe ni yupi miongoni mwa washitakiwa wengine waliokuwepo katika mahakama hiyo.
"Hivi huyo Zombe ni yupi? Mimi huwa namsikia tu sijawahi kumuona," alisikika mmoja wa wananchi hao akimuuliza mwenzake huku mwingine akidai kuwa naye hajawahi onana naye uso kwa uso, zaidi ya kumuona kwenye Luninga tu.
Kufuatia hali hiyo baadhi ya wananchi hao walimsubiri mshitakiwa huyo nje ya geti la mahakama hiyo na mara walipowaona watuhumiwa wakitoka nje ya mahakama hiyo, walisogea karibu huku kila mmoja akijitahidi kutafuta nafasi ili kuweza kumuona vizuri mshtakiwa huyo lakini wengi wao hawakufanikiwa.

No comments: