Thursday, June 12, 2008

ZOMBE LEO

DPP adai uchunguzi wa Tume ya Rais ulibainiwaliouawa hawakuwa majambazi



ALIYEKUWA Katibu wa Tume ya Rais ya kuchunguza tukio la vifo vya wafanyabiashara wa madini, Elieza Feleshi ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa tume hiyo, iliridhika kuwa wafanyabiashara hao, hawakuwa majambazi na wala hapakuwa na tukio lolote la kurushiana risasi kati yao na polisi.
Feleshi ambaye ni Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) alikuwa akitoa ushahidi jana katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara hao, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi na Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna Msaidizi(ACP ) Abdallah Zombe na askari wenzake 12.
Mbele ya Jaji Kiongozi wa Salum Massati anayesikiliza kesi hiyo, Feleshi ambaye ni shahidi wa 28 katika kesi hiyo, alidai kuwa tume hiyo ilibaini ukweli huo, baada ya kufanya uchunguzi uliowahusisha mashahidi 90.
Feleshi alidai katika mahakama hiyo kuwa, tume hiyo ilikuwa ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Mussa Kipenka na kwamba ilibaini kuwa wafanyabiashara hao walikamatwa na askari hao na kuondoka nao wakiwa hai.
Alidai Tume hiyo, haikuridhika na maelezo ya askari polisi waliyoyatoa katika tume hiyo, kwamba askari walirushiana risasi na wafanyabiashara hao.
Feleshi alidai kuwa askari hao walishindwa kuithibitishia tume hiyo ukweli wa tukio la kurushiana risasi katika eneo la tukio hilo.
“Tume haikuridhishwa na maelezo hayo, kwa sababu haikuona viashiria vya mapambano kati ya wafanyabiashara na askari katika eneo la tukio. Makamishna waliuliza uwezekano wa kutokea mapambano kati ya askari na wafanyabiashara, lakini wale askari walishikilia msimamo wao kwamba, walirushiana risasi. Tume ilibaki na mashaka na maswali mengi ambayo ilibidi tuyafanyie kazi,” alidai Feleshi.
Feleshi alidai kuwa baada ya Tume hiyo kuundwa na Rais Kikwete Januari 23, 2006 ilitembelea eneo la tukio kulikodaiwa kutokea mashambulizi hayo na hatimaye wafanyabiashara hao kuuawa.
“Kwanza tulitembelea eneo la Barabara ya Sam Nujoma mahali ambako ilidaiwa kutokea uporaji wa pesa za Kampuni ya Bidco tukioongozwa na SP Bageni,”alieleza Feleshi na kuongeza kuwa pia walitembelea eneo la ukuta wa Posta mahali , ambako ilisemekana kulitokea mapambano kati ya askari polisi na wafanyabiashara hao.
Alidai wakiwa katika eneo hilo la ukuta wa Posta Bageni alikiri kuwa alifika katika eneo hilo, akiwa na askari wake ili kufuatilia majambazi waliodaiwa kupora pesa za Bidco.
Alidai ukutani kulikuwa na matundu madogo yaliyokuwa yamezungushiwa alama yakidaiwa kuwa ni ya risasi za askari polisi zilizowajeruhi wafanyabiashara hao.
“Lakini tulipoangalia chini hapakuwa na damu wala ukutani. Ndipo Makamishna waliweka mashaka na kuuliza maswali ili kujiridhisha. Pia Makamishna walijiuliza iweje watu wanaoruka ukuta wajeruhiwe wote katika sehemu moja,” alidai Feleshi.
Feleshi alidai baadaye waliachana na SP Bageni na kwenda kuwahoji baadhi ya wakazi wa eneo hilo eneo la gereji.
Alidai miongoni mwa watu waliowauliza katika eneo hilo kama waliwahi kusikia milio ya risasi katika eneo hilo ni Mkuu wa Usalama wa eneo hilo, Thadeo Katabazi ambaye ni Askari Jeshi Mstaafu na anayeishi mita 12 kutoka mahali walikodaiwa kujeruhiwa wafanyabiashara hao.
Alidai watu wote waliohojiwa walisema kuwa katika eneo hilo, hawakuwahi kusikia milio ya risasi, wala kuona damu na kusikia habari za majambazi.
Feleshi alidai baada ya kutoka katika eneo hilo, walielekea eneo la Sinza Palestina ambako walikutana na watu wengi ambao walishuhudia wafanyabiashara wao wakikamatwa akiwemo Benadetha Ngonyani (Shahidi namba 2 katika kasi hiyo), ambaye wafanyabiashara hao walikuwa wemekwenda kwake siku hiyo waliyokamatwa.
“Benadetha alitueleza jinsi wafanyabiashara hao walivyofika nyumbani kwake na uhusiano wa wafanyabiashara hao na mumewe na jinsi wafanyabiashara hao, walivyokamatwa na askari polisi wakati wakitaka kuondoka,” alidai Feleshi.
Aliongeza kuwa Benadetha aliwaeleza kuwa baada askari kuwakamata, lilifika gari lingine dogo likiwa na askari watatu ambao waliwafunga pingu na kuwapekua wafanyabiashara hao.
“Benadetha alitueleza walipowapekua Sabinus alikutwa na bastola na katika gari lao wakakuta mkoba wenye pesa na baada ya hapo askari polisi waliondoka nao katika gari lao aina ya Pickup na gari la marehemu liliendeshwa na askari mmoja,” alidai.
Feleshia aliendelea kueleza kuwa baada ya kutembelea katika eneo hilo, walirudi ili kuanza kazi rasmi ya kuwasikiliza mashahidi wengine waliokuwa wamejitokeza baada ya kutoa tangazo katika vyombo vya habari kuwa mtu yeyote mwenye taarifa kuhusiana na tukio hilo afike mbele ya tume hiyo.
Akizungumzia utaratibu wa kazi wa tume hiyo, Feleshi alidai kuwa walitumia utaratibu wa kimahakama wakiongozwa na sheria ya uundaji wa tume za uchunguzi sura ya 23 na mashahidi ambao walikuwa wanaapishwa.Alidai kuwa katika uchunguzi wao waliongozwa na Hadidu za Rejea sita ambazo ni pamoja na kuchunguza vyanzo vya sababu na mazingira ya vifo vya wafanyabiashara hao na kuchunguza ukweli wa maelezo ya jeshi la polisi kuwa walihusika katika kupora fedha za Bidco.
Alizitaja hadidu za rejea nyingine kuwa ni kuchunguza majina ya marehemu, eneo walilokuwa wakiishi na kazi walizokuwa wakizifanya.
“Nyingine ilikuwa ni kuchunguza uhalali wa nguvu iliyotumiwa na askari polisi kama ilikuwa katika utaratibu wa kawaida na kutoa maoni na ushauri kwa tukio zima,” alidai Feleshi na kuongeza kuwa tume hiyo ilipewa siku 21 kukamilisha kazi.
Alidai baadaye waliwaita mashahidi na kuwasikiliza kuanzia Januari 26, 2006 katika Ukumbi wa Karimjee na kwamba tume hiyo, iliwahoji askari wote walioshiriki katika tukio hilo.
Pia alidai tume hiyo iliwahoji raia wa kawaida na kwamba kuna mashahidi wengine ambao tume iliwaita mara mbili akiwemo Zombe na Bageni.
Aliieleza mahakama hiyo kuwa sababu ya kuwaita akina Zombe mara mbili katika tume hiyo ni kwa kuwa maelezo yao yalikuwa na mkanganyiko kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa mfano katika taarifa ya polisi waliyoitoa Januari 15, 2006, polisi walisema watu wale waliuawa ndani ya gari wakati wakirushiana risasi na polisi, lakini baadaye yakaja maelezo kwamba yalitokea mapambano katika ukuta wa posta, maelezo ambayo hayakuwemo,” alifafanua Feleshi.
Feleshi hakuweza kueleza kama Zombe na Bageni walipoitwa katika tume hiyo, walieleza nini kuhusiana na tukio hilo.
Alidai kuwa maelezo ya mashahidi hao, yalichukuliwa kwa kumbukumbu za maandishi na kwa vinasa sauti 36.
Feleshi aliongeza kuwa baadaye tume hiyo ilikwenda hadi Mahenge Morogoro ambako walipata utambuzi wa marehemu hao kwa majina na kazi walizokuwa wakizifanya.
Miongoni mwa mashahidi hao alikuwemo baba mzazi na mjomba wa marehemu hao. Wengine walikuwa ni Inspekta Maganga wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ulanga ambaye alithibitisha kuwa Sabinus alikuwa akimiliki bastola baada ya kufuata taratibu zote halali na kwamba, hawakuwa na kumbukumbu zozote kama aliwahi kufanya uhalifu.
Alidai walikutana na Mathew Ngonyani (Shahidi wa pili) ambaye alikuwa akifanya nao kazi na kwamba, alithibitisha kuwa Sabinus mwishoni mwa Desemba alipata jiwe kubwa ambalo waliliita jiwe la mwaka kwa kuwa mwaka huo, hapakuwa na jiwe kubwa kama hilo.
“Ngonyani alielezea jinsi Sabinus alivyojiandaa na kuamua kwenda kuuza madini yake katika soko la Arusha na Dar es Salaam na kwamba hata yeye alimpa sehemu ya madini yake akamuuzie,” alidai.
Alidai pia tume ilifika katika Kijiji cha Epanko katika migodi ya marehemu hao na kukutana na wachimbaji walioajiriwa katika migodi hiyo na kuelezea jinsi jiwe hilo lilivyopatikana na kwamba lilikuwa na uzito wa kama kilo saba.
Alidai kuwa shahidi mwingine ni Shaaban Manyanya (shahidi namba 25), ambaye alipiga simu akiwa Zanzibar akiomba ulinzi ili aweze kufika mbele ya tume hiyo kutoa ushahidi na kwamba, alipofika alieleza kuwa yeye na wenzake walihusika katika uporaji wa pesa za Bidco.
Feleshi alidai kwa mujibu wa uchunguzi wa tume hiyo, iliridhika kuwa wafanyabiashara hao hawakuhusika na uporaji wa pesa za Bidco na wala hapakuwa na tukio la kurushiana risasi.
Baada ya maelezo ya ushahidi wake Feleshi, aliulizwa maswali mbalimbali na mawakili wa utetezi, Wakili Jerome Msemwa katika kumtetea mteja wake Zombe alinukuu Gazeti la Mwananchi la Februari 22 mwaka 2006 lililomkariri aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Adadi Rajabu kuwa Zombe hakuwa na hatia ya kushitakiwa mahakamani.
Akitumia gazeti hilo, Msemwa alidai kwa mujibu wa Rajabu na hata katika ripoti ya tume hiyo, haikupendekeza Zombe ashitakiwe kuhusiana na tukio la mauaji hayo, bali ilipendekeza achukuliwe hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuvuliwa ukamanda wa mkoa wa Rukwa na kuhamishiwa Makao Makuu ya Polisi.
Msemwa: Shahidi, kwa hiyo utakubaliana nami kuwa mshitakiwa wa kwanza katika ripoti ya tume hiyo, hakupendekezwa ashitakiwe mahakamani kwa mauaji?
Feleshi: Ripoti haikumzungumzia kwa sababu wakati huo hakuwepo katika orodha ya awali ya washitakiwa 15.
Gaudioz Ishengoma: Shahidi umezungumzia habari ya mashaka kwa sababu hamkuona damu je, umepata taarifa kuwa Mkemia wa Serikali alichukua udongo mahali pale na kupima akakuta hakuna damu ya binadamu?
Feleshi: Sijajihusisha na hilo.
Majura Magafu: Mlisoma ripoti ya timu ya uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi?
Feleshi: Ndiyo.
Magafu: Walisemaje?
Feleshi: Walisema wao wametoa maoni kwa kadri ya uchunguzi wao.
Denis Msafiri: Shahidi umeeleza kuwa tume ilipata mashaka kwa kutokukuta damu eneo la tukio je, utakubaliana nami kuwa mahali pale ni barabara ya umma tena yenye vumbi ambayo hutumika wakati wote na haikufungwa?
Feleshi: Ndio na kwa hali hiyo hata watu wangelishuhudia tukio hilo.
PP Mtaki: Shahidi umesomewa Gazeti la Mwananchi kuwa Adadi, alisema Zombe hatashitakiwa, Adadi alikuwa ni nani wakati huo?
Feleshi: Alikuwa ni DCI.
PP Mtaki: Je, ndiye alikuwa na mamlaka ya mwisho ya kumshitaki au kutomshtaki mtuhumiwa?
Feleshi: Hapana.
PP Mtaki: Nani alikuwa na mamlaka?
Feleshi: Ni DPP.
PP Mtaki: Kwa nini Zombe aliitwa mara mbili kwenye tume?
Feleshi: Ni kutokana na maelezo yenye mkanganyiko. Awali jeshi la polisi lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa watu wale waliuawa na polisi wakiwa ndani ya ukuta wa Posta haikuwepo ndio maana akaitwa tena.
Mshauri Kimoro: Shahidi umesema Bageni ndiye aliyetoa amri ya mashambulizi, je alitoa kwa kundi zima au kwa watu wangapi?
Feleshi: Kwa kundi zima.
Kimoro: Alisema ni askari wangapi walifyatua risasi?
Feleshi: Alisema wawili tu.
Kimoro: Je, tume ilibaini kulikuwa na uhalali wa nguvu iliyotumiwa na polisi katika tukio hilo?
Feleshi: Hapakuwa na uhalali kwa kuwa tayari wale watu walikuwa wamekamatwa na hakukuwa na haja ya kurushiana risasi.
Kesi hiyo imeahirishwa na itaendelea leo katika mahakama hiyo.

1 comment:

Anonymous said...

Mpoki, thanx bro. Niko Ohio, USA nilikuwa sijui nini kinaendelelea na hii case. Thanx to you