Wednesday, June 04, 2008

ZOMBE ZAIDI

Wananchi wakitoka usikiliza kesi ya akina Zombe katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, kesi hiyo imekuw akivutio sana!

Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam jana ilikataa kupokea vielelezo vya picha vilivyotolewa na upande wa mashitaka katika kesi ya mauaji inayomkabili Zombe na wenzake 12.
Hatua hiyo ilifuatia muda mfupi baada ya shahidi wa 18 katika kesi hiyo, Sajin Nasibu kuanza kutoa ushahidi.
Nasibu aliieleza mahakama kuwa anafanya kazi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kama mtaalamu wa kupiga picha katika kitengo cha utambulisho.
Alieleza Februari 22, mwaka 2006 akiwa kazini aliitwa na mkuu wake wa kazi na kupewa maelekezo ya kwenda kukagua tukio lililotokea Sinza la watu wanne kuuawa na polisi.
“Tulipewa maelekezo ya kupiga picha sehemu mbalimbali za tukio na tulipiga picha zaidi ya 10 na kuzikabidhi kwa timu ya wapelelezi tuliokuwa tumekwenda nao,” alieleza Nasibu.
Kabla shahidi huyo, hajaendelea kutoa ushahidi wake mmoja wa mawakili wa upande wa mashtaka, Angaza Mwaipopo aliiomba mahakama ipokee picha hizo na kuwa vielelezo katika kesi hiyo.
Hatua hiyo iliibua mjadala mkali baina ya pande mbili za mashtaka na utetezi na mmoja wa mawakili upande wa utetezi, Majura Magafu aliieleza mahakama kuwa wanapinga kupokelewa kwa vielelezo hivyo kwa kuwa hawakuelezwa kama vitatumika wakati wa kuendesha kesi.
“Katika vielelezo walivyosema kwamba vitatumika wakati wa kuendesha kesi hiki hawakukiorodhesha na katika sheria ya ushahidi sura ya 6 kifungu cha 3 kinaeleza kuwa picha ni kielelezo,”alieleza Magafu.
Jaji Kiongozi Salum Masati baada ya kusikiliza hoja zote alikataa kielelezo hicho kisipokelewe katika mahakama hiyo. Pia alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka la kutaka kuwasilisha hoja kuwa kielelezo hicho kipokelewe mahakamani leo.
Naye shahidi wa 17 katika kesi hiyo, Luteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Emmanuel Mkonga aliieleza mahakama kuwa Januari 7, mwaka 2006 alisafiri kutoka Mahenge kwenda Arusha kupitia Dar es Salaam akiwa na ndugu zake watano, wakiwemo marehemu Ephraim Chigumbi na Sabinus Chigumbi na kwamba walikuwa wakitumia gari la marehemu Jongo.
Alidai walipofika Arusha marehemu Ephraim na Sabinus walienda kwenye soko la madini na baada ya kurudi kwenye hoteli waliyofikia, aliwaona wakiwa na mkoba mkubwa uliokuwa umejaa hela ambazo hakujua zilikuwa ni kiasi gani.
Alieleza Januari 12, mwaka 2006 waliondoka Arusha na kurejea Dar es Salaam na siku hiyo, ndugu zake walifikia Hoteli ya Bondeni na yeye alikwenda kulala Keko kwa ndugu yao mwingine.
Alidai Januari 13, mwaka 2006 alipeleka gari gereji kwa ajili ya kwenda kupaka rangi na ndugu zake wengine walibaki hotelini.
“Januari 15, mwaka 2006 asubuhi nilienda gereji kufuatilia gari lakini ndugu yangu Vasco niliyekuwa nimeongozana naye alinieleza kuwa alipokea taarifa kutoka katika hoteli waliyokuwa wamefikia marehemu kuwa walikuwa hawajaonekana,” alieleza Mkonga.
Nasibu alidai kuwa baada ya kwenda kufuatilia katika hoteli hiyo na vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio, waliwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kuangalia na walipoingia katika chumba cha maiti walikuta miili ya ndugu zao ikiwa na majeraha sehemu za usoni.
Alidai wakiwa Muhimbili walivamiwa na watu wasiowaelewa ambao walikuwa wamevaa kininja na kuwakamata na kuwapeleka Kituo Kikuu cha polisi ambako walionana na Zombe.
“Tulipofika kwa Zombe alitamka kuwa sisi ni majambazi na akaniambia mimi kuwa ndiye kinara wao kule Mahenge na kwamba nilikuwa nawafundisha ujambazi, nilifadhaika sana,” alidai Nasibu.
Shahidi huyo alieleza waliwekwa mahabusu siku mbili na askari kuchukua maelezo yao na baadaye walitolewa nje na Zombe aliamuru waachiwe kwa kuwa hawakuwa majambazi.
Kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2006 kwa mara ya kwanza, Zombe na wenzake 12 walifikishwa mahakamani Septemba 28, mwaka juzi mbele ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Laurian Kalegeya ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Zombe alipandishwa katika mahakama hiyo, kwa mara ya kwanza Juni 9, saa 4.00 asubuhi na Juni 15 mchana alifutiwa shtaka la mauaji lilokuwa likimkabili peke yake mbele ya Kaimu Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Addy Lyamuya na kuunganishwa na wenzake 12 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi.

No comments: