SHAHIDI wa 15 katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake 12, Koplo C 7521, Xavery Joseph Kajela amedai kuwa alishinikizwa kubadili taarifa ya silaha na risasi alizowakabidhi baadhi ya watuhumiwa ili kuwalinda askari wenzake waliokabidhiwa silaha.
Akitoa ushahidi jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Koplo Kajela ambaye ni mtunza ghala la silaha katika Kituo cha Polisi Oysterbay, aliieleza mahakama hiyo kuwa siku tatu baada ya mauaji hayo, alishinikizwa na Mkuu wa Upelelezi wa kituo hicho, (OC-CID) SP Christopher Bageni kubadili taarifa ili kuonyesha kuwa baadhi ya risasi zilikuwa zimetumika katika mapambano ya askari na majambazi hao.
Akiongozwa na Naibu Kiongozi wa Waendesha Mashtaka wa Serikali, Jasson Kaishozi, Koplo Kajela alidai kuwa mbali na kushinikizwa kubadilisha taarifa ya idadi ya risasi zilizokuwa zimerejeshwa, pia SP Bageni alimwamuru ampatie askari mmoja silaha na risasi ili aende kufyatua porini.
Alibainisha lengo la shinikizo hilo, lilikuwa ni kuonyesha katika taarifa hiyo kuwa risasi ambazo zilikuwa zimepungua, ndizo zilizokuwa zimetumika katika mapambano baina ya askari na wafanyabiashara hao wa madini waliokuwa wameuawa kwa tuhuma za ujambazi.
Akisimulia zaidi mbele ya Jaji Salum Masatti anayesikiliza kesi hiyo, Koplo Kajela alidai kuwa siku ya tukio la mauaji ya wafanyabiashara hao, aliwakabidhi silaha baadhi ya watuhumiwa na kwamba wote walizirejesha zikiwa na idadi ya risasi walizokabidhiwa isipokuwa askari mmoja tu ambaye alitumia risasi kadhaa.
Koplo Kajela alifafanua kuwa Koplo Saad alimkabidhi bunduki aina ya SMG namba 3A0199P na risasi 30, lakini alirejesha bunduki na risasi 21 tu.
Alidai pia kuwa alimkabidhi Konstebo Rashid bunduki aina ya SMG namba 13059192 na risasi 30, alirudisha bunduki hiyo na risasi zote 30 wakati Koplo Rajabu alimkabidhi bastola aina ya Chinese na risasi nane ambazo pia alizirejesha zote.
Alidai askari wengine aliowakabidhi silaha hizo kuwa ni D 9321 Konstebo Rashid Mohamed, D 4656 Koplo Rajabu Hamis Bakari, ambao wote ni watuhumiwa walioko mahakamani na kwamba D 56 62 Koplo Saadi hadi sasa hajulikani aliko.
Aliendelea kudai baada ya kupokea na kuzikagua silaha hizo na kuandika taarifa katika kitabu cha kumbukumbu, siku tatu baadaye alipokea amri kutoka kwa SP Bageni kwamba anapaswa kubadilisha taarifa hiyo na kumpatia silaha na risasi Koplo Rajabu ili aende mahali popote afyatue risasi tatu na kisha kuandika taarifa nyingine kuwa risasi tatu zilitumika tofauti na taarifa ya awali kuwa askari huyo alirejesha risasi zote, alizokabidhiwa.
“Nilishinikizwa na uongozi yaani Mkuu wa Upelelezi kituoni (OC-CID) Christopher Bageni kuwa nimpe silaha na risasi Koplo Rajabu, ili akafyatue risasi tatu porini ili kumsaidia, kwani bosi alidai kuwa jambo hilo lilikuwa gumu,” alieleza Koplo Kajela.
Alidai kutokana na shinikizo hilo, alitii na kumkabidhi Koplo Rajabu silaha na risasi na kurekebisha kumbukumbu katika kitabu hicho ili zisomeke kuwa risasi tatu zilitumika wakati awali hazikutumika.
Mbali na maelezo hayo, katika mahojiano na mawakili wa upande wa utetezi Koplo Kajela alieleza zaidi kama ifuatavyo.
Wakili Gaudioz Ishengoma: Unapopokea silaha na kukagua taarifa huwa uzipeleka kwa nani?
Shahidi Koplo Kajela: Huwa ninampa mkuu wa kituo.
Ishengoma: Sasa unakubaliana na mimi kuwa mwenye amri ya mwisho ya kuruhusu silaha itoke ni (OCS) Mkuu wa Kituo?
Koplo Kajela: Afisa yeyote mwenye cheo cha kuanzia Gazzetted anaweza kuruhusu silaha itoke.
Ishengona: Unaifahamu PGO ni nini?
Koplo Kajela: Ndio ni mwongozo wa utendaji wa kazi wa Jeshi la Polisi.
Ishengoma: Nikisema kwa mujibu wa PGO OCS ndiye hutoa amri kuruhusu silaha itoke, tena kwa maandishi utasemaje?
Koplo Kajela: Pamoja na hayo.
Ishengoma: Hayo maagizo ya Bageni yalikuwa ya maandishi au ya mdomo?
Koplo Kajela: Verbally (ya mdomo).
Ishengoma: Kwa hiyo hayo maandishi mekundu katika marekebisho ya taarifa aliyaandika Bageni au wewe?
Koplo Kajela: Niliandika mimi.
Ishengoma: Katika kumbukumbu zako za utoaji wa silaha Kituo cha Polisi Oysterbay au mahali popote kuna mahali ambako kuna hizi taarifa ulizozieleza hapa leo?
Koplo Kajela: Taarifa ziko katika quotebook na hii ndio halisi.
Ishengoma: Kwa hiyo Tibaigana anaweza kuwa pale Central akakuagiza kutoa silaha ukatoa na hata bila maandishi?
Koplo Kajela: Ndio inakubalika kwani inaitwa ‘Verbal Command’.
Ishengoma: Hiyo amri ya SP Bageni ilikuwa ni halali?
Koplo Kajela: Ndio ilikuwa halali.
Ishengoma: Umesema wakati Bageni anakuamuru hivyo alikuambia kwamba unafanya hivyo ili kuwaokoa askari hao katika janga hili, je, huoni kama na wewe uliwasaidia?
Koplo Kajela: Nisingeweza kukataa kwa sababu ilikuwa ni hali ngumu na niliogopa.
Ishengoma: Lakini ulijua kuwa ilikuwa kinyume cha utaratibu?
Koplo Kajela: Nilijua, lakini nilishinikizwa.
Ishengoma: Kwa hiyo ‘uli-forge’?
Koplo Kajela: Ndivyo inavyoonekana.
Ishengoma: Wewe kama askari polisi mwenye uzoefu wa miaka zaidi ya 25 kazini, si unajua kuwa askari anaruhusiwa kutii amri halali tu?
Koplo Kajela: Kuna amri kwamba, tekeleza kwanza ndio uulize.
Ishengoma: Nikikuambia kwamba huna uthibitisho kuwa Bageni alikuamuru utii amri yake utasemaje?
Koplo Kajela: Nimesema ilikuwa ni Verbal Command, unatekeleza kwanza ndio unauliza.
Wakili Majura Magafu: Mbona kuna maneno mengi tu umeyazungumza hapa na katika ‘statement’ yako uliyoitoa polisi hayako?
Koplo Kajela: Ni kwa sababu niliapa kusema ukweli.
Majura: Umesema ulilazimika kubadilisha taarifa ya awali na kurekebisha kwa kalamu nyekundu mbona katika maelezo yako hayaendani na maelezo ya awali ulipohojiwa na askari polisi?
Koplo Kajela: Niliyoyasema leo ndio sahihi.
Magafu: Kwa hiyo utapenda kuiondoa ‘statement’ hii hapa mahakamani kama sehemu ya ushahidi?
Koplo Kajela: Mahakama ndio itachambua na kuona yapi ya kweli.
Koplo Kajela alipoulizwa na Wakili Magafu iwapo alishamwambia OCS wa Oysterbay kuwa Bageni alimshinikiza, alijibu wote ni askari polisi na kwamba asingeweza kumshtaki kiongozi kwa kiongozi mwenzake.
Naye shahidi wa 16, Ramadhani Mfaume Juma ambaye ni ndugu wa marehemu Juma ambaye ni dereva teksi aliiambia mahakama kuwa wakati wakiwa msikitini kwa ajili ya ibada ya kuaga mwili wa marehemu Juma, gari ya polisi ilifika ikiwa na askari waliokuwa na bunduki huku wameficha nyuso zao.
Alidai walipofika Zombe alisema watu waliowaua ni majambazi wala si kwamba wanawaonea.
Alidai ingawa alikuwa hajawahi kumwona Zombe, lakini kinachomfanya amkumbuke hadi sasa ni kwa kuwa alitangaza kupitia vyombo vya habari kuwa wamewaua majambazi na pia alipokwenda msikitini Muhimbili.
Mahojiano kati ya Wakili Moses Maira na shahidi Juma yalikuwa kama ifutavyo.
Wakili Maira: Kama nikisema ulikuwa umeona kivuli cha Zombe, kwani siku hiyo Zombe hakuwepo Muhimbili, bali alikuwa amekwenda Uwanja wa Ndege kwenye msafara wa Rais utasemaje?
Shahidi Juma: Kwani siku ina saa ngapi, je, mimi nikikuambia leo nilikuwa Manzese na sasa niko hapa hutakubali?
Wakili Majura Magafu: Nikisema siku hiyo Zombe alikuwa kwenye msafara wa Rais kuanzia asubuhi hadi jioni utasemaje?
Juma: Kwa kuwa unamtetea utasema hivyo, lakini mimi nasema alikuja na nilimwona.
No comments:
Post a Comment