SHAHIDI wa 23, katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge Morogoro na dereva teksi, SP Juma Ndaki, alidai mahakamani jana kuwa mshitakiwa wa kwanza ACP Abdallah Zombe alikasirika baada ya kukuta pesa zilizokamatwa kutoka kwa wafanyabiashara hao zilikuwa pungufu kinyume na kiasi alichoambiwa awali.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, jana ilielezwa kuwa baada ya Zombe kubaini upungufu huo, katika Kituo cha Polisi cha Urafiki jijini Dar es Salaam ambako zilikuwa zikihesabiwa na maofisa wenzake wa jeshi hilo, aliwaagiza maafisa wa jeshi hilo, fedha hizo zipatikane zote.
Fedha hizo zilipelekwa katika kituo hicho na ASP Ahmed Makelle ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi katika kituo hicho (OC-CID) na ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo.
SP Ndaki alidai fedha hizo zilihesabiwa mbele yake kama Mkuu wa Kituo hicho wakati huo, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (OC-CID) SP Christopher Bageni, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Magomeni SSP Matage na ASP Makelle
Akiongozwa na Naibu Kiongozi wa Waendesha Mashtaka wa Serikali (PP), Jasson Kaishozi, SP Ndaki alidai mbele ya Jaji Kiongozi wa Mahakama hiyo, Salum Masatti kuwa baada ya fedha hizo kuhesabiwa, zilipatikana Sh 2.775 milioni.
“Baada ya kumaliza kuhesabu, SP Bageni alihoji kwa nini pesa hizo zilikuwa ni kidogo wakati kulikuwa na taarifa kuwa pesa hizo ni kiasi fulani,” alieleza SP Ndaki.
SP Ndaki alidai kabla Makelle hajajibu swali hilo, aliingia Zombe na alipoelezwa kuwa kiasi cha pesa kilichopatikana, alisikitika na kusema kiasi hicho kilikuwa ni kidogo tofauti na kiasi halisi na ndipo akatoa agizo pesa hizo zipatikane zote mara moja na kisha aliondoka.
Awali, akisimulia tukio hilo lilivyotokea SP Ndaki alidai siku hiyo Januari 14, mwaka 2006, majira ya saa 12:00 alipata taarifa kwa njia ya mawasiliano ya ‘Radio call’ kuwa kulikuwa na tukio la ujambazi lililokuwa limetokea Barabara ya Sam Nujoma kwamba gari moja lilikuwa limeporwa pesa na majambazi.
Alidai baada ya kutoa taarifa hizo waliondoka askari watatu wa kitengo cha upelelezi (CID) kwenda eneo la tukio wakiwa na gari dogo aina ya Toyota namba T 262 AAP.
“Askari hao ni SP Makelle, ambaye ni mshitakiwa wa tatu, WP Jane ambaye ni mshitakiwa wa tano na Koplo Abenet ambaye ni mshitakiwa wa 10,” SP Ndaki aliwataja askari hao.
SP Ndaki alidai baada muda mfupi SP Makelle alimtaarifu kwa njia ya ‘radio call’ kuwa walikuwa wamewakamata majambazi hao wakiwa na pesa kiasi cha Sh5milioni, pamoja na silaha moja aina ya bastola.
Alidai baadaye walifika watu wawili katika kituo hicho, mwanamke na mwanamume wakiwatafuta ndugu zao waliokuwa wamekamatwa na polisi na kuuliza kama walikuwa wamefikishwa katika kituo hicho.
“Niliwajibu nilikuwa sijaona mtu yeyote aliyekuwa amekamatwa na nikawashauri waende kuangalia kituo cha Polisi cha Kijitonyama,” alidai SP Ndaki.
Kwa mujibu wa mwenendo wa ushahidi wa kesi hiyo, watu hao waliofika katika kituo hicho, kuwatafuta ndugu zao hao ni shahidi wa tano, Jane Joseph na shahidi namba nne Venance Mchami ambao ni wanandoa na ambao walikuwa ni wabia na mmoja wa wafanyabiashara waliouawa, Mathias Lunkombe.
“Baadaye walirudi tena na kusema kuwa huko nako hawakuwaona, nami nikawaambia kuwa nilikuwa bado sijaona mtu yeyote aliyekamatwa na kufikishwa katika kituo hicho,” alidai SP Ndaki.
Alidai muda mfupi baada ya watu hao kuondoka, lilifika gari moja dogo aina ya Toyota Chaser namba T 617AAS yenye rangi ya fedha, likiwa linaendeshwa na askari polisi kutoka Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
SP Ndaki alidai hakufahamu idadi ya askari waliofika katika kituo hicho kwa kuwa hakuwaona wakati wakiingia ila kwa kukisia walikuwa ni zaidi ya askari mmoja.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa katika mahakama hiyo, na shahidi namba nane, Rajabu Said katika kesi hiyo, gari hilo ni lile walilolitumia wafanyabiashara hao kabla ya kuuawa wakati walipokwenda Sinza kupeleka fedha kwa mke wa rafiki yao Ngonyani.
Alidai baada ya askari hao kukabidhi gari hilo, waliendelea kuwepo katika kituo hicho na baadaye majira ya usiku kati ya saa 3 na saa 4 alifika ASP Makelle, akiwa na gari aliloondoka nalo akiwa na wenzake kwenda kwenye tukio hilo.
Hata hivyo, SP Ndaki alidai haelewi kama askari wengine walioambatana na ASP Makelle, walirudi pamoja katika gari hilo kwani wakati huo, aliona gari hilo likiwa limeegeshwa pembeni na kwamba yeye na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Magomeni SSP, Matage, walikuwa wakiendelea na shughuli nyingine.
“Nusu saa baada ya ASP Makelle kufika, naye SP Bageni alikuja na kutukuta tumesimama na SSP Matage na alimwomba Matage awe shuhuda wa kilelezo kilichopatikana katika eneo la tukio wakati akikabidhiwa kielelezo cha fedha,” alidai SP Ndaki.
“ASP Makelle aliambiwa alete mkoba aliokuwa nao, naye akaleta ‘mkoba’ begi dogo jeusi ndipo tukaingia wote ofisini kwangu. Alipoufungua mkoba huo kulikwa na pesa na zilipohesabiwa zilipatikana Sh 2.775 milioni,” alidai SP Ndaki.
Alidai baada ya pesa hizo kuhesabiwa na kukuta zikiwa pungufu, Zombe alikasirika na kuondoka huku akiagiza fedha hizo zipatikane zote, haraka.
SP Ndaki alidai mara moja SP Bageni alibeba mkoba huo wenye fedha na kuondoka nao kuelekea katika kituo chake cha Oysterbay.
Mbali na maelezo ya ushahidi wa SP Ndaki pia alifafanua zaidi katika maswali na majibu baada ya mawakili wa upande wa utetezi kumhoji.
Wakili Jerome Msemwa: Shahidi umesema ASP Makelle alikuambia kuwa fedha hizo zilikuwa ni Sh5 milioni, je baada ya kukuta upungufu huo ulisikia kuna kiasi kingine kimepatikana?
Shahidi SP Ndaki: Siko ‘aware’.
Msemwa: Umesema wakati huo ulikuwa na SSP Matage, je kwa sasa yuko wapi?
SP Ndaki: Kwa sasa ni RPC. Rukwa (Kamanda wa Polisi Mkoa).
Msemwa: Unaweza kuiambia Mahakama hii Tukufu kwa Chain of Command ya jeshi la Polisi pale mzungumzaji mkuu alikuwa ni nani?
SP Ndaki: Alikuwa ni OCD Matage.
Msemwa: Nini majukumu ya OCD?
SP Ndaki: Hutoa oda kwa tatizo ama kwa jambo lolote.
Msemwa: Ni nini majukumu ya OC-CID?
SP Ndaki: Ni kufanya upelelezi.
Msemwa: Nikisema Zombe hakujileta pale bali aliitwa na OC-CID unasemaje?
SP Ndaki: Hilo sikulisikia.
Msemwa: Zaidi ya fedha kuna kitu kingine kilichofunguliwa pale?
SP Ndaki: Hapa nazungumzia kielelezo kilichopelekwa katika kituo hicho tu.
Msemwa: Je, ulisikia mtuhumiwa wa kwanza (Zombe) kwamba aliondoka na kitu chochote kuhusiana na tukio hilo?
SP Ndaki: Hapana.
Wakili Gaudiz Ishengoma: Shahidi, kiuongozi Matage na Bageni wanatofautiana?
SP Ndaki: Ndio, mmoja ni OCD na huyo ni OC-CID.
Ishengoma: Kwa hiyo Zombe alipofika aliyetoa ripoti ya tukio hilo alikuwa ni Matage?
SP Ndaki: Ndio, kwa sababu ndiye alikuwa mkubwa pale.
Ishengoma: Umesema hujui hasa tukio hilo la ujambazi lilitokea wapi ila kwa taarifa za awali uliambiwa kuwa ni Sam Nujoma, je, kiutendaji kulikuwa na tatizo lolote kwa Bageni kufika pale?
SP Ndaki: Hapakuwa na tatizo.
Ishengoma: Umesema awali pesa zilizotajwa katika ‘redio call’ zilikuwa ni Sh5 milioni, je ilikuwa ni busara Bageni kuondoka bila kuuliza kuwa pesa nyingine ziko wapi baada ya kukuta pungufu?
SP Ndaki: Ilikuwa ni lazima aulize kwa kuwa tukio hilo, lilitokea katika eneo lake.
Wakili Majura Magafu: Shahidi, umesema gari lililetwa kituoni kwako na askari kutoka Kituo cha Chuo Kikuu, je, gari hilo lilihusu tukio gani?
SP Ndaki: Sikuweza kujua.
Magafu: Wewe ndiye ulikuwa OCS wa Kituo cha Urafiki, kwa nini hukutaka kujua gari hilo, lililetwa kwako na askari wa kituo kingine?
SP Ndaki: Kwa kuwa nilikuwa na Boss wangu na alipaswa kuuliza.
Magafu: Nikikuambia gari hilo ndilo lililohusika katika tukio lililotuweka hapa nitakuwa nakosea?
SP Ndaki: Unakosea kwa sababu mimi sikujua.
Magafu: Umesema baada ya fedha zile kuhakikiwa na kupatikana Sh 2.775 milioni zikiwa pungufu, je, mshtakiwa wa tatu alitoa jibu gani?
SP Ndaki: Kabla hajajibu, ndio Zombe aliingia na kuagiza fedha hizo zipatikane mara moja zote.
Magafu: Kwa hiyo hadi leo hii wewe binafsi hujui upungufu wa fedha hizo, ulitokea katika mazingira gani?
SP Ndaki: Hilo sijui.
PP Kaishozi: Shahidi, umesema siku hiyo ya tukio mlikuwa mkitumia mawasiliano gani?
SP Ndaki: Tulikuwa tukitumia ‘radio call’.
PP Kaishozi: Kwa mawasiliano hayo, je, uliwahi kumsikia mtu yeyote akimuita Zombe ili aende katika kituo hicho?
SP Ndaki: Sikuwahi kusikia hilo.
PP Kaishozi: Umeulizwa kama gari lile lililopelekwa katika kituo hicho, lilisajiliwa kuwa limepokelewa, je, wewe ulikuwa mpelelezi katika suala hilo?
SP Ndaki: Mimi kama Commanding Officer nilipaswa kuangalia kama limesajiliwa.
PP Kaishozi: Ulifanya hivyo?
SP Ndaki: Ndio niliangalia na nikalikuta.
Mshauri wa Mahakama, Nicolas Kimolo: Shahidi umesema SP Makelle alikuambia kwamba majambazi wamekamatwa na Sh 5 milioni pamoja na silaha, je aliporudi kituoni ulipata taarifa kwake kuhusu silaha hiyo?
SP Ndaki: Sikupata taarifa maana mkuu wangu alikuwepo.
Magreth Mosi: SP Makelle alikueleza wamekamata majambazi wangapi na ni eneo gani?
SP Ndaki: Hakunieleza ni majambazi wangapi ila alisema ni eneo la Sinza.
Jaji Masatti: Baada ya kuwakamata SP Makelle alikuambia aliwapeleka wapi?
SP Ndaki: Hakuniambia.
Kesi hiyo itaendelea tena keshokutwa Jumatatu.
No comments:
Post a Comment