Thursday, June 05, 2008

ZOMBE

Daktari asema marehemu walipigwa risasi pamoja!


SHAHIDI wa 19 katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge Morogoro na dereva teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam, waliouawa na askari polisi wakidhaniwa ni majambazi, Dk Martin Phillip Mbonde, amedai mahakamani kuwa inaonekana wafanyabiashara hao, walikalishwa sehemu moja na kupigwa risasi kwa pamoja.
Dk Mbonde alitoa madai hayo jana, wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake 12, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam baada ya kuulizwa swali na Naibu Kiongozi wa Waendesha Mashtaka wa Serikali, Jasson Kaishozi.
Daktari huyo ambaye ni Muhadhiri Chuo Kikuu cha Muhimbili na mfanyakazi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Kitengo cha Uchunguzi wa Chanzo cha Vifo vya Binadamu (Pathology), alikuwa ni mmoja wa watu waliochunguza maiti za wafanyabiashara hao.
Mahojiano kati ya wakili huyo, mshauri wa mahakama na shahidi huyo, yalikuwa kama yafuatavyo.
Kaishozi: Shahidi, hebu ieleze mahakama hii je, ni nini ‘Pattern’ ya majeraha uliyoyaona kwa marehemu hao?
Dk Mbonde: Hali ya majeraha hayo inaonyesha kuwa ni kama vile marehemu walikalishwa mahali pamoja na wote kuanzwa kupigwa risasi.
Alipoulizwa na Mshauri wa Mahakama Magreth Mosi kuwa alijuaje au ni nini ambacho kinamfanya aseme kuwa marehemu walikalishwa sehemu moja na kupigwa risasi, shahidi huyo alisema majeraha yaliyokuwa sehemu moja tu katika miili ya marehemu hao, yalionyesha kuwa walikalishwa sehemu moja.
“Hii ni kwasababu kuwa mahali risasi zilipoingilia na mahali zilipotokea ni sehemu moja tu. Kama kungekuwa na mapambano ya kurushiana risasi basi risasi hizo zingekuwa zimeingilia katika sehemu tofauti tofauti katika miili,” alidai Dk Mbonde.
Awali akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Kaishozi kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Salum Masatti anayesikiliza kesi hiyo, Dk Mbonde alidai marehemu wote walikuwa na majeraha ya risasi walizopigwa shingoni kwa nyuma na kutokezea mbele.
Dk Mbonde alifafanua kuwa marehemu Ephraimu Chigumbi alikuwa na majeraha matatu, sehemu za usoni, mkononi, kifuani na shingoni.
Alidai Chigumbi alipigwa risasi shingoni kwa nyuma, ambayo iliacha jeraha lenye ukubwa wa sentimita moja kwa moja na kutokea mbele mdomoni sehemu ya kulia na kuacha jeraha lenye ukubwa wa sentimita nane kwa nane.
Shahidi huyo, alidai risasi hiyo ilimvunja taya na baadhi ya meno na kupasua mishipa ya damu na kusababisha damu nyingi kuvuja na kwamba chanzo cha kifo chake ni majeraha ya risasi hiyo.
Aliongeza kuwa marehemu Sabinus Chigumbi (Jongo) alipigwa risasi mbili, moja shingoni kwa nyuma na kuacha jeraha lenye ukubwa wa sentimita moja kwa moja na kutokea mbele karibu na taya la chini na kuacha jeraha la ukubwa wa sentimita sita kwa nne.
Alidai risasi ya pili alipigwa katika mkono wa kushoto na kutokea kwa nyuma na kwa mbele, hivyo kuacha jeraha la ukubwa wa sentimita sita kwa sita na ilivunja mifupa na kupasua mishipa ya damu na kusababisha damu nyingi kuvuja na kwamba risasi hizo, zilikuwa chanzo cha kifo chake.
Kuhusu marehemu Mathias Lunkombe, Dk Mbonde alidai marehemu huyo alikuwa na majeraha matatu ya risasi na kwamba risasi moja ililengwa kwenye taya la kulia na kuacha jeraha kubwa la sentimita moja kwa moja na kutokea kushoto chini ya taya.
“Risasi nyingine mbili alipigwa shingoni katika pingili ya nne ya mfupa wa shingo na kuvunjika mataya na ubongo kuathirika pamoja na mishipa ya damu kupasuka na kusababisha damu nyingi kuvuja. Hivyo chanzo cha kifo hicho kilikuwa ni majeraha ya risasi za bunduki,” alidai Dk Mbonde.
Akisimulia sababu za kifo cha dereva teksi, Juma Ndugu, Dk Mbonde alidai alikuwa na jeraha moja la risasi iliyovunja pingili ya sita ya mfupa wa shingo kwa nyuma na kuacha jeraha lenye ukubwa wa sentimita moja kwa moja na kutokea mbele na kuacha jeraha lenye ukubwa wa sentimita sita kwa sita.
Aliongeza kuwa risasi hiyo, ilivunja pingili ya sita ya shingo ya marehemu Ndugu na kuumiza uti wa mgongo jambo lililosababisha kuvuja kwa damu nyingi na hatimaye kufariki dunia.
Baadaye alipoulizwa na wakili wa upande wa utetezi, Jerome Msemwa iwapo marehemu walikuwa na majeraha mengine katika miili yao kama vile kukatwa sehemu za viuongo vyao Dk Mbonde alidai hakuwahi kuona.
Alieleza kuwa kama mtu angeliangalia kwa haraka jeraha hilo, angedhani marehemu Juma alikatwa shingoni kwa kitu chenye ncha kali kwa kuwa risasi ilichana ngozi ya sehemu ya shingoni.
Mbali na wakili Msemwa, Dk Mbonde alihojiwa na mawakili wengine wa upande wa utetezi na sehemu ya mahojiano yao ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Gaudioz Ishengoma: Shahidi ulipoulizwa na msomi mwenzangu, ulisema hujawahi kuwa askari polisi na wala huna utaalamu wa risasi, je, majeraha yale kwa asili hakuna kitu kingine kinachoweza kusababisha majeraha yale?
Dk Mbonde: Hakuna
Ishengoma: Je ulifanya upasuaji wa miili ya wale marehemu?
Dk Mbonde: Ndio.
Ishengoma: Je, ulikuta risasi ndani?
Dk Mbonde: Hapana.
Ishengoma: Sasa ulijuaje kuwa hayo ni majeraha ya risasi?
Dk Mbonde: “Kuna tofauti kubwa sana kati ya jeraha la risasi na jeraha la mshale au kitu chochote chenye incha kali. Kwanza, risasi ikiingia mwilini inapenya na kutokeza nje tofauti na vitu vingine vyenye ncha kali, lakini pia risasi inapoingia mwilini inavunjavunja mifupa, lakini vitu vyenye ncha kali kama kisu haviwezi kuvunja mfupa”.
Mbali na Dk Mbonde, shahidi mwingine namba 18, E.5448 Sajenti Nasibu Masoud anayefanya kazi Makao Makuu ya Polisi kitengo cha picha aliiambia mahakama kuwa, siku chache baada ya tukio la mauaji hayo, aliagizwa na mkuu wake wa kazi, SP Hamis kwenda kupiga picha Sinza C mahali ambako wafanyabiashara hao walikamatwa.
Shahidi Masoud akiongozwa na PP Angaza Mwipopo, alidai akiwa Sinza C alipiga picha zisizopungua nane katika maeneo tofauti tofauti, ikiwamo iliko nyumba ya Ngonyani ambaye ni shahidi wa kwanza kwenye kesi hiyo, ambako marehemu walikamatwa.
Alidai picha nyingine alipiga sehemu ya ukuta wa kibanda walikokuwa wamekaa akina Mjatta ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo na nyingine alipiga eneo lilipopaki gari la marehemu na eneo lingine ambako Mama Ngonyani (shahidi namba mbili) na marehemu Jongo walikokuwa wamekwenda kuzungumza.
Masoud alidai mbali na eneo hilo la Sinza C pia alikwenda kupiga picha eneo la ukuta wa Posta ambako ilisemekana kuwa ndiko marehemu walikouawa wakati wakijibizana na askari polisi.
Alidai alipiga picha hizo akiongozwa na mkuu wake wa kazi aliyeambatana naye, Kaimu Kamishna Msaidizi Mkuu wa Polisi (SACP) Mkumbi na kwamba, katika ukuta huo kulikuwa na matundu manne madogo ambayo yalidaiwa kuwa ni ya risasi zilizotokana na mapambano.
Alifafanua kuwa hakuwa na uhakika kama matundu hayo yalikuwa ni risasi ila yalionekana kwamba yalikuwa matundu madogo yaliyozungushiwa alama ya duara kwa kutumia chaki.
Alidai matundu hayo yalionekena kupishana, lakini kwa umbali mfupi na kwamba alisafisha picha hizo na kuziweka katika albam na kuzikabidhi makao makuu.
Naye shahidi wa 20 katika kesi hiyo, Issa Salum (52) aliieleza mahakama kuwa wakati akiwa mlinzi katika gereji iliyoko Sinza C, hakuwahi kusikia milio ya risasi wala bunduki.
Shahidi huyo alidai alikuwa mlinzi kwenye gereji hiyo kwa muda wa miaka mitatu na kwamba, kipindi cha mwezi Januari mwaka 2006 hakuwahi kusikia milio yoyote ya risasi ama kuona tukio lolote la ujambazi katika eneo hilo.
Kesi hiyo namba 26 ya mwaka 2006 kwa mara ya kwanza, Zombe na wenzake 12 walifikishwa mahakamani Septemba 28, mwaka juzi mbele ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Laurian Kalegeya ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Zombe alipandishwa katika mahakama hiyo kwa mara ya kwanza Juni 9, saa 4:00 asubuhi na Juni 15 mchana alifutiwa shtaka la mauaji lililokuwa likimkabili peke yake mbele ya Kaimu Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Addy Lyamuya na kuunganishwa na wenzake 12 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi.
Jaji Masati anayesikiliza kesi hiyo aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea tena.



















No comments: