Friday, August 01, 2008

MAMBO YA MALYA HADHARANI

Kumbe mallya ndiye aliyemwendesha Chacha!!!Malya (kushoto) akisaidiwa kuingia hospitali ya General Dodoma baada yakupata ajali na Chacha, yeye alidai hajui kuendesha!

KIFO cha Mbunge wa Tarime Chacha Wangwe, kimezidi kugubikwa na giza nene baada ya fundi magari katika gereji iliyoko eneo la Sido mjini hapa kusema kwamba, mtu anayedaiwa kuwa dereva wa gari iliyopata ajali na kuumua mbunge huyo, Deus Mallya, ndiye aliyeendesha gari la marehemu hadi gereji kabla ya safari siku ya ajali.
Maelezo hayo ya fundi huyo Israel Remen, ambayo yanashabihiana na ya watoto wa marehemu, yanapingana na kauli ya Mallya ambaye alikuwa katika gari moja na marehemu Wangwe, lakini (Mallya) anadai kwamba hajui kuendesha gari.
Akizungumza na gazeti hili katika gereji hiyo iliyopo karibu na ofisi za Shirika la Sido, Remen alisema, awali marehemu alipita na Mallya na kusema gari lingerudishwa na rafiki yake huyo kutengenezwa.
Alizidi kusimulia kwamba, baadaye Mallya alilifikisha gari hilo gereji hapo akiwa analiendesha na likafanyiwa matengenezo mbalimbali
Remen alitaja matengenezo hayo kuwa ni pamoja na kumwaga mafuta machafu (oil) na matengenezo mengine madogodogo.
Hata hivyo, alisema baadaye mnamo saa 12.00, Mallya alirudi tena safari hiyo akiwa na marehemu na kutakiwa kukaza sukrubu za tairi la kulia la nyuma.
“Alivyokuja, alikuwa na mheshimiwa (marehemu) ambaye alikaa kiti cha mbele akiwa amekilaza, mimi nikamwambia mheshimiwa usipate tabu kushuka kaa hapo hapo, basi nikakaza kisha wakaondoka Mallya akiwa anaendesha,” alisisitiza.
Fundi huyo alipoulizwa kwamba aliwahi kumwona Mallya akimwendesha marehemu kabla, alijibu: “Si mara moja, nilimwona sana, hapa mjini ndiye alikuwa akimwendesha, hata siku chache zilizopita niliwakuta mjini na wakanipungia mkono.”
Kwa mujibu wa Remen, tayari yeye amehojiwa na polisi na alipelekwa hospitali mkoani hapa kwa ajili ya kumtambua Mallya, na kuongeza kwamba alithibitishia polisi kwamba ndiye aliyefika na gari hiyo akiwa anaendesha.
“Nashangaa anaposema hajui kuendesha gari, alikuja hapa na gari akiwa ndiye anaendesha, na si mara ya kwanza, hata mjini alikuwa akimwendesha mheshimiwa,” alifichua siri.
Kauli hii ya fundi gereji huyo inazidi kuibua mjadala na utata kuhusu mazingira ya kifo cha Wangwe ambaye alikufa Jumatatu usiku, eneo la Pandambili, Wilayani Kongwa akiwa safarini kwenda Dar es Salaam kuwahi mazishi ya mbunge wa kwanza wa Tarime, Bhoke Munanka.

1 comment:

EDWIN NDAKI (EDO) said...

Mwisho ili swala lipo wazi,Mallya unaweza kuta ndio wale vijana "wapambe" wa waheshimiwa.Na ukweli utajulikana huyo dogo ni kweli ajali inatokea alikuwa anaendesha.Kaona hana leseni ndio ikabidi abadili habari.

tutafika tu.

RIP Ras Chacha Zakayo WANGWE