Friday, September 26, 2008

KICHAPO CHA MTIKILA

Uropokaji wamponza
Mch. Mtikila Tarime

HALI imezidi kuwa mbaya kwenye kampeni za uchaguzi wa mbunge na diwani wilayani Tarime, baada ya Mwenyekiti wa chama cha Democratic, Mch. Christopher Mtikila kushambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa vibaya na wananchi wenye hasira, baada ya kudai kwenye mkutano wa hadhara kuwa Chadema ilimuua mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Chacha Wangwe.
Mashambulizi hayo ya aina yake yamekuja siku moja baada ya Kamanda wa Operesheni ya Jeshi la Polisi, Venance Tossi kutangaza kuwa atatumia nguvu kudhibiti wafuasi wa vyama vya upinzani -Chadema na CUF- kwa madai kuwa wana vurugu, ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi wa Chadema kuuawa kwa risasi katika mapigao yanayodaiwa kuwa ya ukoo.
Mtikila, ambaye ni maarufu kwa ushujaa wake wa kutoa tuhuma kali bila ya woga, aliwahi kutoa tuhuma hizo kwa Chadema mapema mwezi huu, akihusisha kifo cha mbunge huyo wa Jimbo la Tarime na mgongano wa kikabila ndani ya chama hicho na kumuhusisha mfanyabiashara mmoja maarufu.
Lakini jana, wakazi wa Tarime hawakumruhusu kuendelea kushusha tuhuma nzito kwa Chadema, na badala yake wale waliokuwa akiwahutubia ndio walioamua kumshambulia kwa mawe na kumjeruhi kiasi cha kushonwa nyuzi saba.
Mchungaji huyo wa makanisa ya ufufuo alikuwa ameanza kueleza kifo cha Wangwe, ambaye alifariki kwenye ajali ya gari ndogo wakati akisafiri kutoka Dodoma kuelekea Dar es salaam, kuhudhuria mazishi ya mfanyabiashara Bhoke Munanka.
Wakati akiendelea kuwahutubia wananchi na kuituhumu Chadema kuwa ndio iliyomuua mbunge huyo wa zamani wa jimbo hilo, ghafla alipondwa na jiwe baada ya kuwa amegeuka upande wa kulia na hivyo kujeruhiwakichwani.
Shambulizi hilo lilisababisha mkutano huo wa hadhara kukatishwa, wakati wasaidizi wake walipoanza harakati za kutafuta usafiri wa kumkimbizia, hospitali ambako alitibiwa na kushonwa nyuzi saba.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Shule ya MsingiSabasaba iliyopo Tarime.
Kifo cha Wangwe kilizua utata mkubwa kutokana na uhusiano wa muda mfupi baina yake na kijana anayedaiwa kuwa alikuwa akiendesha gari hilo, Deus Mallya, ambaye kwa sasa amefunguliwa mashtaka ya makosa yanayohusiana na usalama barabarani, mazingira ya ajali hiyo na mtu hasa aliyekuwa akiendesha gari hilo.
Awali ilisemekana kuwa Wangwe, ambaye alikuwa akijulikana sana kwa kuzua hoja tata bungeni, aliuawa kwa kupigwa risasi, lakini baada ya uchunguzi ilibainika kuwa kifo chake hakikutokana na kushambuliwa kwa risasi.
Lakini Mtikila amekuwa akishikia bango kifo hicho na wiki chache zilizopita aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwarushia shutuma viongozi wa Chadema na mfanyabiashara mmoja kuwa ndio waliosuka njama za kumuua Wangwe, ambaye alikuwa akiripotiwa kuwa na mgogoro na viongozi wenzake wa chama hicho kiasi cha kusimamishwa wadhifa wake wa makamu mwenyekiti.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutibiwa, Mch. Mtikila alisema analitupia lawama Jeshi la Polisi kutokana na shambulio hilo la mawe, ambalo anadai kuwa alishalitaarifu mapema kuwa kulikuwa na njama ambazo alidai zilipangwa na Chadema.
Mchungaji huyo matata alisema mara baada ya kufika mjini Tarime, alipata taarifa za kufanyika kwa mkutano wa kiongozi mmoja wa Chadema na kwamba, katika mkutano huo, kiongozi huyo aliwaagiza wafuasi wake kuhakikisha wanamshambulia kwa mawe ili kumdhibiti yeye asisambaratishe chama hicho.
“Nilitoa taarifa mapema kwa Msimamizi wa Uchaguzi na OCD, niliwaeleza juu ya agizo la mimi kupigwa mawe, lakini nashangaa polisi hawakuweza kuleta ulinzi mkali kwangu licha ya kutoa taarifa hiyo,” alieleza mchungaji huyo.
Alisema kitendo cha kupigwa mawe si cha kiungwana na kwamba kimemsikitisha kwa kuwa anaamini kuwa siasa ni majibizano na hoja na wala si vurugu.
Hata hivyo, Mchungaji Mtikila alisema kuwa hatasitisha kampeni zake na kwamba leo ataendelea na kampeni za chama chake kumnadi mgombea wake Mchungaji, Denison John Manyika.
Kabla ya mkutano huo, Mtikila alifanya mkutano katika kijiji cha Nyamwaga na Sirari ambako alikuwa akisisitiza na kueleza kuwa marehemu Wangwe ameuawa.

4 comments:

Unknown said...

Huyu Gangwe ni mchochezi sana, ingependeza kama angeongezewa kipigo zaidi na zaidi na zaidi; hadi ajue kuwa mdomo wake unajambaga.

Alivyo limbukeni anajikomba kwa CCM ili aweze kurudia tena ile chati ya ke ya siasa ambayo alionekana kuwa ni fisadi baada ya kuchukua fedha kwa Rostam Azizi.

Anonymous said...

Ufisadi ndio kula yake, hana kitu tena baada ya kupokea pesa ya Rostam sasa anavalia kifo cha Wangwe. Wakiweza wampige mpaka mdomo wake umwagike.

Unknown said...

Shauri yake, Arudi kanisani kuhubiri, aanchane na siasa. Maana akicheza hizi siasa zitamtoa roho.

Unknown said...

Iko sikia kuwa hii kimutu iko malizika kabisa na imesha achana na nyama.

Kama ningekuwepo ningeipiga kwa nsale wa lumbo ikufilie mbali