Friday, September 26, 2008

ZOMBE LEO

Damu ilikuwa ya binadamu, asema Mkemia


RIPOTI ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa damu iliyokuwa kwenye udongo uliochukuliwa katika msitu wa Pande ulio Mbezi Louis jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni damu ya binadamu, mahakama ilielezwa jana.
Damu hiyo ni moja ya ushahidi katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es salaam inayomkabili mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake 12 inayoendelea 'kurindima' Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es salaam.
Akitoa ushahidi jana, mkemia mkuu daraja la pili kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias, ambaye ni shahidi wa 37 katika kesi hiyo, aliieleza Mahakama Kuu kuwa licha ya damu hiyo kuwa ya binadamu, alishindwa kutambua makundi ya damu hiyo.
Akitoa ushahidi huo mbele ya Jaji Kiongozi Salum Masatti anayesikiliza kesi hiyo huku akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali (PP), Angaza Mwipopo, Elias alidai alipokea sampo ya udongo huo, Machi 9, 2006 kutoka kwa afisa makao makuu ya polisi, Omar kuufanyia uchunguzi udongo huo ili kujua kama una damu au la.
Elias alieleza kuwa katika fomu ya maswali iliyotoka polisi alitakiwa kuchunguza kwanza kujua kama udongo huo una damu, pili kujua kama ni damu ya mnyama au ni ya binadamu na kisha kujua kuwa damu hiyo iko katika kundi gani.
Katika kutambua kama damu hiyo ni ya mnyama au ni ya binadamu Elias aliieleza mahakama hiyo kuwa, walitumia kemikali maalumu ambayo huchanganywa na vielelezo hivyo ili kubainisha matokeo yanayojulikana ‘Anti-Sera’.
“Baada ya kufanya uchunguzi nilibaini kuwa udongo ule ulikuwa na damu na kwamba damu ile ilikuwa ni ya binadamu, lakini sikuweza kubaini kuwa damu ile ilikuwa katika kundi gani kwa kuwa seli za damu ambazo zingeweza kubainisha kundi zilikuwa zimeharibika,” alidai Elias wakati akisoma ripoti yake ya uchunguzi huo.
Awali jana asubuhi, shahidi wa 36 katika kesi hiyo alidai kuwa walishindwa kupata kumbukumbu za mawasiliano ya simu kati ya Zombe na Christopher Bageni kwa sababu kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ilikuwa imeshafuta kumbukumbu hizo.
Shahidi huyo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Sydney Mkumbi alidai katika mahakama hiyo, kuwa walipoenda Vodacom kati ya Juni na Julai mwaka 2006, waliambiwa kuwa kumbukumbu za mawasiliano za Januari 14, mwaka 2006 zilikuwa zimeshaharibiwa.
“Vodacom walisema huwa wanaharibu kumbukumbu kila baada ya miezi sita na sisi tulipokwenda walisema kumbukumbu za Januari 14 mwaka 2006 tayari zimeharibiwa,” alidai Mama Mkumbi.
Shahidi huyo alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuieleza mahakama kuwa siku ya tukio Zombe na Bageni, ambaye ni mshitakiwa wa pili, walikuwa wakiwasiliana kwa simu ya upepo na simu ya kiganjani.
Alidai hawakufuatilia kujua kumbukumbu za mawasiliano ya simu ya upepo kwa siku hiyo ya tukio kwa sababu walifikiri kuwa hazikuwa na umuhimu.
Shahidi huyo pia alidai karibu washitakiwa wote waliandika maelezo yao upya wakati walipokuwa mahabusu na kwamba, maelezo yao hayatofautiani na ya mshitakiwa wa 11 na 12.
Wakati mawakili wakimuhoji shahidi wa 37 kuhusu uchunguzi wa damu, sehemu ya mahojiano ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Majura Magafu: Shahidi, utakubaliana na mimi kuwa kitambulisho cha damu huwa ni chembechembe na si rangi?
Shahidi: Ndio kuna chembechembe zinazounda damu lakini mimi ninazungumzia zinazoweza kutambulisha kundi la damu.
Jaji: Umelielewa swali lake?, alihoji jaji Rudia swali ili shahidi asikie vizuri (Magafu alirudia swali hilo na shahidi alijibu “Ndio”).
Wakili: Kwa hiyo hizo seli ndizo zinazoweza kutambulisha kuwa hii ni damu na hii siyo damu?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Ni muda gani ambao seli zinaweza kubainisha hii ni damu au la?
Shahidi: Hutegemea hali ya mahali ambako damu ipo na kwamba kama mvua imenyesha katika eneo hilo.
Wakili: Ndio maana ninauliza kama mvua inanyesha, au inapigwa na jua na wadudu wanapitapita, je inachukua muda gani hadi seli kuharibika, ni wiki nane, ama siku mbili au ni muda gani?
Shahidi: Kama mvua inanyesha si rahisi kuweza kutambua aina ya kundi la damu.
Jaji: Mbona unakimbilia kundi? Anauliza ni muda gani hadi damu iharibike?
Shahidi: Inategemea muda na hali inayoizunguka damu hiyo mahali ilipo.
Wakili: Sasa katika mazingira hayo itachukua muda gani, mwezi wiki mbili siku tatu, je, inachukua muda gani hadi isiweze kutambulika?
Shahidi: Mazingira niliyotaja yakitokea inaweza kuharibika.
Wakili Rongino Myovela: Shahidi, ni wakati gani hiyo kemikali ya Anti-sera inashindwa kutoa matokeo sahihi?
Shahidi: Kwanza inategemea na uhifadhi wake, ni lazima iwe imehifadhiwa katika hali inayostahili kwa mfano katika friji, lakini kama ikitolewa nje haiwezi kufaa tena.
Wakili: Nani anatunza friji inayohifadhi kemikali hiyo?
Shahidi: Inatunzwa katika ofisi ya mkemia mkuu.
Wakili: Wewe unafriji hiyo ofisini kwako?
Shahidi: Sina.
Wakili: Nikisema kwa sababu wewe siyo mtunza friji ya kemikali hiyo bali ni mtu mwingine kwa hiyo, huna uhakika kama zilitunzwa sahihi na kwamba kwa hali hiyo hata yale matokeo hayakuwa sahihi utasemaje?
Shahidi: Si kweli.
Wakili: Kwa nini?
Shahidi: Lazima kabla ya kuanza uchunguzi tuna-‘test ant-sera’ kama inafanya kazi, kama ikikataa huna haja kuendelea nayo tena.
Wakili: Katika utambuzi wenu wa damu kama ni ya binadamu au ni ya mnyama kuna asilimia ngapi za kutokea makosa?
Shahidi: Zile kemikali makosa yake huwa ni kidogo sana mara nyingi usahihi wake ni asilimia 99.9.
Wakili: Wewe ulipata wapi hizo takwimu?
Shahidi: Kutokana na kumbukumbu za ubora wa chunguzi tunazozifanya.
Wakili: Nikisema hiyo asilimia 0.1 inayosalia ndio ilisababisha matokeo yasiyo sahihi katika uchunguzi wako unaoutolea ushahidi huu unasemaje?
Shahidi: Usahihi niliousema ndio huo huo.
Wakili: Kwa kuwa utaalamu wako na shule yako, huwezi kueleza zaidi ya hapo, aliuliza wakili Myovela huku akikaa.
Wakili Denis Msafiri: Shahidi, umesema ulibaini kuwa ile ilikuwa ni damu, lakini udongo una mchanganyiko wa vitu vingi, je, una uhakika gani kama ile kemikali haikuweza kuharibiwa na udongo hivyo ikashindwa kutoa matokeo sahihi?
Shahidi: Kabla ya kufanya uchunguzi, tunaifanyia majaribio ile kemikali na kuitenganisha na damu na udongo.
Wakili: Umesema ulishindwa kubaini makundi ya damu je, naweza kuwa sahihi nikisema ile sampuli ya udongo uliyoletewa ilikuwa ni moja lakini ikagawanywa katika sehemu nne?
Shahidi: Sababu nilizozitoa ni kwamba chembechembe za damu zilikuwa zimeharibika. Kama ilikuwa ni moja au ngapi mimi sijui.
Wakili:Unafahamu mchanganuo wa udongo?
Shahidi: Nafahamu.
Wakili: Je, uliweza kuchunguza kama udongo ule ulikuwa ni wa aina moja au aina tofauti tofauti?
Shahidi: Maombi ya uchunguzi niliyoletewa yalikuwa ni kutambua kama katika udongo huo kuna damu, na kama damu hiyo ni ya binadamu au ya mnyama na pia kutambua makundi ya damu hiyo, Hivyo mimi nilibaki kwenye maswali niliyotakiwa kuyatolea majibu tu, alijibu shahidi huyo huku washauri wa mahakama wakitikisa vichwa.

No comments: