Tuesday, September 23, 2008

KIZUNGUMKUTI NMB

Wateja wa benki ya NMB wakizubiri labda tawi la Mlimani City lingefunguliw ajana jioni lakini wapi!
Sehemu pekee wateja waliweza kupata pesa ilikuwa katika mashine za ATM lakini baadae ntyingine zilizidiwa na kuwataka wateja wasubiri baadae.
Wakati mambo yakiwa magumu kwa wateja wafanyakazi walikuwa wamejikusanya Msimbazi Centre wakisubiri matokea ya kusainiwa mkataba baina ya uongozi wa benki na Serikali lakini wapi!
Mkurugenzi Mkuu wa NMB Ben Christiaanse akizungumza na wahandishi wa habari katika makao makuu ya NMB,akisema tatizo si wao bali ni serikali.Kulia ni Afisa Utumishi Mkuu Kabeho Solo

HALI ya simanzi, vilio, kufoka na ulalamishi ilitanda karibu katika matawi yote ya Benki ya NMB jana baada ya wateja wa kampuni hiyo kushindwa kupata huduma kutokana na mgomo wa wafanyakazi.
Hali hiyo ilitokea kwa wateja ambao walitaka kutuma, kuweka au kuchukua fedha, lakini wakakuta milango ya matawi ya benki hiyo ikiwa imefungwa huku mashine za kuchukulia fedha, ATM, zikiwa na maneno “Samahani mashine hii haitumiki kwa sasa, tafadhali jaribu tena baadaye au tumia mashine nyingine”.
Wafanyakazi hao walianza mgomo huo kuishinikiza serikali kusaini mkataba wa malipo ya mkupuo ya mafao waliyostahili kupata wakati benki hiyo ikibinafsishwa kwa mwekezaji wa sasa.
Pia wanadai kutengewa asilimia tano ya hisa ambazo benki hiyo imeanza kuziuza, mafao kwa wafanyakazi na fedha na mfuko wa kujikopesha.
Mkataba huo, uliokubaliwa na pande zote- wafanyakazi, menejimenti ya NMB na serikali-, ulitakiwa usainiwe Agosti 27 kabla ya kusogezwa mbele hadi Agosti 28, lakini serikali haikutokea katika kutia saini na kusababisha chama kinachounganisha wafanyakazi wa taasisi hiyo, Tuico kutangaza mgomo.
“Tunasikitika kuwataarifu wateja wetu kwamba tawi la NMB limefungwa kwa leo tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza,” ndivyo milango mingi ya matawi ya benki hiyo ilivyokuwa imeandikwa nchini kote.
Mwananchi ilishuhudia matawi mengi ya benki hiyo jijini Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro, Tarime, Dodoma, Tanga na Moshi yakiwa hayafanyi kazi huku mashine za ATM katika baadhi ya matawi zikifanya kazi hadi majira saa 6:00 kabla ya kuishiwa fedha.
Wateja wanaohudumiwa na zaidi ya matawi 120 yaliyotapakaa nchi nzima waliathiriwa na mgomo huo, wakiwemo wafanyakazi wa taasisi muhimu za serikali kama Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, walimu, wafanyakazi wa baadhi ya wizara za serikali pamoja na wafanyakazi wa halmashauri zote.
"Tumelazimika kufunga matawi yote kwa sababu karibu asilimia 90 ya wafanyakazi wote wamegoma," alisema Mwenyekiti Mtendaji wa benki hiyo, Ben Christianse, ambaye benki yake ina wafanyakazi wapatao 2,000 kote nchini.

No comments: