Tuesday, September 23, 2008

ZOMBE LEO

Watuhumiwa wakirejeshwa mahabusu jana baada ya kusikilizwa kwa kesi yao.
Wananchi wanaofuatilia kesi hiyo wakiondoka chumba cha mahakama baada ya kesi kuahirishwa.

SHAHIDI wa 33 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge na dereva teksi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa upelelezi mkoani Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe na wenzake 12, ameieleza Mahakama Kuu kuwa alipokwenda kwenye ukuta wa Shirika la Posta alikuta matundu sita badala ya manne aliyoyaona awali.
Shahidi huyo, Sajenti Nicobay Mwakajinga (40) aliieleza mahakama hiyo kuwa anafanya kazi makao makuu ya upepelezi ya jeshi la polisi akiwa mkaguzi na mchoraji ramani za matukio.
Akiongozwa na wakili wa serikali, Jasson Kaishozy, shahidi huyo alidai kuwa alitumwa kwenda kuchora ramani katika eneo la ukuta huo wa Posta ulio Barabara ya Sam Nujoma, ambako inadaiwa fedha za Kampuni ya Bidco ziliporwa na hivyo kutokea mapambano baina ya majambazi na polisi.

Alisema Februari 23, mwaka 2006 aliagizwa kwenda kuchora ramani ya eneo la tukio la Bidco na ukuta wa posta na kwamba Bageni (mshitakiwa wa pili) ndiye aliyekuwa akimpa maelekezo ya maeneo husika wakati anakwenda kuchora ramani.
Alisema walipofika kwenye ukuta huo kwa mara ya kwanza aliona matundu manne yanayodaiwa kuwa ni ya risasi na kwamba aliona damu iliyochanganyika na udongo.
“Nilichukua sampuli kidogo za damu na kuzipeleka ofisini kwa mtaalamu wa maabara ambaye alizipeleka kwa Mkemia Mkuu wa serikali kwa uchunguzi,” alisema Mwakajinga.
Shahidi huyo alidai baada ya kuchora ramani ya eneo hilo alirudi ofisini na kuikabidhi kwa bosi wake, ACP Edith Mgawe na kwamba alichora pia ramani ya eneo la Sam Nujoma kulikoporwa fedha za Bidco.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa Februari 22 mwaka 2006 alienda pia katika eneo la Sinza ‘C’ wakiwa na maafisa wengine wa makao makuu ya upelelezi na pia alichora ramani katika eneo hilo.
Alisema baada ya kutoka eneo la Sinza ‘C’ walikwenda tena katika eneo la ukuta huo wa posta na alishangaa kukuta matundu yanayodaiwa kuwa ya risasi yameongezeka na kuwa sita.
Shahidi huyo alisema ramani za matukio ya msitu wa Pande na Bunju alizichora kwa maelekezo ya shahidi wa 31, Sajini Moja Kabenga aliyekwenda huko na kwamba yeye hakwenda katika maeneo hayo.
Ramani zote za matukio ya msitu wa Pande, Bunju, Sam Nujoma, ukuta wa posta na Sinza ‘C’ zilipokelewa na mahakama jana kama kielelezo katika kesi hiyo.
Baadhi ya mahojiano baina ya shahidi huyo na mawakili Kaishozy, Maira, Magafu, Ishengoma, Myovela na Msafiri yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili Kaishozy: Wewe hasa unahusika na matukio gani?
Shahidi: Matukio ya ajali kubwa, maafa yanayotokana na majanga, na matukio ya vifo vyenye utata.
Wakili: Umefanya kazi hiyo kwa muda gani?
Shahidi: Kwa zaidi ya miaka 20.
Wakili: Utaalamu huo umeupata wapi?
Shahidi: Kwanza nina kipaji na mafunzo mengine niliyoyapata nilipokuwa chuoni wakati nachukua mafunzo ya upolisi, somo la ramani pia nilifundishwa.
Wakili: Ulipoitwa na Mgawe ofisini kwake ulimkuta na nani?
Shahidi: Nilimkuta akiwa na Zombe.
Wakili: Alikutaka ukafanye nini?
Shahidi: Alinitaka nikachore ramani ya tukio ukuta wa posta nikiongozana na Bageni.
Wakili: Bageni alikuwa wapi wakati huo?
Shahidi: Alinifuata ofisini akasema nani anaitwa Mwakajinga nikasema mimi hapa.
Wakili: Nani alikuwa kiongozi wa msafara wenu?
Shahidi: Bageni ndiye alikuwa kiongozi wa msafara wetu.
Wakili: Ulipofika huko ukuta wa posta ulifanya nini?
Shahidi: Kwanza nilikagua eneo lote na kuanza kuchora ramani.
Wakili: Bageni alikuonyesha nini eneo la posta?
Shahidi: Alinionyesha eneo ambalo majambazi yalipigwa risasi; eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako polisi walipaki gari; eneo ambalo wao walisimama; eneo ambalo majambazi yalitaka kuruka ukuta; mahali ambako majambazi yaliangukia.
Wakili: Alikuonyesha kitu gani kingine?
Shahidi: Alinionyesha matundu ya risasi kwenye ukuta wa posta na yalikuwa manne.
Wakili: Bageni alipajuaje mahali hapo?
Shahidi: Alisema aliwahi kufika hapo wakati wa tukio.
Wakili: Eneo la ukuta wa posta kuna majirani wowote?
Shahidi: Pembeni ya ukuta wa posta kuna gereji na kampuni ya kuuza maji safi.
Wakili: Ulifanya mahojiano na majirani uliowakuta pale?
Shahidi: Ndio lakini walisema wao hawafahamu chochote.
Wakili: Februari 22 mwaka 2006 kulitokea nini?
Shahidi: Nilikuwa ofisini kwangu nikaitwa na Mama Mkumbi.
Wakili: Alikueleza nini?
Shahidi: Aliniambia natakiwa kwenda kuchora ramani eneo la Sinza ‘C’.
Wakili: Mlipofika huko ilikuwaje?
Shahidi: Tuliwakuta Mama Ngonyani (shahidi wa pili) na Mjatta (shahidi wa sita).
Wakili: Baada ya hapo mlifanya nini?
Shahidi: Nilipata maelezo kutoka kwa Mjatta na kuanza kuweka alama kabla ya kuchora ramani.
Wakili Moses Maira: Ulipokwenda katika ofisi ya Mgawe ni nani alitoa maelezo ya kuchora ramani kati yake na Zombe?
Shahidi: Mgawe ndiye aliyetoa maelekezo.
Wakili Ishengoma: Je, unafahamu Bageni alifikishwa lini mahakamani?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili Majura Magafu: Je, kuna sehemu yoyote uliyohudhuria mafunzo ya uchoraji ramani ukapewa cheti.
Shahidi: Hapana.
Wakili: Kitu gani kinaweza kuthibitisha wewe ni mtaalamu wa ramani?
Shahidi: Nilipata mafunzo wakati nilipokuwa Chuo cha Polisi Moshi (CCP).
Wakili: Majibu ya damu zilizopelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali yalionyesha nini?
Shahidi: Ni damu lakini haionyeshi kama ni ya binadamu au ya mnyama.
Wakili: Ulipoona matundu ya risasi yameongezeka kutoka manne na kuwa sita hukushangaa?
Shahidi: Nilishangaa.
Wakili: Uliwahi kumuuliza Mama Mkumbi?
Shahidi: Ndio nilimuuliza na hata yeye alishangaa.
Wakili: Utakubaliana nami kwamba mlipoenda Sinza hapakuwepo na mtuhumiwa wa aina yoyote?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Kwenye tume ya rais ulihojiwa?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Longino Myovela: Iambie mahakama kuna sampuli ngapi za damu zilizopelekwa kwa mkemia?
Shahidi: Nne.
Wakili: Kwa ufahamu wako kuna ripoti ngapi za mkemia ambazo zimepelekwa polisi baada ya kupima sampuli za damu?
Shahidi: Sina idadi.
Wakili: Msafiri: Ulipoenda Sinza, Mgawe alikuambia ukachore ramani kwa ajili ya kitu gani?
Shahidi: Kwa ajili ya uchunguzi.

No comments: