Tuesday, September 09, 2008

MAFISADI

Mafisadi wazuiwa kuingia Marekani
HUKU sakata la ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na mchakato wa utoaji zabuni kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura likiwa halijatoa majibu yanayokidhi kiu ya umma, Serikali ya Marekani imetangaza kuwafungia mlango watuhumiwa wa ufisadi unaogusa maslahi yake, kuingia nchini humo kwa matembezi, kuwekeza au kutumia mali walizochota.
Nchi hiyo pia imetangaza kuwafukuza maafisa wa serikali wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ambao tayari wamewekeza nchini humo au kusafiri kwa ajili ya matumizi ya mali walizopata kinyume cha taratibu.
Marekani imekuwa ikionekana kama kiota cha mafisadi, ambao hujichotea mamilioni ya fedha kwenye serikali za nchi changa na kutowekea kwenye taifa hilo kwa lengo la kuwekeza, kutembea au kuanza maisha mapya.
Lakini jana, Balozi wa Marekani nchini, Mark Green alisema katika taarifa yake kuwa, watuhumiwa wa ufisadi, waomba na wapokea rushwa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao wanaofaidika na ufisadi huo, hawataruhusiwa kuingia nchini humo.
“Tangazo hili linawazuia watu hasa maafisa wa serikali wanaojihusisha na ufisadi wa mali ya umma kuingia Marekani na kufurahia matunda ya ufisadi wao, na huu ni ujumbe kwamba Marekani imedhamiria kuungana na nguvu za kimataifa kupambana na ufisadi kokote duniani," alisema Green.
Alisema uamuzi huo ni tangazo jipya namba PP7750 la Rais wa nchi hiyo, George W. Bush na linawahusu maafisa wa umma na viongozi wa serikali wenye tabia ya kuomba na kupokea rushwa au kutumia madaraka yao vibaya kwa faida binafsi.
"Hili ni tangazo la Rais wa Marekani na linawahusu maafisa wa umma na serikali wenye tabia ya kupokea rushwa ya fedha au mali na wanaotumia vibaya madaraka yao. Pia linawahusu maafisa wa serikali wenye tabia ya kufuja fedha za umma, kuingilia uhuru wa mahakama, uchaguzi na shughuli nyingine za umma," alisema.
Kwa mujibu wa Balozi Green, marufuku hiyo ya kuingia Marekani pia inawahusu wachumba, watoto na wategemezi wa wafanyakazi wa sekta binafsi wenye tabia ya kuwahonga watendaji wa serikali na maafisa wa umma ili wafanye mambo kwa maslahi yao badala ya umma wanaoutumikia.
Green alisema Marekani haitakubali kuwa kiota salama cha mafisadi na walarushwa na mpango huo mpya wa kuwazuia mafisadi kuingia nchini humo, umelenga kuieleza dunia kwamba Marekani iko makini katika suala hilo.
"Uwazi na vita dhidi ya ufisadi ni tunu za Marekani. Tunaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ili kung'oa mizizi ya ufisadi na kumpeleka mbele ya sheria mtu yeyote anayetuhumiwa na kubainika kushiriki matendo ya kifisadi," alisema Green katika taarifa yake.
Alisema mpango huo unawalenga watumishi walioshiriki ufisadi nchini mwao na kuathiri maslahi ya Marekani, ambayo ni pamoja na shughuli za biashara za kimataifa na uchumi za nchi hiyo.
Green alitaja maslahi mengine ya Marekani yanayopaswa kulindwa kuwa ni, malengo ya misaada yake kwa nchi husika, usalama wa nchi hiyo, ujenzi wa demokrasia na mambo yanayokiuka sheria mpya ya rushwa inayofanyika katika matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Mpango huo wa Marekani umeanza kuwa maarufu duniani, baada ya kuanza kutekelezwa na karibu nchi zote zilizoendelea (G8) kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya nchi hizo yaliyofikiwa mwaka 2003.
Katika Mkutano huo wa Juni 2003, Rais George Bush wa Marekani na viongozi wengine wa nchi hizo walikubaliana kutoruhusu nchi zao kuwa kimbilio la Mafisadi kutoka nchi zinazoendelea.
Marekani na wenzake pia wamekubaliana kushirikiana na nchi zinazoendelea kuwatambua, kuwatafuta, kufuatilia mali za mafisadi na kuzikamata kisha kuzirudisha kwa wahusika na kuwafungulia mashtaka.
Hivi karibuni viongozi hao katika mkutano mwingine uliofanyika Hokkaido, walikubaliana kuendeleza ushirikiano huo unaoongozwa na Umoja wa Nchi za Amerika (OAS) na Jukwaa la Kiuchumi la Asia Pacific Cooperation (APEC)
Uamuzi wa Marekani kuwazuia mafisadi kuingia nchini humo, umekuja wakati Tanzania ikiwa inakabiliwa na changamoto kubwa ya baadhi ya maafisa wa serikali yake kushiriki ufisadi.
Baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele kwamba maafisa wa serikali wanashiriki ufisadi ni kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu ya Tanzania (EPA), ununuzi wa rada, mkataba wa kufua umeme wa dharura wa Richmond na mikataba mibovu ya madini.
Baadhi ya tuhuma hizo za ufisadi zilisababisha Rais Jakaya Kikwete kuvunja baraza lake la mawaziri kutokana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu baada ya kuhusishwa katika kashfa ya Richmond.
Rais pia alimvua madaraka aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Marehemu Dk Daud Ballali kutokana na tuhuma za ufisadi uliofanywa kwenye akaunti ya madeni ya nje ya Benki hiyo (EPA).
Ballali alivuliwa wadhifa wake na kukutwa na umauti akiwa Marekani alikokuwa ameenda kutibiwa muda mfupi baada ya Kampuni ya Ernst&Young kumhusisha na ufisadi wa (BoT).
Mbali na kumvua madaraka Gavana Ballali, Rais pia ameagiza kufungwa kwa akaunti hiyo na maafisa wa benki hiyo waliohusika na ufisadi kuachishwa kazi, kisha makampuni yote yaliyochota fedha hizo kufilisiwa na fedha kurejeshwa Hazina.

No comments: