Tuesday, September 09, 2008

NAPE ANATISHA

Nape Achanganya Taifa
HATUA ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (CCM) kumsimamisha na kupendekeza kumfukuza uanachama,Nape Nnauye, inaelekea kupingwa vikali na vikundi vya kijamii, vikiwemo vyama vya siasa na hata ndani ya kada za vijana wa chama hicho tawala.
Aidha, mtoto huyo wa mwanasiasa wa zamani wa CCM, hayati Moses Nnauye amesema vyombo vya juu vya chama hicho vitamtendea haki katika kuamua suala hilo, ambalo alisema bado liko kwenye mkakati.
Nape alisimamishwa uanachama katika kikao cha Baraza Kuu la UVCCM kilichofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, akidaiwa kushindwa kuthibitisha tuhuma alizozitoa dhidi ya vigogo wa chama hicho kuhusu mkataba wa jengo la uwekezaji la UVCCM lililo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Nnauye alisema Baraza Kuu si kikao cha mwisho kinachoweza kumsimamisha uanachama, na kwamba yeye kama mwanachama halali wa umoja huo ana imani haki itatendeka katika vikao vya juu, ambavyo ni Kamati Kuu ya CCM, inayokutana leo, na Halmashauri Kuu itakayokutana kesho.
"Uamuzi wa baraza haunikatishi tamaa kwa kuwa vikao vya juu vya chama vinaweza kutengua maamuzi haya na nina imani na vikao hivyo na nina imani kwa chama kuwa, haki itatendeka na hatimaye kupata haki yangu," alisema Nape.
Hata hivyo, Nape alisema mpaka sasa hajapokea barua rasmi au maelezo yoyote ya kumfahamisha juu ya uamuzi huo zaidi ya kusoma kwenye vyombo vya habari tu.
Wakati Nape akisema hayo wanaharakati wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu (Sahringon) na Kituo cha Msaada wa Kisheria (LHRC), Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Mwesiga Baregu na vyama vya upinzani, Civic United Front (CUF), Tanzania Labour Party (TLP) na Chadema ni miongoni mwa makundi yaliyoishambulia hatua hiyo dhidi ya kijana Nape Nnauye.
Makundi mengine yanayopinga hatua hiyo ambayo kabla ya kufikiwa kwake ilipigiwa debe kwa nguvu na wazee wa CCM, ni makundi ya vijana hao wa UVCCM kutoka mikoa ya Morogoro na Mbeya.
Dodoma juzi wakati wa mkutano huo, makundi yalianza kujitokeza muda mfupi baada ya kumalizika Kikao cha Baraza Kuu la UVCCM, baadhi ya wajumbe wakisikika wakisema wamepoteza imani na Jumuiya hiyo kwa madai kuwa Nape ameonewa katika uamuzi huo.
Wajumbe hao walisema Nape alipaswa kupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kumpa adhabu hiyo kubwa kuliko kosa analodaiwa kulifanya ambalo pia baraza limeshindwa kulithibitisha.
Walisema juzi jioni katika Hoteli ya New Dodoma walikokuwa wamekusanyika kwenye sherehe baada ya kumalizika kikao hicho ambako baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo walionekana kusherehekea uamuzi wa kumfukuza Nape.
Walisema kitendo cha kupendekeza Nape afukuzwe uanachama na kauli kwamba adhabu hiyo haitoshi bali anapaswa kupewa adhabu kubwa zaidi ni dalili za udikteta katika jumuiya hiyo.
“Ukweli ni kuwa tunashindwa kusema kwa kuwa, wenzetu wameshika kwenye mpini na sisi tumeshika kwenye makali, lakini ukweli utabaki palepale kuwa Nape alikuwa ni chaguo la wengi na hili tunaamini kuwa litatugawa katika makundi,” alisema mjumbe mmoja.
Mjumbe huyo ambaye alikataa kutaja jina lake gazetini, alisema mpango wa kumfukuza Nape ulipangwa tangu mwanzo na kwamba hata kama wao wangesimama kumtetea, bado hotuba ya Dk Nchimbi katika ufunguzi wa kikao hicho ilionekana
kuwa alikuwa akilenga kumshughulikia.
Gazeti hili lilishuhudia kundi la watu wachache waliohudhuria chakula hicho kilichoandaliwa na aliyekuwa katibu mkuu wa UVCCM, ambaye kwa sasa ni mweka hazina wa CCM, Amos Makala, huku wengine wakigoma kushiriki sherehe hizo kwa kile walichoeleza kuwa ni kumsaliti Nape ambaye alikuwa mtetezi wa haki ndani ya UVCCM.
UVCCM Wilaya ya Morogoro Mjini imewataka viongozi wa serikali na chama hicho kuacha kuingilia uchaguzi wa jumuiya hiyo kwa kuwa, kufanya hivyo ni kutengeneza makundi ndani ya chama.
Katibu wa UVCCM Isack Kalleiya, alisema jana kuwa ni vizuri vijana wakaachwa kuamua kumchagua kiongozi wanayemtaka, badala ya uchaguzi kuongozwa na maslahi binafsi ya viongozi wakuu wa CCM.
Alisema tayari wameshapata taarifa za kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa serikali na chama kutaka kutumia uchaguzi huo, kwa nia ya kujijengea makundi yatakayoweza kuwasaidia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
“Zipo taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa serikali na chama wanataka kuingilia uchaguzi wa jumuiya, kwa maslahi yao ikiwa ni pamoja na kupandikiza makundi kwa ajili ya kuwasaidia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hali ambayo hatuwezi kuivumilia,”alisema Kalleiya.
Baadhi ya wanachama wa UVCCM Mkoa wa Mbeya wamesema wameshitushwa na kitendo cha Baraza Kuu la Umoja huo kumvua uanachama Nape Nnauye.
Wakizungumza na gazeti hili jana wanachama hao walisema wanaamini kitendo hicho kinakatisha tamaa kwa kuwa ni fitina waliyofanya watu wachache kwa faida yao.
Walisema vijana ndiyo taifa linalotegemewa katika kusukuma gurudumu la maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuongoza CCM, lakini kinachofanyika ni viongozi wa ngazi za juu kuingilia katika masuala ya vijana na kushinikiza kutolewa kwa maamuzi yenye maslahi binafsi.
Mmoja wa wanachama hao, David Halson, alisema anaamini uamuzi huo siyo wa viongozi wa UVCCM bali shinikizo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu wa CCM, ambao wamekuwa wakiingilia mambo ya utendani ndani ya jumuiya hiyo kwa ajili ya maslahi binafsi.
Alisema ni ukweli usiopingika kwamba ndani ya CCM kuna baadhi ya vigogo waanaoamini kuwa, chama hicho ni mali yao na hakuna anayeweza kuwakosoa wala kuwaondoa.
“Tukio hili linatufanya tuamini kuwa hakuna demokrasia ndani ya chama, na hakuna maana ya kuwa na Jumuiya ya vijana, ambayo ina uongozi wake lakini ina shindwa kuendesha jumuiya hiyo mpaka iweze kupata shinikizo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu,”alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wanachama wengine akiwemo, Nelson Nselemo, aliyesema kuwa hakuna asiyejua kuwa katika kinyang'anyiro hicho wamo watoto wa vingunge na kwamba, hali hiyo inaonyesha kuwa ndani ya CCM kuna tabia ya kurithishana uongozi.
Alisema kitendo hicho ni cha aibu kwa kuwa kinavuruga utendaji kazi wa UVCCM, ambao sasa nao unaoonekana kuingiliwa na watu wenye maslahi binafsi.
Wanaharakati wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu (Sahringon) na Kituo cha Msaada wa Kisheria (LHRC) wamesema uamuzi wa kumvua uanachama Nape, haukuzingatia haki na misingi ya kibinadamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Francis Kiwanga alisema kuwa, kitendo hicho hakikuzingatia misingi ya utawala bora na haki za binadamu kwa sababu adhabu hiyo imeangalia upande mmoja.
Alisema, kuna mambo mengi yanafanyika ndani ya chama, lakini adhabu zake zinakuwa ndogo na haziwezi kuleta madhara kwa wanachama wake, lakini suala la Nape kusema ukweli juu ya ufisadi ni kosa linaloweza kumvua uanachama.
Alisema: “Kitendo alichofanyiwa Nape sio cha kiungwana, ni uonevu na kinakiuka misingi ya utawala bora na sheria kwa sababu, huwezi kumwadhibu mtu kwa kusema ukweli. Kama unaona amekiuka kanuni na taratibu za chama walipaswa wampe adhabu ya kawaida kama wanavyotoa kwa wengine, hiyo ni sawa na kukomeshana.”
Alisema kumuadhibu Nape kwa kusema ukweli ni kukiuka Kauli Mbiu ya CCM inayoeleza “nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko”.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mratibu Taifa wa Sahringon, Richard Shilamba aliyesema kuwa, kamati hiyo ilipaswa ifuate misingi ya sheria na katiba kabla ya kutoa adhabu hiyo.
Alisema, viongozi wengi wamekuwa na utaratibu wa kukiuka sheria kwa kutetea maslahi yao zaidi bila ya kuangalia upande wa pili, hivyo kamati hiyo kama ilitaka kutoa adhabu ilipaswa ianze kwa watuhumiwa wa ufisadi ambao ndio chimbuko la matatizo hayo.
“Kama kamati hiyo imeamua kutoa adhabu ilipaswa iangalie chimbuko la vuguvugu hilo na chanzo chake, lakini kumuadhibu Nape peke yake ni sawa na kumuonea huku watuhumiwa wa ufisadi wanaendelea,”alisema Shilamba.
Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu amemtaka mwanasiasa mkongwe nchini na kada wa CCM Kaimu Kamanda wa Vijana wa chama hicho, Kingunge Ngombale Mwiru kuachana na siasa kwa kuwa imemshinda.
Prof Baregu alisema jana kuwa Kingunge anapaswa kuacha siasa kwa kuwa hawezi kwenda na wakati badala yake kazi hiyo sasa awaachie vijana wenye ari na moyo wa uzalendo.
Alisema inasikitisha kuona wakongwe wa chama hicho wanashawishi adhabu kwa vijana wanaojitokeza kupinga ufisadi.
“Kingunge amechoka namshauri astaafu siasa aachie vijana wenye nguvu na uchungu kwa maslahi ya taifa,ili waokoe jahazi hili linaloenda kuzama”alisema Prof Baregu.
Alisema Nape hakutendewa haki ndani ya chama chao kwani uamuzi huo unatatiza, taratibu hazikuchukuliwa kutokana na mambo mengi yanayo husika na ufisadi yanaundiwa tume na kuchunguzwa,hili alilosema Nape lingetakiwa lichunguzwe halafu ukweli ungejulikana na hatua za kisheria zingefuata.
“Hakutendewa haki ya kisiasa wala utawala bora ndani ya chama tawala hivyo nchi yetu ukiwa msema ukweli ndio wana kuchukia”alisema.
Vyama vya CUF, TLP na CHADEMA vimeelezea hatua ya Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuushawishi Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) umfukuze uanachama Mjumbe wa NEC, Nape Nnauye kama ukosefu wa demokrasia na uhuru wa kujieleza ndani ya CCM.
Viongozi wa vyama hivyo waliliambia gazeti hili jana kuwa kitendo cha makada wa CCM, Yusuf Makamba, Kingunge Ngombale Mwiru na Rashid Kawawa kushinikiza uamuzi huo kitaipeleka nchi kusikoelezeka.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilibrod Slaa alisema ameshindwa kuelewa mantiki ya CCM kumfukuza mtu anayesema ukweli badala ya kumtia moyo ili aendelea kufichua maovu.
"Kama kasema uongo mbona hatuwaoni wakijitokeza hadharani na ukweli kumpinga? Utaratibu huo ni mbovu na hauna maslahi kwa taifa," alisema Dk Slaa.
Naye Agustine Mrema alisema CCM ni chama cha mafisadi hivyo hakuna mtu anayesimama kinyume cha mafisadi akaachwa huru bila kujengewa 'zengwe'.
Alisema hashangai kuona Nape anafukuzwa uanachama kwa misimamo yake dhidi ya mafisadi kwani anajua ufisadi ndio mtaji wa CCM.
"Angewezaji kukaa na mafisadi wakati yeye si fisadi. Ninamshauri atafakari kwa kina na kuona endapo ana moyo wa mageuzi ya kweli aje upinzani tufanye kazi," alisema.
Kauli ya Mrema imeungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Juma Duni Haji aliyewataka wazee wa CCM kusoma alama za nyakati na kuacha siasa za Kivukoni kwani zitalipeleka taifa pabaya.
"Kingunge ni rafiki yangu namwomba aache siasa kama anashindwa kusoma alama za nyakati. Huu sio wakati wa siasa za Kivukoni, ni wakati wa siasa za uwazi na ukweli," alisema.

No comments: