Wednesday, September 24, 2008

MGOMO NMB

Jaji Mwipopo akisoma maamuzi yake jana mchana katika Mahakama Kuu divisheni ya kazi. Wengine walimwita Mwaipopo wakifikiri ni Mnyakyusa!
Taabu iliendelea kwa wananchi kwani hata ATM kwa siku ya jana inaonekana ziligoma, pesa hazikutoka. Wengine walisubiri siku nzima kieleweke.
Viongozi wa TUICO wakiwasiliana na wakili wao baada ya jaji kumaliza kutoa maamuzi yake.

JAJI wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Jaji Mfawidhi Ernest Mwipopo, jana alibatilisha mgomo wa wafanyakazi wa Benki ya NMB na kuwataka warejee kazini ndani ya muda wa saa tatu, uamuzi ambao umeridhiwa na wafanyakazi.
Wafanyakazi hao kutoka karibu matawi yote zaidi ya 120 nchini kote, waliamua kugoma kwa muda usiojulikana wakiishinikiza serikali kusaini makubaliano ya malipo ya mkupuo wa fedha ambazo walistahili kulipwa wakati benki hiyo ikichukuliwa na mwekezaji mpya, kutengewa asilimia tano ya hisa na pia fedha za mfuko wa kujikopesha.
Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Mwipopo alizitaka pande mbili zinazopingana kutoa matangazo kwenye vyombo vyote vya habari kuwajulisha wafanyakazi hao kuwa wanatakiwa kurejea kazini kuanzia saa 11:25 jioni jana hadi leo 2:00 asubuhi.
Katika hukumu hiyo iliyodumu kwa muda wa saa mbili kuandaliwa na kusomwa, Jaji Mwipopo alisema Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuona upungufu katika hoja tatu za wafanyakazi hao walizozitoa kutetea mgomo wao.
"Naamuru mfanyakazi ambaye hakuweza kuripoti kazini leo (jana) awe ameripoti kazini kwake kesho (leo) saa 2:00 asubuhi na naagiza uongozi wa NMB uwapokee wafanyakazi hao wote bila masharti na usiwape adhabu kwa kushiriki mgomo huo."
Saa chache baadaye, wafanyakazi waliokuwa wamekutana kwenye Ukumbi wa Msimbazi Centre, walitaarifiwa kuhusu uamuzi huo na baadaye kukubaliana kuwa wataripoti kazini leo kama ilivyoamriwa na mahakama hiyo.
Baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani na Taasisi za Benki (Tuico), Boniphace Nkakatisi kuwaeleza uamuzi huo, waliweka msimamo kuwa wasingerejea kazini na kumpa kiongozi huyo wakati mgumu wa kuwaelewesha.
"Nina waomba mrudi kazini kwa moyo mkunjufu tena kwa kujituma kama awali na kutii amri ya mahakama wakati sisi tunarudi mezani kwa majadiliano zaidi," alisema
Jaji Mwipopo alitumia muda mwingi kuwauliza maswali mawakili hao na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yao:
Jaji: Kwa nini, msomi Khamis, mahakama isiamini kuwa mgomvi wa Tuico ni serikali iliyokataa kusaini mabaliano yenu na sio NMB?
Wakili Khamis: Ndio maana nilisema kuna haja ya sisi kupata muda wa kuwasilisha nyaraka zetu kwa maandishi kwani makubaliano yalihusu pande tatu, wafanyakazi, NMB na serikali. Kabla ya serikali, NMB ilitakiwa iwe imesaini kwanza.
Jaji: Baada ya kutoa notisi ya saa 48 Ijumaa saa 10:45 jioni, kwa nini msingegoma Jumapili siku ambayo notisi yenu iliisha badala yake mkachagua Jumatatu?
Wakili Khamis: Sheria inataka watu wagome baada ya notisi, na kwa mujibu wa sheria hiyo hakuna ubaya watu kugoma muda wowote baada ya muda wa notisi hiyo kumalizika.
Jaji: Kwa nini masaa hayo 48 hayakuwa ya siku za kazi na hivyo kuishia Jumatatu na mgomo mkaanza leo (jana)?
Wakili Khamis: Siku za kazi sio za tarehe za mwezi, ni siku ambazo wafanyakazi wa taasisi wanatakiwa kufanya kazi na kwa NMB ni siku zote kwani ATM zinafanya kazi masaa 24, hivyo ni sahihi kuhesabu Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi kwa NMB.
Baada ya mahojiano na wakili wa wafanyakazi, Jaji Mwipopo alimgeukia wakili wa NMB na sehemu ya mahojiano yao ni kama ifuatavyo:
Jaji: Kwa nini nyie (NMB) msionekane pia kuwa mna hila na mnashirikiana na wafanyakazi hao kuishinikiza serikali isaini makubaliano kwa kutotoa taarifa mapema kwamba Jumatatu mgomo unaanza?
Wakili Mbwambo: Tunashukuru kwamba unatukumbusha uwezekano wa kuwasiliana na ofisi yako hata siku za mwisho wa juma, lakini katika hali ya kawaida isingeweza kuwaza kwamba tungeweza kukupata siku hiyo.
Jaji: Kwa nini mnaomba viongozi hawa wakamatwe, wafilisiwe na wafungwe kama wafungwa wa madai badala ya kuomba mahakama izuie mgomo?
Wakili Mbwambo: Hili ni ombi moja tu, kumbuka pia tumeiomba mahakama ichukue hatua nyingine yoyote inayoona inafaa kunusuru hali hiyo.
Baada ya maswali na majibu hayo yaliyodumu kwa takriban saa 1:30 Jaji Mwipopo alisema: "Kuhusu maombi ya NMB kwamba viongozi wakuu wanne wasikilizwe leo na amri itolewe ya kukamatwa, kufilisiwa na kufungwa kama wafungwa wa madai, natoa amri kwamba mahakama imewapa muda ili waweze kujitetea kwa maandishi na vielelezo na kuwasilisha pingamizi la kiapo kesho, (leo) kesho kutwa wampe nakala ya hati hiyo wakili wa mwajiri na Septemba 26 tukutane hapo saa 4:00 asubuhi kuendelea na shauri hili."

No comments: