Wednesday, September 24, 2008

ZOMBE LEO

Mtuhumiwa namba moja, Afande Abdallah Zombe akiwa full na madocument yake ya mwendo wa kesi wakati akirejea mahabusu jana.

MKURUGENZI wa zamani wa upelelezi wa makosa ya jinai, DCI, Adadi Rajabu, imedaiwa, alipewa taarifa za mpango wa mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge mkoani Morogoro na dereva mmoja wa teksi katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa mkuu wa upelelezi mkoani Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake 12.
Shahidi wa 35 katika kesi hiyo, Omar Mohamed aliieleza Mahakama Kuu jana kuwa, baada ya Zombe kuamuru wafanyabiashara hao na dereva wa teksi kuuawa, mshtakiwa wa pili, Christopher Bageni alisisitiza watu hao hawakuwa majambazi, lakini Zombe alishinikiza wauawe akieleza kuwa alishawasiliana na DCI Rajabu, ambaye hivi sasa ni balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Akisoma maelezo ya ungamo la Rashid Lema (mshtakiwa wa 11 katika kesi hiyo), shahidi wa 35 Omar Mohamed, ambaye ni Hakimu katika Mahakama ya Mwanzo ya Magomeni, alisema: “Nilijitahidi kumsihi Zombe kuwa watu hao, hawakuhusika lakini ilishindikana na aliniambia ameshampa taarifa DCI Rajabu.”
Mohamed alichukua maelezo hayo ya ungamo la mshtakiwa wa 11 wakati akiwa hakimu katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni.
Hata hivyo, hakukuwa na maelezo marefu kuhusu mkuu huyo wa zamani wa upelelezi na hata katika maswali, suala hilo halikuibuka.
Mahakama ilielezwa kuwa, Bageni alipofika katika Barabara ya Sam Nujoma alikuta lori aina ya Mercedes Benz la kampuni ya Bidco ambalo lilibeba fedha zilizoporwa na kwamba aliteremka na kwenda kumhoji dereva wa gari hilo.
“Huku akiwa anaendelea kumhoji, alipokea taarifa kwenye ‘radio call’ na baada ya kuongea kwa dakika kadhaa ilitokea gari aina ya pick-up la kituo cha polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na gari nyingine ndogo mbili,” alisema Lema.
Alisema, pick-up hiyo ilikuwa na watu wanne na kati yao wawili walikuwa wamefungwa pingu na wawili walifungwa kwa mashati.
Alisema kwenye gari ndogo alishuka Ahmed Makele (mshtakiwa wa tatu) na kwamba walikuwa wakiwasiliana na baadhi ya viongozi wa polisi kwa kutumia ‘radio call’ na simu ya kiganjani.
Lema alisema wakati akizungumza kwa simu, Bageni alienda kwa askari waliokuwa kwenye gari hilo la Chuo Kikuu na kuhoji waliokuwa wamelazwa kwenye gari hiyo ni akina nani, lakini walimjibu kuwa wamekamatwa wakiwa na silaha na pesa.
“Mimi nilimuuliza mmoja wa wale watu waliokuwa wamefungwa pingu mna matatizo gani, kijana mmoja alinijibu 'mimi afande sijui tumekosa nini,” alisema Lema.
Alisema baada ya kumaliza kuzungumza naye Bageni alikuja akiwa na dereva wa lori la Bidco na kuwaambia wafanyabiashara hao, wasimame na kukaa.
“Baada ya hapo Bageni akamuuliza yule dereva wa Bidco miongoni mwa wale wafanyabiashara na dereva teksi unaweza ukamtambua aliyekutolea bastola au aliyekuwepo katika unyang’anyi?” alisema Lema.

Alisema baada ya dereva huyo kuulizwa hivyo, aliwatazama wafanyabiashara hao na dereva teksi na alijibu kuwa miongoni mwa watu hao, hayupo mtuhumiwa.
“Sisi tulikusanyika askari 15, akaja Bageni akatuuliza hawa watu mnawaonaje, askari mmoja ambaye sikumtambua alijibu 'hawa si wahusika',” alisema Lema.
Alisema baada ya Bageni kuambiwa si wahusika alisogea pembeni akawa anazungumza na simu na baadaye aliporudi aliwaambia kuwa, RCO Zombe ametamka kuwa watu hao waende "wakachinjwe."
Mahakama ilielezwa kuwa baada ya amri hiyo, Bageni aliita gari aina ya Land Rover Defender iliyokuwa doria maeneo ya Tegeta na kuamuru wafanyabiashara hao washushwe kwenye gari la polisi la Chuo Kikuu na kuingia kwenye gari lao.
“Baada ya kuingia kwenye Defender, Bageni aliamuru msafara uelekee Mbezi Luisi msituni na tulipofika kule Bageni aliamuru Koplo Saad aanze kuwaua mmoja baada ya mwingine,” alisema Lema.
Baada ya zoezi la kuwaua kumalizika, Bageni aliamuru Lema aingie kwenye gari na kuanza kupokea miili ya marehemu hao.
“Baadaye Bageni alisogea pembeni na kuendelea kuwasiliana na aliporejea akamteua meja mmoja kutoka kituo cha polisi cha Chuo Kikuu na kumwambia aongozane na gari moja ili awapeleke marehemu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),” alidai Lema.
Lema alidai baada ya siku tatu kupita walipewa taarifa na Bageni kuwa wanahitajika makao makuu ya upelelezi polisi kwenda kutoa maelezo juu ya tukio hilo la mauaji yaliyofanyika Januari 14, mwaka 2006.
Lema alisema kabla ya kwenda Makao Makuu waliitwa na Zombe na kuwaeleza namna wanavyotakiwa kwenda kujibu.
“Tulipofika kwa Zombe alituambia kuwa 'tunajipanga namna ya kujibu hizi tuhuma na atakayeenda tofauti na sisi, tutambebesha mzigo kwmba yeye ndiye aliyeua',” alidai Lema.
Alidai baada ya hapo Zombe aliwapatia karatasi zilizokuwa zimechapwa ili wazisome na kuzirudisha kwake, lakini yeye baada ya kuisoma aliikunja na kuiweka mfukoni.
Alisema walipofika makao makuu kabla hajaandika maelezo yake, alimuuliza askari aliyekuwa akimhoji kama akiandika kitu ambacho hajakifanya hakitamletea matatizo yoyote? Na askari huyo alimjibu kuwa, viongozi wamejipanga hivyo.
“Niliandika maelezo ambayo hayakuwa ya kweli kwa sababu nilishinikizwa na viongozi wa ngazi za juu na hata yale niliyoyatoa kwenye Tume ya Jaji Kipenka hayakuwa ya kweli,” alisema Lema.
Lema alidai kwamba, pia walipowapeleka maafisa wa Tume ya Jaji Kipenka kuwaonyesha eneo walikouawa majambazi katika ukuta wa Posta, ilikuwa ni uongo.
Kabla ya maelezo hayo, hayajapokewa na mahakama, mabishano makali yalizuka baina ya upande wa utetezi na upande wa mashtaka.
Upande wa utetezi ulipinga maelezo hayo yasipokewe mahakamani kwa kuwa taratibu za kisheria hazikufuatwa wakati yanachukuliwa.
“Tunapinga maelezo haya yasipokewe kwa sababu onyo halikutolewa wakati mshtakiwa anaanza kuchukuliwa maelezo haya na pia yatakuwa hayawatendei haki washtakiwa kwani yanagusa washitakiwa wengi,” alisema wakili wa upande wa utetezi, Moses Maira.
Hoja hizo zilipingwa na wakili wa serikali, Alexander Mzikila kwa madai kuwa maelezo hayo ni halali kutolewa mahakamani na kwamba yamefuata taratibu zote za kisheria.
Jaji Kiongozi Salum Massati alitupilia mbali hoja hiyo ya upande wa utetezi.
Katika hatua nyingine, shahidi wa 34 katika kesi hiyo, Sajenti Elly Nkya, jana alimjia juu wakili wa upande wa utetezi, Jerome Nsemwa akimtaka asimharibie ndoa yake.
Shahidi huyo, alilazimika kutoa maneno hayo mahakamani baada ya Nsemwa kumweleza kuwa Zombe alikuwa akimpa lifti na kwamba pamoja na hayo bado aliweka lebo ya jina la Zombe kwenye CD ya picha alizopiga.
Nsemwa alikuwa akimhoji shahidi huyo jana kuhusiana na ushahidi alioutoa katika kesi hiyo kwa kuwa ndiye aliyepiga picha za video katika maeneo yote ya tukio hilo.
Kutokana na mahojiano hayo, Jaji Massati alilazimika kuingilia kati na kumtaka Nsemwa aendelee na maswali mengine.
Baadhi ya mahojiano baina ya wakili Nsemwa na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Nsemwa: Kazi ya kuchukua picha za video uliifanya tarehe ngapi?
Shahidi: Niliifanya Februari 22 na Machi 7 mwaka 2006.
Wakili: Kulebo jina la Zombe kwenye CD ilikuwa amri ya nani?
Shahidi: Ni utaratibu wangu wa kazi sikuambiwa na mtu mwingine.
Wakili: Machi 8, mwaka 2006 au kabla ya hapo ulikuwa unakaa wapi?
Shahidi: Nilikuwa naishi Kijichi.
Wakili: Una miliki gari?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Jirani yako alikuwa nani?
Shahidi: Zombe.
Wakili: Umehama lini Kijichi?
Shahidi: Mwaka 2005.
Wakili: Zombe alikuwa anakupa lifti?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Wakati unailebo CD, Zombe alikuwa mtuhumiwa?
Shahidi: Hapana, mheshimiwa naomba mahakama yako inilinde usiniharibie ndoa yangu wala ndoa ya Zombe mimi nina mume wangu, niliandika kwa kumbukumbu zangu.
Wakili: Toka umeanza kulebo jina la Zombe kwenye CD hadi leo ulitabiri Zombe ataletwa mahakamani?
Shahidi: Sikutabiri ila ni utaratibu wangu wa kazi.

Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi, mawakili wa watuhumiwa walimuuliza maswali shahidi huyo.
Wakili Jerome Msemwa:Shahidi, mnapoandika Confession Statement (maelezo ya ungamo)
mnaweza kumuuliza mtuhumiwa maswali?
Shahidi: Kuna maswali tunaweza kuuliza kama vile jina au kama kuna mahali
hapakueleweka vizuri.
Wakili: Katika statement ya mtuhumiwa wa 11, umeandika kuwa mshtakiwa wa kwanza
alimwagiza mshtakiwa wa pili kuwa wafanyabiashara hao wanapaswa kuuawa?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Ulimuuliza mtuhumiwa wa 11 kama kuna askari wengine katika wale 14 kati ya 15 waliokuwepo kwenye eneo la tukio? Na je, walisikia Zombe akimwagiza mshtakiwa wa pili kuwa watu wale wachinjwe?
Shahidi: Sikumuuliza.
Wakili: Kwa nini hukumuuliza? Je, hukuona umuhimu wa kumuuliza mshtakiwa wa 11?
Shahidi: Hakukuwa na umuhimu wa kumuuliza.
Wakili: Kwa nini hapakuwa na umuhimu?
Shahidi: Kwa sababu mtuhumiwa 11 alikuja kwa hiari yake mwenyewe kueleza alichokijua.
Wakili: Kwa hiyo mtuhumiwa wa 11 hakusema lolote kama askari wengine 14 nao
walisikia Zombe akimwagiza Bageni?
Shahidi: Mimi nilirekodi alichokisema mshtakiwa 11.
Wakili: Umesema Rashid (mshtakiwa wa 11) alikwambia kuwa mshtakiwa wa kwanza
alimwambia mshtakiwa wa pili kuwa watu wale wachinjwe,je, wewe uliamini hayo
maneno?
Shahidi: Sikuhitaji kuamini ama kutokuamini kwani kazi yangu ilikuwa ni kuandika tu, kile alichokuwa akikisema mshtakiwa huyo.
Wakili: Mshtakiwa wa 11 alisema aliwahi kumsikia yeye mwenyewe Zombe akiwasiliana na Bageni ambaye ni mshtakiwa wa pili?
Shahidi: Hakusema alisikia mawasiliano ya Zombe na Bageni, bali Bageni alikuwa
kiunganishi.
Wakili: Kwa hiyo ni ‘hear say’ tu (uvumi)?
Shahidi: Alisikia kwa Bageni.
Wakili: Katika ‘statement’ yake, Rashid alisema Zombe alikwepo kwenye eneo la tukio?
Shahidi: Hakumtaja.
Wakili Gaudiozi Ishengoma:Shahidi,unajua jinsi mlinzi wa amani anavyochaguliwa?
Shahidi: Ndio, nafahamu.
Wakili: Ni vipi?
Shahidi: Ukiwa hakimu wa mahakama ya mwanzo moja kwa moja unakuwa mlinzi wa amani.
Wakili: Mtuhumiwa wa 11 alipokuja kwako kutoa maelezo ya ungamo, je, ulimuuliza ni kwa nini alikuja kwako kama mlinzi wa amani?
Shahidi: Kwanza mtuhumiwa anapokuja unamuuliza kama amelazimishwa au amekuja kwa hiari yake, pia unamuuliza kama yuko tayari maelezo yake yatolewe mahakamani kama ushahidi.
Wakili: Shahidi, katika mahojiano na Msomi mwenzangu Msemwa kuna maneno mengine
uliyomuuliza mtuhumiwa lakini hukuyaandika katika ‘statement’ yako, je, ulimwambia mtuhumiwa kuhusu hilo?
Shahidi: Yapi hayo, kwani wewe ulikuwepo? Alijibu kwa kuhoji shahidi huyo na
kusababisha wasikilizaji kucheka.
Wakili Majura Magafu:Shahidi, unafahamu ni nini maana ya maelezo ya ungamo?
Shahidi: Ndio nafahamu.
Wakili: Ni nini?
Shahidi: Ni maelezo ya mtuhumiwa mbele ya mlinzi wa amani.
Wakili: Akikiri kosa, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Ni kweli.
Wakili: Kwa hiyo unapoandika maelezo ya ungamo maana yake ni kwamba mtuhumiwa anakiri kosa, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Ni kweli.
Wakili: Katika maelezo yake mtuhumiwa kuna sehemu ambako mtuhumiwa amekiri waziwazi
kuua?
Shahidi: Hakuna mahali alikosema kuwa aliua.
Wakili: Je, Rashid Lema alikuja kwako na alikuwa akituhumiwa na shtaka gani?
Shahidi: La mauaji.
Wakili: Kwa hiyo ulitarajia aje kukiri kuwa ameua, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Nilitarajia hivyo.
Wakili: Mtuhumiwa alikueleza kuwa katika eneo la tukio walikuwa askari 15, mbali na Zombe na Bageni, kuna watuhumiwa wengine aliowataja kuwepo kwenye tukio la mauaji?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Ni akina nani kwa majina?
Shahidi: Ni Saadi, Frank na Rajabu.
Wakili: Alipomtaja Saadi, alisema shughuli yake ilikuwa ni nini?
Shahidi: Alisema ndiye aliyewapiga risasi watu wale.
Wakili: Je, mbali na kuwataja Frank na Rajabu kuwa ni askari wenzake aliokuwa nao katika eneo la tukio, je, mtuhumiwa wa 11, alisema jinsi Frank na Rajabu
walivyohusika?
Shahidi: Alisema ni askari aliokuwa nao pamoja.
Baada ya maswali hayo kutoka kwa mawakili wa upande wa utetezi,washauri wa mahakama
walipewa nafasi ya kumuuliza shahidi maswali kuhusiana na ushahidi wake, lakini wote watatu hawakuwa na swali lolote la kuuliza.
Kutokana na washauri wa mahakama kutokuwa na maswali, mwendesha mashtaka wa
serikali, Alexander Mzikila alisimama tena na kumuongoza shahidi huyo kujibu baadhi
ya hoja za mawakili zilizotokana na maswali yao.
PP: Umeulizwa na msomi Magafu kuwa katika maelezo ya mshtakiwa wa 11 hakuna mahali
ambapo alikiri kosa, hebu isaidie mahakama, Rashid alikiri nini katika maelezo yake?
Shahidi: Alikiri kuwepo katika tukio na kushuhudia mauaji na kupokea miili ya
wafanyabiashara hao na kuiweka kwenye gari.
PP: Ukiwa kama mlinzi wa amani, mtuhumiwa anapoletwa kwako huja kuchukuliwa maelezo
yapi hasa?
Shahidi: Ni maelezo ya ungamo.
Baada ya kujibu hoja hizo, Jaji Kiongozi, Salum Masatti, aliahirisha kesi hiyo hadi
leo saa 3.00 kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa tena mahakamani hapo na kuwaagiza watuhumiwa kuendelea kuwa mahabusu.No comments: