Tuesday, September 30, 2008

TARIME KUMEKUCHA

Polisi anaswa akinunua kadi za Chadema



SARAKASI za 'kushikana uchawi' na 'kuzidiana kete' zimeendelea kwenye kampeni za uchaguzi wa mbunge na diwani wa Tarime baada ya askari polisi wa Kikosi cha Operesheni Maalum, kinachoongozwa na Kamanda Venance Tossi, kukamatwa akiwa katika jaribio la kununua kadi 20 za uanachama wa Chadema.

Tukio hilo lumekuja siku moja baada ya mwanafunzi wa kidato cha tatu kukamatwa kwenye ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) akisaka mteja wa kununua shahada za kupigia kura, tukio ambalo pia lilitanguliwa na vituko vingi, kurushiana maneno makali, mapambano na kupakana matope.

Lakini tukio la jana linaingia kwenye historia.

Askari aliyetambulika kwa jina la Emmanuel Zacharia, ambaye ni wa Kikosi cha Kutuliza Fujo (FFU) kutoka mkoani wa Arusha, akiwa miongoni mwa polisi 400 waliomwagwa wilayani Tarime kwa ajili ya oparesheni maalum ya kidemokrasia na kuzuia mapigano baina ya koo, alikamatwa kwenye ofisi za Chadema akijaribu kununua kadi.

Askari huyo anadaiwa kwenda kwenye ofisi hizo zilizo Mtaa wa Saronge, kitongoji cha Serengeti majira ya saa 8:00 na kutaka kuonana na maofisa wa chama hicho kwa madai kuwa anataka kununua kadi za uanachama.

Lakini ombi lake la kadi nyingi lilistua wengine na hivyo hata kabla ya kutimiza azma yake, walinzi maalum wa Chadema, maarufu kama Blue Guard, walimchunguza na kubaini kuwa ni polisi.

"Baada ya kuingia ofisini, kijana huyo alionekana kuwa na wasiwasi, kitu ambacho kilitupa mashaka pia na tukamuweka chini ya ulinzi," alisema mjumbe wa mkutano mkuu wa Chadema, Dk. Ben Kapwani.

“Tulimuweka chini ya ulinzi kwa muda na kumfanyia upekuzi na tulimkuta akiwa na vitambulisho vya benki na barua ya ofisa wa jeshi ikimtambulisha kwa mkuu yeyote wa benki kuwa huyo ni askari polisi na apatiwe msaada wa kufungua akaunti. Amedai ametoka Arusha akiwa kwenye timu ya askari wa Tossi, tumemuuliza sababu ya kuitaka kadi hajasema.”

Dk. Kapwani alisema kuwa kutokana na hali hiyo waliwapigia simu polisi na maofisa wao wengine ambao walifika wakiwa katika magari mawili ya FFU na baada ya kuzungumza na maofisa wa Chadema, polisi hao waliruhusiwa kumchukua askari huyo na kumpekeka kituoni.

“Baada ya kutoa taarifa polisi walimtuma mkuu wa FFU ambaye tunamtambua kwa jina O. M Lyampa na alipofika hapa alimtambua polisi huyo na kutueleza kuwa ni askari wao, na ndipo tulipowaruhusu kumchukua,” alieleza katibu msaidizi wa Chadema wilayani hapa, Chacha Daniel Okon'go.

Wakati askari wenzake wakimtwaa walikuwa wakimuuliza na kumhoji mwenzao kuwa ni vipi ameweza kufika katika maeneo hayo yasiyomhusu, lakini hakuwajibu.

Kamanda Tossi alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa askari wake, alijibu kwa ukali na kusema kuwa hawezi kujua masuala yote ya serikali na kufafanua kwamba serikali inao watumishi wengi wa ngazi mbalimbali na baadaye akakata simu yake ya mkononi.

No comments: