Friday, September 19, 2008

SIMULIZI ZAMUSENDO

'Jela imeathiri maisha yangu' Samahani kuna mdau amenikumbusha kuwa makala nilizoandika Mwananchi baada ya kuhojiana na Musendo zingekuwa nzuru kama zingekuwemo humu ili wengine wapate fahamu kilichomsibu. Endelea....

Ilikuwa siku, wiki mwezi na miezi na hatimaye miaka mitatu na miezi kadhaa ilikwisha, Zephania Musendo alijikuta kuwa mtu huru tena juzi baada ya kumaliza adhabu yake ya kutumikia kifungo cha miaka mitano.Aliachiwa huru kutoka Gereza la Mkuza lililo Kibaha mkoani Pwani.Musendo ni mwandishi mwandamizi ambaye amepitia vyombo mbalimbali vya habari, mara ya mwisho akiwa analiongoza Gazeti la Family Mirror akiwa mhariri mkuu.Lakini bidii yake ya kazi na ujuzi aliokuwa nao ulizimwa ghafla baada ya Hakimu wa Mahakama ya Kisutu kumhukumu kifungo cha miaka mitanojela kwa madai ya kula rushwa ya Sh 100,000 baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCB) kumshtaki.“Imeathiri sana maisha yangu, imeharibu familia yangu na nimepata hasara kwani kipato kimesimama kwa muda wote na mipango yangu imeparaganyika,” anasema Musendo katika mahojiano maalum na Gazeti la Mwananchi jana.Musendo, ambaye kwa sasa ameungana na familia yake nyumbani kwake Kawe jijini Dar es Salaam, anasema kuwa mipango yake kwa sasa ni kujiweka sawa, na kama akipata kazi atashukuru ili aweze kuisaidia tena familia yake akiwa kichwa cha familia.Lakini anapokumbuka kusimama ghafla kwa maisha yake, Musendo anaongea kwa masikitiko.Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu ilimuona Musendo kuwa ana hatia ya kupokea rushwa ya shilingi 100,000, lakini katika mazungumzo na Mwananchi, kama alivyojieleza mahakamani, Musendo anazidi kusisitiza kuwa hakupokea rushwa na kukamatwa kwake kulikuwa ni njama za kumzima asitekeleza wajibu wake."Yote haya yalinipata baada ya Family Mirror kuandika tuhuma za rushwa ndani ya PCB na kumhusisha kiongozi mwandamizi, Edward Hosea ambaye kwa kipindi hicho alikuwa Mkurugenzi wa Operesheni," anasimulia."Kulikuwa na taarifa kuwa Hosea anajihusisha na masuala ya rushwa, na aliagiza mwandishi wake ili kuweza kufuatilia hilo na kuthibitisha hata ndani ya taasisi hiyo.“Mwandishi alikwenda na hata (mkurugenzi wa PCB, Anatory)Kamazima alithibitisha kusikia tuhuma hizo. Hivyo tukawa tunazifanyia kazi.”Kwa maoni yake, Musendo anaona kuwa kutokana na habari hiyo, Hosea (sasa ni Mkurugenzi wa PCCB) aliamua kumwadhibu na kwamba, alifanikiwa kwani mahakama ilimuona kuwa ana hatia na akakaa jela kwa miaka yote mitatu."Kutumikia kifungo kwa miaka yote mitatu si mchezo," alisema."Sikuwahi kukutana na Hosea hata siku moja. Alikuwa akifanya jitihada ili niweze kuonana naye."Anasema Hosea,alimtumia mwandishi mwingine ili amfuate waweze kuonana naye.Anasema baada ya kukutana Sheraton waliongea mambo mbalimbali na Hosea alimsihi kuwa habari hiyo isitumike, (wakati huo ilikuwa bado haijaandikwa) na kudai kuwa ilikuwa ni njama za baadhi ya watu ili asipate cheo cha juu cha taasisi hiyo.“Aliniambia kuwa mambo yote hayo yalikuwa majungu, na kuwa wakati huo bosi wake alikuwa anatarajia kustaafu hivyo watu walikuwa wakitaka asipate nafasi ya ukurugenzi. Mimi nilimjibu kuwa tutatuma mwandishi ikithibitika tungeitoa,” anasema.Musendo anaeleza kuwa baada ya habari kutoka Hosea alimtafuta tena na kutaka wakutane Sheraton tena ili wazungumze na alitaka kuwa wakutane saa 10:00 jioni, naye alitimiza hilo kwa kuitikia wito.Hata hivyo, anasema kuwa ilipofika saa 11:00 aliamua kuondoka hotelini hapo kwa gari la ofisini ili arejee kazini kwake kuendelea na shughuli nyingine.“Nilipofika pale Red Cross Hosea akanipigia na kuomba radhi kuwa alikuwa amechelewa kidogo na kuwa kwa muda huo alikuwa ameshafika pale hotelini, nilimwamuru dereva turudi na nikakutana naye mlangoni.“Nilipofika ndani tukatoka na kukaa nyuma kwenye bustani, akanieleza kuwa aniagizie bia lakini mimi sikutaka kunywa bia nikaagiza soda yeye akawa anakunywa chai."Tulizungumza kwa muda na ghafla Hosea alinyanyuka na kulikuwa na watu kama sita walioingia na kuzunguka meza yetu na mmoja alimwingiza mkono mfukoni.“Wakaniambia nitulie nisifanye vurugu yoyote na kuwa walikuwa wanashuku nimepokea rushwa, wakaniamuru nitoe vitu vyote mfukoni na mimi nilitelekeza kwa kutoa kila kitu pamoja na pesa nilizokuwa nazo."Anasema baada ya kuweka mezani walikagua na kuweka pembeni baadhi ya pesa na kusema kuwa alikuwa na pesa zao kiasi cha Sh100,000 na hivyo aliamriwa kuwa yuko chini ya ulinzi.Baada ya hapo akasema kuwa walimchukua na kutoka naye nje wakidai kuwa na mahojiano zaidi.“Tulipofika nje nikawaomba nimtaarifu dereva wangu ili arudi ofisini, lakini hawakukubali na waliondoka na mimi hadi polisi Oysterbay ambako nililala huko," anasema.“Pia nilisikia kuwa hata dereva wangu alikamatwa baadaye na yeye alilala Central Police kwa kosa la uzururaji nadhani.”Anasema kwa mlolongo huo wa matukio alijua kabisa kuwa hawa watu hawakuwa na nia njema naye na mpango huo ulikuwa kumkomoa, kwani dereva hakuwa na kosa lolote."Kesho yake nilipata dhamana na wakaniambia kuwa siku inayofuata niripoti ili nifikishwe mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa."Tulipofika mahakamani nilitakiwa kuwekewa dhamana ya Sh500,000 taslim na kwa kuwa ofisini walikuwa wanashughulikia hilo, hawakusubiri na kunipeleka Keko ambako nililala kwa siku tano kabla ya dhamana kukamilishwa," anasema.Anaeleza kuwa kesi iliendeshwa kutoka mwaka 2003 na ilipofika Mei 17 2005 alihukumiwa kifungo hicho ambacho haamini kama ilikuwa halali kwa sababu alijaribu kuweka mambo yote hadharani, ikashindikana."Lakini namshukuru Mungu nimetoka," anasema.
Kesho simulizi ya Musendo juu ya matatizo mbalimbali aliyoyapata wakati akiwa kifungoni hadi anatoka jela, itaendelea.

3 comments:

Mswahilina said...

Pole sana ndugu yangu Zephania Musendo.
Yote ni Maisha.

Anonymous said...

Aise

Inasikitisha sana.Wakati nasoma hii habari nilikuwa nalengwalengwa na machozi.Aise hao kina Kosea ni washenzi sana. Wamemdhulumu Zephania kiasi hiki.Aise kwa Mungu kutakuwa na mambo kabisa.
Nampa pole sana Zephania. Mungu atamfungulia njia nyengine za kupata riziki haraka.
Naomba wanaotoa msaada wa kisheria wamsaidie aishitaki serikali kwa kumuweka ndani siku zote hizo.
Naomba uendelee kutupasha hii habari.
Asante.

Tahir
USA

Anonymous said...

hao hao wazuiaji ndio hao hao watoaji ni BALAA hamna kitu nchi hii labda tutambike