Wednesday, September 03, 2008

ZOMBE LEO

Zombe aibua ubishi msituni Abdalla Zombe akiwashauriana na wakili wake, Majura Magafu, wakati kesi ikiendelea katika ukuta wa Posta ambapo palidaiwa kuwapo majibizxano ya risasi.
Kesi ikiendeshwa katika msuitu unaodaiwa wafanyabaishara wa Mahenge waliuawa!

MABISHANO makali yalizuka jana katika Msitu wa Pande Mbezi Louis, kati ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (ACP) Abdallah Zombe na mshtakiwa wa 11 Koplo Rashidi Lema, wakati Mahakama Kuu ilipohamia katika msitu huo kuona eneo linalodaiwa kuwa wafanyabiashara wa madini wa Mahenge na dereva teksi waliodaiwa kuwa majambazi waliuawa huko.
Mabishano hayo yalitokea muda mfupi baada ya mahakama kukamilisha shughuli zake katika eneo hilo, wakati watu walipoanza kuingia katika magari yao wakiwemo washtakiwa ili kuendelea na msafara, kisha Zombe alisikika akisema kuwa hajawahi kufika katika msitu huo.
“Walahi wabilahi sijawahi kufika huku mambo haya makubwa kumbe mji huu ni mkubwa namna hii!” alisikika Zombe.
Baada ya kutoa kauli hiyo, mshtakiwa wa 11 Koplo Rashid naye alisikika akimjibu Zombe kwa hasira.
“Hilo utaeleza mahakamani na utaeleza sehemu mliyokuwa mnanywea bia siku ile na bia zilinyweka ngapi,” alisema Rashid.
Koplo Rashidi ndiye aliyeeleza kuwa majambazi yanayodaiwa kuuawa na polisi yaliuawa katika Msitu wa Pande na si eneo la Sinza C kama polisi walivyodai.
Mahakama ilianzia msafara wake katika eneo la Sinza C, ambalo linadaiwa na polisi kuwa majambazi hayo yalikamatwa eneo hilo.
Katika eneo hilo la Sinza kabla mahakama haijaondoka, Jaji Kiongozi Salum Massati aliwauliza washitakiwa kama walikuwa na lolote la kuzungumza lakini walijibu kuwa hawakuwa na lolote.
Katika eneo la ukuta wa Shirika la Posta kunakodaiwa kuwa na matundu yaliyotokana na mapambano ya polisi na majambazi, Zombe aliiomba mahakama itafute mtu ambaye atapewa bunduki na kupiga katika ukuta huo ili kubaini ukweli wa matundu hayo.
Jaji alimjibu Zombe kuwa suala hilo litazungumziwa mahakamani.
Baadhi ya mahojiano baina ya wakili wa serikali Alexander Mazikila na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edson Mmari, ambaye ni shahidi wa 30 katika kesi hiyo yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Mzikila: Je, mlipofika hapa (Sinza) waliwaeleza ni magari gani ya polisi yalikuja?
Shahidi: Walisema lilikuja gari la Bageni (mshtakiwa wa pili) na gari la Makele (Mshtakiwa wa tatu).
Wakili: Waliwaeleza baada ya kuwakamata marehemu walielekea njia ipi?
Shahidi: Walielekea njia ya upande wa magharibi.
Wakili: Wakati majambazi hayo yanakamatwa waliwaeleza wao walikuwa wapi?
Shahidi: Walikuwa eneo la Maiduka.
Wakili: Baada ya kutoka eneo la Sinza C mlielekea wapi?
Shahidi: Tulienda Sam Nujoma kwenye eneo ambalo fedha za kampuni ya Bidco ziliporwa.
Wakili: Je, fedha hizo zilikuwa zimebebwa kwenye gari gani?
Shahidi: Zilibebwa kwenye gari aina ya Mercedes Benz la Kampuni ya Bidco.
Wakili: Katika eneo hili (Sam Nujoma) kuna mabadiliko yametokea, je, kitu gani kimekufanya ulikumbuke, uliweka alama?
Shahidi: Nimelikumbuka kwa sababu upande wa pili wa barabara kulikuwa na Banda la Kampuni ya Konoike.
Wakili: Baada ya kutoka hapa mlielekea wapi?
Shahidi: Tulielekea katika eneo la ukuta wa Posta mahali ambako kunadaiwa kulikuwa na matundu ya risasi yaliyotokea baada ya majibizano ya polisi na majambazi.
Wakili: Wewe ni askari wa siku nyingi na pia ni mpelelezi unazungumziaje matundu haya?
Shahidi: Hata kama ungepiga kwa karibu na risasi ikapita kwenye mwili wa binadamu lazima ingepasua ukuta zaidi.
Wakili: Kwa kuwa Bageni aliwaeleza baada ya mapambano yale kulikuwa na majeruhi, je, nyie katika uchunguzi wenu mlibaini nini?
Shahidi: Kulikuwa hakuna majeruhi.
Wakili: Je, mliangalia kama kulikuwa na kitu kingine chochote kilichoashiria mapambano?
Shahidi: Tuliangalia ukuta wa pili lakini hatukuweza kuona kama kulikuwa na matundu ya risasi.
Wakili: Baada ya hapa mlielekea wapi?
Shahidi: Tulielekea Msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis kwenye eneo ambalo wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliuliwa kule.
Wakili: Je, mlipofika hapa (msituni) mlizikuta maiti za hao majambazi?
Shahidi: Hatukuzikuta lakini tuliambiwa walizichukua na kuzipeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakili Majura Magafu: Je, baada ya kuonyeshwa hili eneo mliweka alama yoyote?
Shahidi: Hakuna alama maalum tuliyoweka.
Wakili: Bunju mlienda lini?
Shahidi: Siku hiyo hiyo.
Wakili: Mlipofikia hapa (Bunju) mlifanikiwa kupata nini?
Shahidi: Hatukupata kitu zaidi ya kupiga picha za kawaida za video.
Wakili: Je, picha hizo zilipigwa na nani?
Shahidi: Sajent Elly alipiga picha za video na Sajent Moja alipiga picha za kawaida.
Baada ya mahakama kumaliza kutembelea maeneo husika Jaji Kiongozi Massati aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea tena.


4 comments:

John Mwaipopo said...

Yote 9 tunataka mwisho wa siku haki itendeke na ionekane kuwa imetendeka. Kuna tofauti hapo.

Anonymous said...

hapa patamu kwani sasa ndo inaanza kuonekana steringi kuuwawa tena kapewa upande wa pili wa msumeno aushike ndo kaona unakata.kidogo sheria imeanza kukata kotekote

peter maganga said...

ni huruma tukio linavyokwenda lakini inabidi haki itendeke ndipo raia waielewe serikali sababu haijawahi kufika mwisho na watuhumiwa wakubwa wengi huishia ishu kumalizwa juujuu.

Anonymous said...

Jamani ndugu zangu mimi naomba niulize swali, hivi inakuwaje hawa wahusika wanaaza kumgeuka Zombe?Jamani tamaa za mda mfupi ni noma sana,maana majuto ni mjukuu na fedha walizowarubuni zimekwishaisha na wanaoozea jela.Eee Mola niepushie haya.