Thursday, September 04, 2008

ZOMBE LEO

Shahidi adai SP Bageni alitoa amri ya kuua
SHAHIDI wa 30 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge na dereva jana aliieleza mahakama kuwa Mshitakiwa wa pili SP Christopher Bageni alikuwa akitoa amri kwa Koplo Saad Alawi, ili awauwe wafanyabiashara hao katika msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis wilayani Kinondoni.
Pia shahidi huyo ACP Emson Mmari ambaye kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora aliieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa SP Bageni ndiye aliyekuwa kiongozi wa msafara wakati wa kwenda kuwaua wafanyabiashara hao katika msitu huo.
Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Kiongozi Salum Masatti, shahidi huyo alisema baada ya kumaliza kuwaua wafanyabiashara hao,watuhumiwa waliichukua miili ya marehemu na kuipeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kutumia gari aina ya Defender kutoka katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Alisema miili hiyo ilipelekwa katika hospitali hiyo na Koplo James kutoka Kituo cha Polisi Chuo Kikuu ambaye hivi sasa hajulikani aliko baada ya kutoroka.
Mmari alidai kuwa alipata maelezo hayo kutoka kwa mtuhumiwa wa 11 Koplo Rashidi Lema wakati akifanya upelelezi wa tukio la mauaji hayo.
Alisema mtuhumiwa wa 11 aliwaeleza kuwa yeye hakuhusika kuwaua wafanyabiashara hao bali alikuwa akitazama wakati Koplo Saadi akiwaua wafanyabiashara hao kwa kuwapiga risasi mmoja baada ya mwingine.
Mahojiano kati ya shahidi Mmari na Mawakili yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Majura Magafu: Shahidi, hebu ieleze mahakama hii, mlipopewa jukumu la kufanya uchunguzi ni watuhumiwa wangapi mlitakiwa kuwapeleleza?
Shahidi Mmari: Watu 15.
Magafu: Katika hao 15, je mtuhumiwa wa kwanza (Zombe) alikuwemo?
Mmari: Hakuwemo.
Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa upelelezi wenu haukumuhusisha Zombe?
Mmari: Hatukuwa na maelekezo ya kumchunguza.
Magafu: Kwa hiyo utakubaliana na mimi kuwa hakuna ushahidi wa kujitegemea wa kuwepo kwa mawasiliano kati ya Zombe na Bageni?
Mmari: Tulipata maelezo kutoka kwa mshitakiwa wa 11
Magafu: Huyu mshitakiwa wa 11 alikuambia nini katika mazungumzo ya Bageni na Zombe?
Mmari: Maneno hatukuyasikia.
Magafu: Je, utakubaliana na mimi kuwa mazungumzo hayo, hayahusishi tukio hilo lililotuweka hapa mahakamani?
Mmari: Hilo sijui.
Magafu: Mshitakiwa wa 11 alipokuja kwenu kutoa maelezo, mlimhoji nini na ni kitu gani kilimsukuma kuja kwenu?
Mmari: Alisema ni kutokana na nafsi yake tu kwa sababu yeye hakuhusika katika tukio la kuua.
Magafu: Utakubaliana na mimi kuwa wewe binafsi hujui akina nani waliokwenda kwenye eneo la tukio?
Mmari: Ni hawa walioko hapa?
Magafu: Unathibitishaje kwamba watuhumiwa hawa hapa ndio waliokwenda kwenye eneo la mauaji?
Mmari: Kimazingira.
Magafu: Kwa hiyo utakubaliana na mimi kuwa wewe kama wewe na timu yako ya uchunguzi ukiachilia mbali maelezo ya mtuhumiwa wa 11 hakuna ushahidi wa kujitegemea kuthibitisha kuwa watuhumiwa hao, walikwenda katika msitu wa Pande?
Mmari: Nimesema kutokana na maelezo ya mtuhumiwa wa 11, 12 na 13.
Magafu: Wewe ulimhoji mtuhumiwa wa 13?
Mmari: Mwenzangu ndio alimhoji.
Magafu: Uliwahi kusoma maelezo yake?
Mmari: Ndio.
Magafu: Kwenye maelezo yake ameeleza kuwa walikwenda katika msitu wa Pande?
Mmari: Ndio.
Magafu: Alikwambia walikwenda kufanya nini?
Mmari: Si kuwashughulikia hao marehemu?, alijibu Mmari na kuwafanya wasilikilizaji kucheka.
Wakili Denis Msafiri: Huyu mtuhumiwa wa 11 alikwambia yeye alikuwa akifanya nini wakati walipokweda katika msitu huo wa Pande?
Mmari: Rashid alisema alikuwa akiangalia tu wakati Koplo Saadi akiwafyatulia risasi marehemu.
Msafiri: Aliyepeleka Maiti Muhimbili ni nani?
Mmari: Ni Sajini James wa Kituo cha Chuo Kikuu.
Msafiri: Mlifahamu alitumia gari gani?
Mmari: Alitumia gari aina ya ‘Defender’ ya Kituo cha Oysterbay.
Huku Mmari akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Alexander Mzikila kujibu baadhi ya hoja za mawakili hao, shahidi huyo alisema waliamini maelezo ya mshitakiwa wa 11 kwa sababu aliwapeleka katika maeneo yote yaliyohusiana na mauaji hayo na kwamba waliweza kupata vithibitisho kama vile maganda ya risasi na damu iliyokuwa imeganda katika udongo.

Mmari alidai kutokana na ushahidi wa maelezo walioupata eneo la Sinza C kutoka kwa shahidi Benadetha Limbu ambaye ni shahidi namba 2 katika kesi hiyo na Mjatta Kayamba, marehemu walikamatwa na askari wakiwa wazima na kuondoka nao na kwamba anaamini kuwa watuhumiwa hao, ndio waliowaua wafanyabiashara hao.
“Kama waliwakamata na kuondoka nao wakiwa hai waliwezaje kufariki wakati wakiwa chini ya ulinzi?” alihoji Mmari wakati akiongozwa na Mwendesha Mashitaka, Mzikila kujibu baadhi ya hoja za mawakili wa utetezi.
Pia Mmari alipoulizwa na mshauri wa mahakama hiyo, Nicolaus ni kuwa kama hawakuwa majambazi ni kwa nini watuhumiwa hao, waliwaua wafanyabiashara hao, shahidi huyo, alisema hajui na kwamba watuhumiwa hao, wanajua wenyewe.
Kesi hiyo, inaendelea tena leo, saa 3:00 asubuhi katika mahakama hiyo.

3 comments:

irine said...

Kaka Hongera nakukubali kweli kutuletea kesi ya zombe direct kwani inatusaidia sana kwa sasa tusioenda huko.

Anonymous said...

hey Irine ..hurusiwi ku-comment!

utashitaki!


heri mimi sija---comment!

Anonymous said...

thanx a lot bro!big up