Thursday, February 19, 2009

DR KITINE ALONGA


MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Makete na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), katika serikali ya awamu ya tatu, Dk Hassy Kitine ameonya kwamba, uchafu na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa, mustakabali mbaya wa kisiasa na hali ngumu ya uchumi vinavyoikabili nchi, vinahatarisha usalama wa taifa.
Kauli ya Dk Kitine ambaye alishika wadhifa huo wa Ukurugenzi katikaIdara ya Usalama wa Taifa kwa takribani miaka 30, wakati serikali ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na awamu ya Pili ya Ali Ahssan Mwinyi, imetolewa wakati nchi ikiwa imegubikwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya ufisadi na vita ya chini kwa chini ya kugombea madaraka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk Kitine alionya kwamba, uchumi na maliasili za taifa zimeshikwa na wageni, huku Watanzania walio wengi wakifanya kazi za udereva, ufagiaji barabarani, kazi za ndani na mashambani.
"Nimewaiteni kuzungumzia mustakabali wa nchi yetu, kama mnavyofahamu mimi nimeshika nafasi mbalimbali nyeti kuanzia wakati wa Mwalimu," alifahamisha.
Akifafanua na wakati mwingine akionyesha msisitizo kwa kugonga meza, Dk Kitine ambaye ni mchumi na aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alisema, Watanzania wazawa wenye utajiri halali hawafiki hata watano.
Alisema kama wapo Watanzania wengine wenye fedha nyingi ni ambao wamezipata katika njia chafu ndiyo maana wamekuwa wakizificha ng'ambo.
Alisema katika kipindi cha mwisho wa serikali ya Mkapa, nchi ilivurugika kiasi kwamba, hadi sasa haijulikani pa kuanzia ili kuweza kuisafisha kwani imeoza kutokana na kukosa misingi imara ya uongozi iliyoachwa na Mwalimu Nyerere.
Alionya akisema: “Haiwezi kuongozwa kienyeji".
"Hata hao akina Mramba (Basil), ambao wamekamatwa ni sawa na tone la maji katika bahari. Nchi hii imeoza, wapo wakubwa wanakula rushwa, lakini nani kafungwa?" alihoji.
Akionekana ni mwenye uchungu na uzalendo wa hali ya juu na nchi hii, alisema kuporomoka kwa fikra za utaifa, maadili ya viongozi wa umma, misingi imara ya uongozi kwa ujumla, kumeifikisha nchi katika kiwango cha rushwa kubwa ya kutisha.
Dk Kitine ambaye dhahiri alionekana kuchoshwa na mwenendo wa baadhi ya mambo yanayotendeka nchini, alisema watu wanazungumzia rushwa ndogo wakati wakubwa serikalini wanakula rushwa kubwa zinazoyumbisha uchumi wa nchi na kuleta ufakara kwa Watanzania.
Alionyesha kushangazwa na kutokamatwa kwa baadhi ya watu ambao wanafahamika dhahiri kwamba, wameiba fedha kwa kutumia makampuni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT).
Kwa msisitizo, alisema kuna baadhi ya viongozi serikalini, wakiwemo mawaziri wanapewa kiasi kidogo cha fedha kama Sh 20 milioni na kuachia zabuni au maliasili za nchi ambazo wabakaji uchumi hujipatia kiasi cha fedha kama Sh4 bilioni.
"Watu hawa wabakaji wa uchumi, mara nyingi huwa karibu na viongozi wetu, unaweza kukuta waziri anapewa Sh20 milioni, anafurahi lakini mbakaji uchumi huyo anatengeneza Sh4 bilioni, na kuacha Watanzania hoi," alibainisha.
Alisema maadili yameporomoka kuanzia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutoa mfano kwamba, waziri anajiuzulu wadhifa wake kwa tuhuma kama hizo, lakini bado anabaki kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na mbunge.
"Wakati wa Mwalimu, mtu wa namna hii anapoteza uanachama kwa sababu ameshindwa kulinda kiapo chake na kukiaibisha chama," alisema na kuongeza:
Alisema huu ni wakati ambapo Idara ya Usalama wa Taifa inapaswa kuwa nguzo na mhimili imara wa kuhakikisha viongozi wanaopatikana serikalini wakiwemo mawaziri, wanakuwa waadilifu ili kulinda masilahi ya taifa.

2 comments:

Anonymous said...

Hancy Kitine, huyu mzee alifanya makosa yake zamani. Lakini ni Mtanzania bora... Mzee wa sumo hii ni Good article.. Moja kati ya wazee watakao kuwa kwenye Kipindi changu cha Kutana na Muandishi (meet the Journalist) kitakacho anza soon 2010.

Mdau wa usa

Anonymous said...

Dk Kitine kama sikosei aliachia uwaziri kwa kashifa ya kumpeleka mkewe ulaya kutibiwa kwa gharama za walipa kodi na ni mamilioni ya shilingi yalitumika sasa hapa sijui anaongea nini?? maana hata yeye hakuwa clean plus ametemwa ana wayawaya this is typical Hypocritic politics.