Thursday, February 19, 2009

KESI YA ZOMBE

Shahidi akiri kuwaona wafanyabiashara
wakiwa hai

KESI ya mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge, mkoani Morogoro inayowakabili waliokuwa maafisa na askari wa jeshi la polisi, jana iliendelea kuvuta hisia za watu baada ya mtuhumiwa wa kumi, Abeneth Saro, ambaye alikuwa askari katika Kituo cha Polisi Urafiki, kuieleza Mahakama Kuu kuwa alifika katika eneo la tukio na kuwaona wafanyabiashara hao wakiwa hai.
Akitoa ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo, Saro alidai kuwa, alifika katika eneo hilo akiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, ASP Ahmed Makelle pamoja na PW Jane Andrew.
Alidai kuwa, Makelle na Jane walishuka kwenye gari na kwenda mahali ambapo askari wa Urafiki walikuwa wamesimama wakiwahoji wafanyabiashara hao na yeye alibaki kwenye gari.
Aliongeza kuwa, baada ya Makelle na Jane kurudi kwenye gari, Makelle alichukua radio kwake akatoa taarifa za tukio hilo chumba cha kutoa taarifa control room na kwamba, baada ya hapo Makelle aliwapeleka (wao) hadi Kituo cha Polisi Ubungo Terminal ambako aliwaacha ili wakaendelee na kazi yeye (Makelle) akaondoka.
Hata hivyo, licha ya Saro kukubali kutoa maelezo katika timu ya polisi na kwenye Tume ya Kipenka, aliyakana kuwa siyo yake.
Akiongozwa na Wakili wake Majura Magafu, alidai kuwa maelezo hayo binafsi yanaweza kupatikana katika faili lake la ajira ambalo liko makao makuu ya polisi.
Alijitetea kuwa yeye hahusiki na mauaji hayo kwa kuwa hajawahi kumuua mtu na akaiomba mahakama imtendee haki.
Hata hivyo, kabla ya Saro kupanda kizimbani mshtakiwa wa tisa katika kesi hiyo, PC Michael Sonza, alijitetea kuwa kuwepo kwake kwenye sherehe ya kupongezwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe, ndicho kilichomfanya ashtakiwe.
PC Sonza alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la Mshauri wa Mahakama, Magreth Mosi, kutokana na maelezo ya ushahidi wake wa utetezi aliyotoa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Salum Masatti.
Juzi Sonza ambaye ni miongoni mwa askari wa kituo cha Polisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema, hakuhusika na mauaji ila kilichompoza ni kuwa miongoni mwa watu waliopongezwa na Zombe baada ya tukio hilo.
Mosi alimuuliza kama haoni kuwa kitendo cha kukubali kupongezwa kwa sababu ambazo hakuzijua ndiko kulikomfanya asimamishwe kizimbani alisema: “Mtakatifu Jaji hili ndilo lililoniponza.”
Kabla ya kuulizwa na Mosi, alihojiwa na Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo kama ifiatavyo:
Mwipopo: Umeieleza mahakama kuwa miongoni mwa majukumu yako ni doria, je, katika kituo chenu mna maeneo mangapi mnayofanyia doria?
Sonza: Tunayo kama matano.
Mwipopo: Ni yapi hayo?
Sonza: Ni Changanyikeni, Makongo Juu, Survey, Mlalakuwa na maeneo ya Barabara ya Sam Nujoma kuelekea Mwenge.
Mwipopo: Tarehe 14/1/2006 uliambiwa utafanyia wapi doria?
Sonza: Hatukuwa tumeambiwa ni wapi tutafanya doria.
Mwipopo: Kwenye gari ulilolitaja kuwa ndilo mliloondoka nalo kituoni kwenda kwenye doria, mlipanda askari wangapi siku hiyo?
Sonza: Niliokwisha kuwataja, mimi, James, Mabula, Nyangelela, Festu na Noel ambaye ndiye alikuwa dereva.
Mwipopo: Mlipewa silaha gani?
Sonza: SMG
Mwipopo: Hakuna aliyepewa bastola?
Sonza: Hilo sikujua.
Mwipopo: Kulikuwa na aliyekuwa na redio call?
Sonza: Ndio alikuwa ni Koplo Felix.
Mwipopo: Kule Changanyikeni mlimwacha nani?
Sonza: Hatukumwacha mtu.
Mwipopo: Lakini Makongo Juu waliwaacha wewe na Mabula ni sahihi?
Sonza: Ni sahihi Mtukufu Jaji.
Mwipopo: Walipowashusha waliwaambia wao wanakwenda wapi?
Sonza: Hawakutuambia.
Mwipopo: Mlipokwenda kupongezwa kwa RPC aliwaambia anawapongeza kwa kazi gani?
Sonza: Kwamba kwa kukamata majambazi.
Mwipopo: Hukuona umuhimu wa kusema wewe hukuwepo, hivyo na wewe uliridhika tu na pongezi kwa kazi ambayo hukuifanya?
Sonza: Kwa kuwa ni kiongozi wa juu nisingeweza kumuuliza.
Mwipopo: Ulimweleza OCS ili naye ajue kuwa pongezi ulizopewa hukustahili?
Sonza: OCS pia ni ngazi ya juu kumueleza.
Mwipopo: Ni nani basi uliyemweleza kuwa wewe hukuwa miongoni mwa waliokamata hao majambazi?
Sonza: Nilimweleza Sajenti Nico wa makao makuu ya polisi upelelezi.
Mwipopo: Ni lini ulimweleza?
Sonza: Sikumbuki tarehe.
Mwipopo: Je, ni mwishoni mwa mwezi Januari ulipokwenda kuhojiwa?.. maana jana ulisema uliitwa kuhojiwa mwishoni mwa mwezi huo.
Sonza: Ndio.
Mwipopo: Wewe uliona ni kawaida kupongezwa kwa kazi ambayo hujaifanya na ukakaa kimya?
Sonza: Kwa kuwa kilikuwa ni kituo changu cha kazi, hivyo nilijua tumepongezwa kwa ujumla.
Mwipopo: Umewahi kuandika maelezo kuhusiana na tukio hili mara ngapi?
Sonza: Mara mbili.
Mwipopo: Kwa Sajenti Nico CID Headquarters na Central (Makao Makuu ya Polisi na Kituo Kikuu).
Wakili: Sajenti Nico alikueleza sababu za kukuhoji?
Sonza: Ndio alisema ni kuhusu tukio la Sinza.
Mwipopo: Sajenti Nico alikueleza kuwa yuko kwenye timu au chombo chochote kinachochunguza tukio hilo?
Sonza: Hakunieleza.
Mwipopo: Hapa kuna kielelezo cha maelezo kilichotolewa mahakamani, hebu kiangalie na kisha uieleze mahakama ni nani aliyetoa maelezo hayo.

Sonza: Inaonekana ni D8289. PC Michael.
Mwipopo: Ambalo ndilo jina na namba yako?
Sonza: Ndio.
Hata hivyo, aliyakana maelezo hayo kuwa siyo yale aliyoyaandika.
Maelezo hayo yanasema siku ya tukio mshtakiwa huyo pamoja na aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo ambaye tayari ameachiwa, Koplo Morris Nyangelela, walikuwa kwenye doria Survey na maeneo ya Barabara ya Sam Nujoma.
Kielelezo hicho kinaendelea kusomeka kuwa wakiendelea na doria walisikia taarifa za tukio la ujambazi eneo la Barabara ya Sam Nujoma kupitia kwenye redio call wakaelekea huko na mara wakaona gari la doria la Kituo cha Oysterbay, walilifuata na mara wakasikia risasi zikilia akainama na kwamba, baada ya kutulia aliinuka na kuona watu wanne wakiwa wamelala chini wamejeruhiwa ambapo walichukuliwa hadi Barabara ya Sam Nujoma na kutambuliwa na wamiliki wa Kampuni ya Bidco walioporwa fedha zao.
Majeruhi wale na dereva wa gari la Chuo Kikuu aliulizwa kama kulikuwa na mafuta ya kutosha, akasema hayatoshi ndipo majeruhi wakahamishiwa kwenye gari la Oysterbay na kupelekwa Hospitali ya Muhimbili.
Mwipopo: Unasemaje kuhusu maelezo hayo?
Sonza: Mtukufu Jaji si ya kwangu haya.
Hata hivyo, Sonza alikubali baadhi ya maelezo binafsi kama vile jina la kituo cha polisi alichoanzia kazi, kuwa doria siku ya tukio, kupewa bunduki na risasi 30 kuwa ni sahihi lakini akakana kuwa hakuzaliwa Mbozi, bali alizaliwa Kyela na kwamba hakuhamia Kituo cha Chuo Kikuu mwaka 2001.

Mwipopo: ACP Mgasa ulikuwa unamfahamu?
Sonza: Hapana sikuwa namfahamu.
Mwipopo: Alikuwa na sababu yoyote ya kukusingizia?
Sonza: Hapana.
Mwipopo: Ulitoa maelezo kwenye Tume ya Jaji Kipenka?
Sonza: Ndio.
Mwipopo: Maelezo hayo uliyatoa chini ya kiapo?
Uliyoyaeleza kwenye tume hiyo ni sawa na uliyoyaeleza hapa mahakamani?
Sonza: Ndio.
Mwipopo: Mimi nasema uliyotoa huko ni tofauti na uliyoyaongea hapa.
Mwipopo: Ulitoa maelezo yako kwenye timu ya Mama Mkumbi Central?
Sonza: Ndio.
Mwipopo: Nani alikuhoji?
Sonza: Sikumbuki maana walikuwepo maafisa watatu.
Mwipopo: Angalia haya maelezo, unayatambua kuwa ni yako au si ya kwako?
Sonza: Mtukufu Jaji haya si ya kwangu.
Mwipopo: Hebu ieleze mahakama ni lipi hukulisema siku ile.
Sonza: Nilichokisema ni kile nilichokieleza hapa.
Mwipopo: Kingine ni kipi?
Sonza: Aliyeandika maelezo yangu siye huyu, yule alikuwa Inspekta lakini hapa inaonekana ni Sajenti kwa hiyo siye.
Mwipopo: Mama Mkumbi ulikuwa na kisa naye?
Sonza: Hapana.
Baada ya maswali hayo kutoka kwa Wakili Mwipopo, Wakili wa mshtakiwa, Majura Magafu alimwongoza kujibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na Mwipopo.
Magafu: Shahidi ulipopanda gari ya Chuo Kikuu kwenda kwa RPC mliambiwa kuwa mnakwenda kufanya nini?
Sonza: Hatukuambiwa.
Magafu: Baada ya kupewa mkono wa pongezi askari wa Chuo Kikuu mlipewa nafasi ya kuongea?
Sonza: Mtukufu Jaji, hatukupewa nafasi
hiyo.
Magafu: Nani aliandika maelezo yako ulipohojiwa CID makao makuu?
Sonza: Ni Inspekta Nico.
Magafu: Huyu Inspekta Salum anayeonekana katika kielelezo D.6 kuwa ndiye aliyeandika maelezo yako unamfahamu?
Sonza: Mtukufu Jaji simfahamu.
Magafu: Umesema aliyeandika maelezo yako Central alikuwa na cheo gani?
Sonza: Inspekta.
Magafu: Huyo anayeonekana katika kielelezo hiki ana cheo gani?
Sonza: Sajenti.
Kisha washauri wa mahakama pia hususan Magreth Mosi walimhoji mshtakiwa kama yafuatavyo.
Mosi: Shahidi mlipoingia ofisini kwa RPC kupongezwa hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuwa ni kwa nini mnapongezwa?
Sonza: Hayakuwepo maelezo Mtukufu Jaji.
Mosi: Huoni kuwa kukubali kupongezwa kwa sababu ambazo hukuzijua ndiko kumekusababisha kuwa kizimbani leo?
Sonza: Mtukufu Jaji huko ndiko kulikoniponza.
Katika kesi hiyo Zombe na wenzake wanatuhumiwa kuwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge, mkoani Morogoro.
Washtakiwa katika kesi hiyo walioko mahakamani sasa kwa mpangilio ni Abdallah Zombe, SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, WP 4593 PC Jane Andrew, CPL Emmanuel Mabula, D8289 PC Michael Sonza, D 2300CPL Ebeneth Saro, D.9312D/C Rashid Lema, D4656 C/CPL Rajab Bakari na D.1367 D/CPL Festus Gwabisabi.
Kesi inaendelea leo

No comments: