Friday, February 20, 2009

UBADHILIFU BOTBaada ya kuachiwa kwa Dhamana, Mahakama yaamuru Liyumba akamatwe!
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeagiza Mkurugenzi wa zamani wa Utawala na Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba aliyeachiwa kwa dhamana siku tatu zilizopita akamatwe pamoja na wadhamini
Wadhamini wake ambao ni wafanyakazi wa BoT Benjamin Nduguru (mhasibu wa benki hiyo) na Agaterus Oto (afisa usalama wa ndani wa benki hiyo) walikamatwa jana na kuachiwa muda mfupi baadaye, lakini Liyumba hakupatikana.
Wadhamini hao walikamatwa majira ya saa 6 mchana na kuwekwa mahabusu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi walipoachiwa saa 10:47 jioni.
Kabla ya wadhamini hao kuachiwa waliingizwa mahakamani saa 10:30 jioni mbele ya Hakimu Mkazi Hadija Msongo.
Liyumba pamoja Meneja Miradi wa benki hiyo, Deogratias Kweka, wanakabiliwa na kesi ya ubadhirifu katika ujenzi wa majengo pacha ya BoT uliyoisababishia serikali hasara ya Sh221 bilioni.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Tabu Mzee alisema kuwa, walipokea hati kwa ajili ya kumkamata Liyumba na wadhamini wake lakini hawajafanikiwa kumpata Liyumba.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Msongo aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa 8 mchana kwa kuwa jalada halisi la kesi hiyo limeitwa mahakama kuu na kuwataka wadhamini hao wafike muda huo.
Akizungumza nje ya mahakama, Mzee alisema tangu jana hati ilipotolewa wamekuwa wanafanya jitihada za kumtafuta Liyumba bila mafanikio na kwamba, bado wanaendelea kumtafuta.
Hatua ya kukamatwa kwa Liyumba na wadhamini wake imekuja siku mbili baada ya Liyumba kuachiwa kwa dhamana ya Sh 882 milioni ambayo ni thamani ya nyumba yake iliyoko Mbezi Juu.
Wakati akitoa uamuzi wa dhamana ya Liyumba, Hakimu Msongo alisema mshitakiwa huyo atakuwa nje kwa dhamana ya Sh 882 milioni wakati mahakama ikijiridhisha na hati nyingine zilizopingwa na upande wa mashitaka.
Alisema mshitakiwa atatakiwa kutimiza masharti ya dhamana ya kiasi kilichobaki cha Sh 54,417,344,800.23 endapo mahakama itaona kuwa hati hizo zina kasoro.
Mawakili wa Liyumba waliwasilisha hati 11 lakini upande wa mashitaka ulizikataa hati kumi na kuikubali moja ambayo ni namba 2233 kitalu H, Mbezi yenye thamani ya Sh 882 million inayomilikiwa na Liyumba mwenyewe.
Uamuzi huo uliushangaza upande wa mashitaka ambapo mwendesha mashitaka wa serikali, Justus Mulokozi, alipinga uamuzi huo wa mshitakiwa kupewa dhamana kwa hati ambayo haikutimiza kiwango cha fedha kilichopangwa na mahakama.
Liyumba na Kweka walipandishwa kizimbani Januari 27, mwaka huu kwa tuhuma za kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh 221 bilioni. Kweka bado yuko rumande baada ya kukosa dhamana.

No comments: