Friday, February 20, 2009

KIBAKA MSALABANI

Jamaa hoi baada ya kutolewas misumali aliyokuwa amewambwa nayo.

Wahudumu wakiokoa maisha ya kibaka huyo!
Kibaka aking'olewa misumali katika hospitali ya Mwananyamala

MKAZI wa Manzese Uzuri, jijini Dar es Salaam, amenusurika kufa baada ya kupigiliwa na misumari kwenye msalaba na wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira, kwa tuhuma za kuiba baiskeli.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea leo maeneo ya Manzese Uzuri baada ya kijana huyo kukutwa na baiskeli iliyodaiwa kuwa ya wizi.

Wakazi wa eneo hilo walimkamata na kisha kutengeneza msalaba na kumtundika juu kwa kumpigilia misumari ya nchi sita kisha kumwacha hapo.

Baadaye wasamaria wema waliopita katika eneo hilo walimwona wakautoa ubao mmoja na kisha kijana huyo akaenda kujisalimisha katika kituo cha polisi akiwa na ubao wa mikononi ambako alipigiliwa mishumari. Polisi wa kituo hicho wakamkimbiza katika Hospitali ya Mwananyamala akiwa kwenye msalaba huo kwa ajili matibabu.

“Sijawahi kuiona katika maisha yangu, wananchi kweli wamekuwa wanyama,” alisema mfanyakazi mmoja wa hospitali hiyo mara baada ya kumpokea mtu huyo aliyeletwa na polisi hospitalini hapo mapema asubuhi jana.

Akisimulia mkasa huo baada ya kumhudumia kwa kumtoa misumari iliyokuwa imepigiliwa mikononi na mabegani; mtumishi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema: “Baadhi misumari iliingia katika mifupa ya mikono na kumuumiza vibaya.”

“Ameumia sana na kuna mifupa ambayo imevunjika baada ya kutobolewa na misumari hiyo mikubwa, lakini ana bahati hajafa,” alisema mtumishi huyo.

Imeelezwa kuwa kijana huyo mara baada ya kukutwa na baiskeli hiyo, wananchi walimkamata na kumsulubu kwa kutengeneza msalaba na baadaye kumpigilia kwenye msalaba na kumwacha akiwa ananing’inia.

Baadaye walipita wasamaria wema walioamua kumsaidia kwa kuondoa ubao mkubwa uliokatisha mgongoni na hivyo yeye kujisalimisha polisi huku ubao uliopigiliwa mikono ukiwa bado mwilini mwake.

Polisi walimchukua na kumpeleka hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na hakufunguliwa mashtaka yoyote kwani hakukuwa na mtu aliyelalamika kuibiwa.

Baada ya kufikishwa hospitalini hapo kijana huyo alikuwa kivutio kwa wagonjwa na ndugu waliowatembelea pamoja na baadhi ya watumishi waliokuwa hapo.

Wengine kwa kushangazwa ama kuvutiwa na kitendo hicho waliamua kupiga picha kwa kutumia simu zao ambazo zilimwonyesha kijana huyo akiwa katika maumivu makali.

Baada ya hapo wahudumu wa hospitali hiyo walimchukua na kumtoa misumari hiyo na kumpatia matibabu.

2 comments:

Anonymous said...

Bongo tambarare, Lakini wawafanyie hivyo mafisadi mbona itakuwa mswano.

Anonymous said...

tumeshafika njia panda ya peponi na motoni, bado masaa machache kila mtu atashuka na mzigo wake mwenyewe, hakubebei mtu.