Thursday, February 12, 2009

MIZENGO ANENA


Pinda ajutia Uwaziri Mkuu, aona mzigo


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema machozi aliyotoa bungeni hivi karibuni, hayakuwa kwa ajili ya kulilia uwaziri mkuu kama baadhi ya watu wanavyodhani, kwani cheo hicho kwake ni mzigo mzito.

Pinda alisema hayo katika mahojiano na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1) yaliyorushwa jana asubuhi, kupitia kipindi cha Jambo Tanzania.

Alifahamisha kuwa hajui jinsi machozi hayo yalivyotoka na kusisitiza kuwa wanaofikiri alikuwa analilia uwaziri mkuu, hawamjui vizuri, kwani hakuwa anajijenga kisiasa na wala hana nia hiyo.

“Sikuwa najijenga kisiasa na wala kuulilia uwaziri mkuu, kwani cheo hicho ni mzigo mkubwa na wanaofikiria nilikuwa naulilia hawakunielewa na hawanijui vizuri,” alisisitiza Pinda.

Alisema tangu ashike wadhifa huo amegundua kuwa muda mwingi ni wa kazi, kwani wakati mwingine huwa anachelewa kulala.

Aliongeza kuwa wadhifa huo umemfanya asionekane kwa wapiga kura wake ambao walikuwa wamemzoea na kukaa naye karibu, lakini hivi sasa wanamuogopa kwa kwa sababu ni waziri mkuu.

Wiki mbili zilizopita, Pinda alilia bungeni alipokuwa akijibu swali la msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed kuhusiana na kauli yake aliyotoa kwenye ziara yake Kanda ya Ziwa kuwa wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nao wauawe.

No comments: