Thursday, February 12, 2009

SANGOMA KUKIONA MZA
Waganga waanza kufanyiziwa kuokoa maalbino
AGIZO la Waziri Mkuu alilotoa wakati wa ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa kuhusiana na ukomeshaji wa mauaji ya albino, limeanza kutekelezwa baada ya vibanda 17 vya nyasi mali ya waganga wa jadi kubomolewa wilayani Ilemela jijini Mwanza.
Zoezi hilo la ubomoaji ambalo limefanyika kwa mgambo wa jiji la Mwanza katika zoezi lililosimamiwa na viongozi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza chini ya mkurugenzi wake Willson Kabwe.
Vibanda vya nyasi vilivyobomolewa ni 13 pamoja na nyumba nne za nyasi ambazo ni mali ya mganga Masai Kasanga aliyekuwa amejenga jirani na shule ya sekondari ya Lumala iliyopo wilayani Ilemela jijini Mwanza. Akielezea zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Willson Kabwe, alisema mamlaka yake imeamua kutekeleza agizo hilo la serikali ambalo lilitolewa na maelekezo yaliyotolea na mkuu wa mkoa wa Mwanza Dk. James Msekela katika hotuba yake wakati wa kupokea maandamano ya maalbino jijini Mwanza.
“Zoezi la leo ni utekelezaji wa agizo la serikali, na hili litakuwa ni zoezi la kudumu kwa vile ujengaji wa vibanda hivi unapingana na sheria ya mipango miji ambayo inazuia kuwepo kwa vibanda katika maeneo ya taasisi ama makazi ya watu. Litakuwa endelevu na leo tumeanzia hapa Ilemela”Alisema Kabwe.
Alisema kabala ya kumvunjia mganga huyu alipewa taarifa ya kuhama na kubomoa vibanda vyake ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia ya ardhi ya eneo hilo sh. 1.2 milioni ambalo alikuwa akilimiliki kihalali lakini licha ya kupokea fidia hiyo aligoma kuhama hatua ambayo imelifanya jiji kuchukua hatua hiyo.
Akielezea hatua hiyo mganga huyo Masai Kasanga ambaye ni mwenyeji wa Bukumbi wilayani Misungwi alisema hakuweza kuhama licha ya kutakiwa kufanya hivyo na kulipwa fidia kutokana na ukweli kuwa fidia hiyo ni ndogo na kwamba uongozi wa jiji haukumpa fidia ya kuhamisha mali zake pamoja na wagonjwa wake.
“Nilipokea fidia lakini niliwaeleza kuwa wanapaswa kunipatia na fedha ya kuhamisha wagonjwa wangu pamoja na vitu vyangu hawakunipa ndiyo maana sikuhama, lakini sasa wamefanya hivi, basi” alieleza.

No comments: