Saturday, February 14, 2009

TUNAKWENDA WAPI?

Wananchi washusha kipigo kwa polisi

KUNDI la wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira, jana waliwavamia na kuwajeruhi kwa mawe na fimbo baadhi ya askari polisi baada ya mmoja wao kumgonga mwanamke kwa pikipiki katika eneo la Soko Kuu la mjini Tabora.
Wananchi hao pia nusura wachome pikipiki hiyo katika tukio la aina yake kwenye eneo hilo lenye watu wengi.
Tukio hilo lilitokea baada ya polisi aliyekuwa akiendesha pikipiki yenye nambari za usajili PT 1314, Koplo Laurent kumgonga mwanamke aliyefahamika kwa jina la Zena Idd, 22, katika Barabara ya Madaraka na wakati akijaribu kutoa msaada kwa majeruhi, alishtukia akivamiwa na kundi la watu walioona tukio hilo.
Wakati askari huyo aliyekuwa na bunduki aina ya SMG kifuani akizongwa na wananchi hao, alichomoa simu na kuwasiliana na wenzake ili wawahi kuja kumsaidia, lakini akapokonywa simu na mwananchi mmoja aliyehisi kuwa alikuwa akiomba msaada wa polisi wengine.
Mara baada ya majeruhi Zena aliyepata mchubuko usoni na kuumia bega la mkono wa kulia kupelekwa hospitali, askari wa usalama barabarani wakiongozwa na mkaguzi msaidizi wa polisi, Haruna Kasubi walifika eneo la tukio kutaka kupima ili wabaini chanzo cha ajali ndipo vurugu za wananchi dhidi ya askari zikaanza na kutaka kuchoma moto pikipiki iliyopata ajali.
Vurugu hizo zilizodumu kwa muda mfupi zikiambatana na askari polisi kufyatua risasi hewani mfululizo huku wananchi wakiendelea kuwarushia mawe, zilisababisha kujeruhiwa kwa mkaguzi huyo wa polisi pamoja na PC Kennedy na askari mwingine aliyefahamika kwa jina la Masatu kabla ya askari hao kulazimika kukimbia.

No comments: