Saturday, February 14, 2009

UWAJIBIKAJI

JK amvua cheo DC Bukoba

RAIS Jakaya Kikwete amemvua madaraka na kumwachisha kazi rasmi kuanzia jana, mkuu wa wilaya ya Bukoba, Albert Mnali aliyeamuru polisi mmoja kuwachapa viboko walimu katika shule tatu za msingi zilizoko wilayani kwake kutokana na kushika mkia katika matokeo ya darasa la saba.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana ilieleza kuwa, Rais Kikwete amechukua hatua hiyo ili iwe fundisho kwa kuwa kitendo alichokifanya mkuu huyo wa wilaya hakikubaliki, kimedhalilisha, cha kuvunja moyo walimu na kinavunja maadili ya kibinadamu.

Katika uamuzi huo, Rais Kikwete alisema mkuu huyo wa wilaya amedhalilisha wadhifa wa ukuu wa wilaya kwa kuwa alikosea kuchukua hatua hiyo kwa kuwa mwenye mamlaka ya kuwawajibisha walimu ni kamati za nidhamu za mikoa na wilaya na wala si mtu mmoja kama alivyofanya mkuu huyo.

Alisema kuwa amechukua hatua hiyo baada ya kufuatilia maelezo ya pande zote zinazohusika na kuwa serikali imeridhia kiongozi huyo avuliwe wadhifa.

Kabla ya rais kumtimua, Mnali amesema "litakalokuwa na liwe", kama uamuzi wake wa kuchapa viboko walimu utagharimu cheo chake.

Mnali alimwamuru koplo aliyekuwa ameongozana naye kuwacharaza viboko walimu 31 wa shule tatu za msingi za Katerero, Kansenene na Kanazi, akidai kuwa aligundua kuwepo kwa uzembe mkubwa kazini, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kazini na kutofundisha ipasavyo kama mikataba yao inavyowataka.

Lakini mkuu huyo wa wilaya hakuonekana kujutia wala kubadilisha msimamo wake wakati alipozungumza na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba katika kikao chao cha kawaida cha kujadili maendeleo ya halmashauri.

"Walimu ndio wameshachapwa viboko kwa hiyo litakalokuwa na liwe," alisema wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ambayo shule hizo tatu ziko chini yake.

"Hata kama nitang'oka madarakani kwa sababu hiyo, lazima nikabidhi suala hili kwa katibu tawala wa wilaya (DAS) na katibu tawala wa mkoa (RAS), ili kama kuna uwezekano wa kuwahamisha walimu kuwapeleka wilaya nyingine kama Ngara na walio katika wilaya hiyo kuletwa wilaya ya Bukoba."

Hata hivyo, mbali na maelezo hayo, madiwani wa halmashauri hiyo hawakuchangia lolote kuhusu njia aliyotumia DC huyo ya 'kuongeza ufanisi' kwa kuchapa viboko walimu katika tukio lililotokea Februari 11 mwaka huu kwenye ofisi za shule hizo tatu.

No comments: