Wednesday, February 25, 2009

UFISADI BOT


Liyumba akielekea katika karandinga kwajili ya kwenda kupata malazi Keko baada ya mapumziko ya siku kadhaa!

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilibatilisha dhamana ya mkurugenzi wa zamani wa utawala na utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba baada ya kuridhika kuwa mtuhumiwa huyo si mwaminifu kutokana na kuwasilisha hati ya kusafiria aliyojua kuwa iliisha muda wake.
Mbali na kubatilisha dhamana hiyo, mahakama pia imezikataa hati zote 10 zilizowasilishwa na mtuhumiwa huyo baada ya kubaini kuwa haziendani na utashi wa masharti ya dhamana na kuamuru zikabidhiwe polisi kwa uchunguzi zaidi.
Liyumba, ambaye aliripotiwa kuwa ametoweka, jana alifika tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuendelea na kesi inayomkabili ya tuhuma za kutumia vibaya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh221 bilioni kutokana na kupitisha maamuzi ya mradi mkubwa na kuutekeleza bila ya ridhaa ya bodi ya wakurugenzi.
Habari za kutoweka kwa Liyumba ziliibuka baada ya upande wa mashtaka kuomba hati ya kumkamata na kulalamika kuwa haukuweza kumpata baada ya Kiyumba kupewa dhamana katika mazingira ya utatanishi baada ya hati zake nyingi kuonekana zina kasoro, lakini akaruhusiwa kurudi uraiani kwa hati ya mali ya Sh882 milioni kati ya Sh55 bilioni zinazotakiwa kwa dhamana.
Mara baada ya Liyumba kupandishwa kizimbani saa 5.17 mbele ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo, wakili wa serikali, Justus Mulokozi, aliitaarifu mahakama kuwa, jana ilikuwa siku ya kutaja kesi hiyo na kwamba baada ya kutolewa hati, mshtakiwa alikamatwa.
Lakini, wakili wa upande wa utetezi, Majura Magafu alipinga kauli hiyo, akisema kuwa mteja wake alifika mwenyewe mahakamani na si kwamba alikamatwa kama alivyoagizwa na mahakama wakati ikiiahirisha kesi hiyo wiki iliyopita.
Kuhusu kwisha muda kwa hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo, Hakimu Msongo alisema mahakama iliwasiliana na Idara ya Uhamiaji na kuthibitishiwa kuwa, mshtakiwa anamiliki hati nyingine ya kusafiria iliyotolewa Juni 10 mwaka 2005 na kwamba muda wake wa kuisha ni Juni 2015 tofauti na hati iliyowasilishwa awali mahakamani hapo ambayo muda wake uliisha Desemba 12 mwaka 2007.
“Mahakama imeona mshtakiwa alitoa taarifa za uongo huku akifahamu kuwa anamiliki hati nyingine ndio maana tulitoa hati ya kumkamata,” alisema Hakimu Msongo.
Lakini Wakili Magafu alitetea kwa kudai kuwa, mtuhumiwa aliwasilisha hati hiyo iliyoisha muda wake kwa bahati mbaya na kwamba hakuwa na lengo la kuihadaa mahakama.
“Tunaomba radhi kwa niaba ya mteja wetu... hilo lilitokea kwa bahati mbaya. Tunaomba hati aliyokuja nayo leo ipokelewe na dhamana yake iendelee,” alisema Magafu.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na wakili wa serikali, Prosper Mwangamila ambaye alidai kuwa Februari 17, upande wa mashtaka ulipinga mahakama kupokea hati hiyo iliyoisha muda na kwamba mahakama ilimuuliza mshtakiwa kama ana hati nyingine, lakini alikana kuwa hakuwa na hati nyingine.
Kutokana na hali hiyo, Wakili Rwebangira aliiomba mahakama kumfutia dhamana mshtakiwa huyo hadi atakapotimiza masharti ya dhamana kwa madai kuwa si mwaminifu.
Baada ya hoja hizo, Hakimu Msongo aliahirisha kesi hiyo saa 6:25 hadi saa 8:00 mchana alipotoa uamuzi juu ya dhamana ya mtuhumiwa huyo. Hakimu Msongo alisema, mahakama imeamua kumfutia dhamana mshtakiwa baada ya kugundua mapungufu katika baadhi ya hati zake.
Hakimu Msongo alisema baada ya kupokea taarifa za Uhamiaji, mahakama iligundua kuwa mshtakiwa alikuwa na hati nyingine yenye namba AB 019418 iliyotolewa Juni 10 mwaka 2005 ambayo inaonyesha muda wake wa kuisha ni Juni 2015.
Hakimu Msongo pia alitupilia mbali hoja za Wakili Magafu kwamba, mteja wake aliwasilisha mahakamani hapo hati ya awali kwa bahati mbaya, akisema hazina msingi kwa kuwa mshtakiwa aliulizwa kama anamiliki hati nyingine na akakana.
Akizungumzia hati 10 zilizokuwa zinahakikiwa na mahakama, Hakimu Msongo alisema, hati hizo zina mapungufu mengi kwani zina majengo yanayofanana; zina mali zinazoharibika na zinazohamishika ambazo alisema hazihusiani na masharti ya dhamana.
“Kwa hiyo hati zote 10 zimekataliwa na mahakama; na ninatoa amri zikabidhiwe polisi kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi... mshtakiwa arudishwe mahabusu,” alisema Msongo.
Awali, wakili mwingine wa upande wa utetezi, Hubert Nyange aliiomba mahakama kesi hiyo ipewe kipaumbele kwa madai kuwa, mshtakiwa wa pili, Deograthias Kweka anaweza kukaa ndani kwa muda mrefu kwani hana uwezo wa kutoa Sh55 bilioni.
“Mheshimiwa tunaomba tupewe mwenendo wa upelelezi kwani siku ambayo Kweka alichukuliwa hakufanyiwa upelelezi wowote, bali alikwenda kukabidhi ofisi,” alisema Nyange.
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Msongo alisema mahakama si sehemu ya upelelezi, ushahidi wala utetezi na kwamba iko kwa ajili ya utoaji na utekelezaji wa haki na si kuingilia upelelezi.
Hakimu Msongo aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 10 mwaka huu itakapotajwa.
Liyumba aliondoka mahakamani hapo majira ya saa 9 mchana akiwa amepanda kwenye basi la Magereza huku akiwa ameshika bomba kwa kukosa siti.
Tofauti na siku nyingine, jana Mahakama ya Kisutu ilifurika umati mkubwa wa watu na wakati wa kupelekwa gerezani Liyumba alikuwa akishangiliwa na mahabusu wengine waliokuwa wakipiga kelele wakisema, "karibu, karibu,"
Jana, Liyumba alitinga mahakamani saa 2.47 asubuhi akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 526 AVB akiwa ameongozana na wakili wake.
Baada ya mtuhumiwa huyo na wakili wake kushuka na kwenda moja kwa moja ofisi ya waendesha mashtaka wa mahakama, Liyumba alijikuta akiswekwa katika chumba cha mahabusu cha mahakama hiyo kwa zaidi ya saa mbili tofauti na watuhumiwa wengine ambao huwa na dhamana.

No comments: