Thursday, February 12, 2009

ZOMBE AZIDI KUJITETEA


Zombe alina na DPP, asema alimfanyizia

MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe ameieleza Mahakama Kuu kuwa kilichomfanya amwage machozi kizimbani jana, ni mchezo mchafu aliofanyiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP).

Juzi Zombe alitokwa machozi mara kadhaa wakati akijitetea mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Masatti kuhusiana na tuhuma za mauji zinazomkabili pamoja na askari wenzake tisa.

Hata hivyo, alipoulizwa na wazee wa baraza kwamba, akiwa RCO alijua ni nani aliyetoa amri ya kuwashambualia marehemu hao waliodaiwa kuwa majambazi, alidai kuwa ni mshtakiwa wa pili SP Christopher Bageni.

Akijibu maswali kutoka kwa waendesha mashtaka(PP) jana kuhusiana na ushahidi wake wa utetezi alioutoa mahakamani hapo juzi, Zombe aliiambia mahakama kuwa maelezo yaliyoandikwa na baadhi ya washtakiwa wakiwa mahabusu, ambayo yalitumia kama ushahidi wa kumuunganisha katika kesi hiyo, yaliandaliwa na DPP mwenyewe na kuwapa washtakiwa hao.

Alidai kuwa barua za maelezo ya washtakiwa hao zote ambazo nakala zake alizitoa juzi mahakamani hapo kama vielelezo kwa ajili ya ushahidi wake yaliandikwa Juni 3, 2006 mchana ingawa baadhi hazina tarehe.

Zombe alidai kuwa barua hizo zote zilitolewa gerezani hapo kupitia kwenye nguo za mmoja wa washtakiwa na kumfikia DPP Juni 5 saa 3 asubuhi.

“Mheshimiwa jaji jana nililia hapa mahakamani kwa sababu ya mchezo huu mchafu niliofanyiwa na DPP. Barua hizi ziliandikwa tarehe 3 mwezi wa 6 mchana na zikafika ofisini kwa DPP tarehe 5 saa 3 asubuhi. Tarehe sita mwezi huo huo DPP anaandika barua ya kuniunganisha mimi katika kesi hii akidai amekamilisha ushahidi kwa kutegemea maelezo haya,” alidai Zombe.

Alidai kuwa aliweza kupata nakala za barua hizo baada ya raia mwema mmoja kuipelekea familia yake na kuwaambia kuwa, hicho ndicho kinachomfanya awe gerezani.

Pia Zombe bila kuwataja, alidai kuna baadhi ya washtakiwa ambao hawakuandika barua hizo walimweleza kilichofanyika dhidi yake na kwamba, kulikuwa na mawasiliano baina ya baadhi ya washtakiwa na DPP kwa njia ya simu.

Aliieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao walikamatwa na simu hizo baada ya mkuu wa gereza kufanya upekuzi na kwamba, mkuu huyo wa gereza amezihifadhi ataziwasilisha mahakamani hapo siku ya kutoa ushahidi wake.

“Mheshimiwa Jaji hata siku nilipokamatwa, waliponiona walishangilia sana wakisema, ‘Zombe huyo Zombe huyo’, kwa kuwa walikuwa wakijua kilichokuwa kinaendelea dhidi yangu.

Hata hivyo Wakili wa Serikali, Alexander Mzikila alidai kuwa nakala za barua alizozitoa mahakamani hapo zote si za kweli, kwa kuwa barua halisi alizo nazo ambazo pia alimuonyesha Zombe zimeandikwa tarehe tofauti na nakala za Zombe na kwamba, hata tarehe ya kufika kwa DPP ni tofauti na tarehe aliyoitaja Zombe.

Sehemu ya mahojino kati Wakili Mzikila na Zombe yalikuwa kama ifuatavyo.

Mzikila: Mshtakiwa, kama sijakosea wewe ni kachero mzoefu uliyebobea kama ulivyojieleza, Barua ya DPP kwenda kwa DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai), na zile za washtakiwa kutoka gerezani kuna mahali ambapo ilikuwa addressed (ilielekezwa) kwako?

Zombe: Hapana, hakuna mahali ilipoelekezwa kwangu. Lakini hizi za washtakiwa nililetewa na raia kunijulisha kuwa hizo ndizo zinaniweka gerezani. Barua hizi hazikupitia kwa mkuu wa gereza na aliiletea familia yangu kwa kunihurumia. Huu ni mchezo mchafu wa DPP.

Mzikila: Utakubaliana nami kuwa barua hizo ulizipata isivyo halali?

Zombe: Zilikuwa kwa maslahi yangu, kwani zilihusu dhuluma ya DPP. Hapaswi kutumia nafasi yake kuonea bali kulinda haki.

Mzikila: Ni halali si halali kwako?

Zombe: Ni halali, maana moja nilipewa na IGP.

Mzikila: Umesema barua hizo si halali kwa kuwa hazikupitia kwa mkuu wa gereza. Kwa mfano barua ya Emmanuel, kama alikuwa mahakamani akaamua kuandika na kumpa askari aifikishe kwa DPP, unasemaje?

Zombe: Ni makosa kwani hata tukiwa mahakamani bado tuko chini ya ulinzi.

Mzikila: Ikipitia kwa askari itamfanya DPP asiifanyie kazi?

Zombe: DPP hana mamlaka wala hakuna sheria kuwasiliana na wafungwa wakiwa gerezani. Ni haramu na ni ukiukwaji wa sheria za magereza namba 10.

Mzikila: Tarehe ulizozitaja kuandikwa na kufika kwa DPP katika nakala zako ni tofauti na zilizo kwenye barua origino (halisi), unasemaje kuhusu tofauti hizo?

Zombe: Ni haramu kwani hazikupita kwa mkuu wa gereza na zinadanganya kwa sababu zote ziliandikwa tarehe 3 mchana na kufika kwa DPP tarehe 5 asubuhi. Na DPP ana mamlaka gani kuzungumza na wafungwa bila idhini ya mkuu wa gereza, kwani siku nyingine anaweza kuwatorosha wafungwa.

Mzikila: Zaidi ya haya unayoyazungumza hapa kuwa barua hizi zimeandikwa tarehe 3 na kupokelewa kwa DPP tarehe 5 je, una ushahidi mwingine wowote?

Zombe: Ushahidi wangu mwingine ni kuwa barua hizi haziwezi kuandikwa na washtakiwa maneno yanayofanana maelezo na mtiririko. Naona ni mtu aliwafundisha ili apate alichotaka na ndiyo maana niko hapa.

Mzikila: Uliwafundisha wewe?

Zombe: Aliwafundisha DPP.

Mzikila: Ulimsikia au uliona akiwafundisha?

Zombe: Kuna simu tano zitaletwa hapa ambazo zilikamatwa kwa washtakiwa. Nashangaa walikuwa wakichaji wapi gerezani na nani aliwapa dola.

Wakili Kaishozi: Ukiwa kama RCO ni msaidizi wa DPP je, uliwahi kutilia mashaka maamuzi ya DPP?

Zombe: Yako mengi sana. Mfano kesi ya wafanyakazi wa Bima waliachiwa na mahakama, lakini DPP akaamua wafunguliwe mashtaka tena, lakini akamtoa mkwewe aliyekuwemo.

Kaishozi: Wewe unajua ushahidi mwingine uliopatikana nje kama alikuwa hahusiki?

Zombe: Kuna kesi nyingi tu.

Ingawa Zombe alimtuhumu DPP kwa kumfanyia alichodia kuwa mchezo mchafu na kwamba, pengine ni rushwa kutoka kwa magazeti aliyoyafungulia mashtaka ya kashfa.

Hata hivyo, alipohojiwa na Wakili Kaishozi alikiri kuwa wakati washtakiwa hao wakiandika maelezo hayo alikuwa bado hajafungua kesi dhidi ya magazeti hayo.

Mbali na kumtuhumu DPP, Zombe pia alidai kuwa maelezo aliyoyatoa mshtakiwa wa 11 Koplo Rashid Lema kumhusisha na kesi hiyo ni kwa sababu ya kutokuwa na uhusiano mzuri baina yao na akadai kuwa Lema aliwahi kuvunja kantini ya Kituo cha Oysterbay na kuiba mamilioni ya pesa na alipofikishwa kwake (Zombe) aliagiza ashtakiwe kijeshi.

Zombe aliunga mkono maelezo ya shahidi wa 36 upande wa mashtaka ambaye alisema hata kama hawakuhusika walipaswa kutoa taarifa kwa wakubwa wao baada ya tukio hilo.

Zombe alisema katika kanuni za Jeshi la Polisi unapaswa kutii amri ya rais tu na amri halali ya afisa wa jeshi hilo na kwamba, ikiwa tukio likitokea askari mdogo akalishuhudia na mkubwa wake akatoa taarifa yenye mashaka, basi anawajibka (askari huyo) kutoa taarifa kwa wakubwa wake.

Alipoulizwa na wazee wa baraza kwamba, akiwa RCO alijua ni nani aliyetoa amri ya kuwashambulia marehemu hao waliodaiwa kuwa majambazi, alisema mshtakiwa wa pili SP Christopher Bageni.

Na kuhusu kuwajibika kwa tukio hilo kati ya askari waliofika alisema anaiachia mahakama ndiyo itakayoamua.

Katika hatua nyingine, Zombe jana alionekana kuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi mbalimbali wa shule za sekondari, ikiwemo Kisota ya Kigamboni ambao walifika mahakamani hapo kumuona na kisha kumshangilia wakati akiondoka kwenye basi la mahabusu.

Wanafunzi hao walikuwa wakimshangilia na kumpungia mkono huku wakimtakia heri na kwamba Mungu atamsaidia.
1 comment:

Anonymous said...

hao wanafunzi wanamshangilia muuaji????