Saturday, March 07, 2009

KAULU YA DR IDRISS

SHIRIKA la Umeme (Tanesco) jana lilitanga kufuta mpango wake wa kununua mitambo ya mitumba ya kuzalisha umeme wa dharura ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited, likisema lisibebeshwe lawama kwa yatakayotokea.
"... na wananchi wa Tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakapokuwa imegubikwa na kiza, mahospitali hayatoi huduma; viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu tulishindwa kufanya maamuzi," alisema mkurugenzi wa Tanesco, Dk. Idrissa Rashid katika mkutano aliouitisha na waandishi wa habari jana.
Uamuzi huo umekuja siku mbili baada ya spika wa Bunge, Samuel Sitta kueleza kuwa msimamo wa kamati ya Nishati na Madini iliyoshauri mitambo hiyo isinunuliwe ndio msimamo wa chombo hicho cha kutunga sheria na hivyo kumaliza mvutano uliokuwepo kati ya kamati hiyo na ile ya hesabu za mashirika ya umma, inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Serikali na Tanesco zilikuwa zinataka mitambo hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme inunuliwe kwa ajili ya kulinusuru taifa na tatizo linalobashiriwa la upungufu wa umeme, ambao Tanesco inadai mahitaji yake yanaongezeka kwa kasi, wakati uzalishaji ni mdogo.
Katika mkutano wake na waandishi jana, Dk. Rashid alisema kuwa mwelekeo wa suala hilo unaonekana kulipeleka shirika lake kwenye ugomvi wa wanasiasa, jukwaa ambalo alisema hawana mamlaka nalo.
"Ni maoni yetu kwamba tumewasilisha suala hili kwenye ngazi zote kwa ukweli thabiti ambao umezingatia hali halisi ya sasa na inayotarajiwa," alisema gavana huyo wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
"Tunaamini kuna hali inayozuia kuwa na mjadala wa uwazi na ukweli kuhusu masuala haya yenye msingi wa utaalamu. Masuala ya taaluma na ufundi, yanamezwa na hoja za kisiasa. Hali hii haina maslahi yoyote kwa mazingira haya tunayokabiliana nayo wala kwa shirika la Tanesco."
Mkurugenzi huyo alisoma uamuzi huo wa Tanesco wa kurasa tano na baada ya kumaliza alisimama na kuanza kuondoka, akikataa kujibu maswali juu ya taarifa hiyo, ambayo awali ilikuwa isomwe juzi, lakini Tanesco ikaahirisha mkutano huo na waandishi bila ya kueleza sababu za uamuzi huo.
Kuhusu suala hilo kugubikwa na hoja za kisiasa, Dk. Rashid alitoa mfano wa kauli za kiongozi mmoja ambaye alisema alinukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema kuwa jitihada hizo ni za "kuwasafisha mafisadi, ni kukiuka taratibu na sheria za nchi".
“... na mwingine alisema akipatiwa fedha, anaweza akapata mitambo mipya ya uwezo huu ndani ya wiki chache tu. Hizi ni kauli zinazopotosha ukweli wala hazizingatii utaalamu bali zimejaa utashi wa kisiasa zaidi na zinachangia kuwavunja mamia ya wafanyakazi wa Tanesco ambao wanafanya kazi kubwa usiku na mchana kuhakikisha nkuwa nchi inapata umeme wa uhakika,” alisema Dk. Rashid.
"Sisi si wanasiasa, wala hatufanyi kazi zetu kwa kuweka mizani au kuangalia upepo wa kisiasa. Ni jambo la huzuni kwamba miongoni mwa wanaotoa hoja za kupotosha umma, wengine amepata nafasi ya kukaa nasi na kubadilishana nasi mawazo juu ya hali ya umeme.

No comments: