Thursday, February 25, 2010

CCJ

BAADA ya kusota kwa miezi miwili sasa, hatimaye Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ametoa barua kwa Chama cha Jamii (CCJ), inayoonyesha kuwa chama hicho kitapata usajili wa muda Machi 2, mwaka huu.
Uamuzi huo wa ofisi ya msajili unaondoa wingu la muda mrefu lililokuwa limetanda kuhusu kucheleweshwa kupewa usajili huo.
Jana mchana Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alitoa barua ya utambulisho kwa uongozi wa CCJ inayoeleza siku ya kupewa usajili wa muda.
Katibu Mkuu wa CCJ Renatus Muabhi, alifahamisha kwamba, msajili aliwapa barua hiyo jana mchana hatua ambayo imeufurahisha uongozi wa chama hicho baada ya kuhaha kwa muda mrefu.
"Uamuzi huo umetufurahisha sana, msajili ametupatia barua ya utambulisho mchana huu, tulisubiri kwa muda mrefu sana zaidi karibu miezi miwili sasa," alisema Muabhi na kuongeza:
"Ndiyo ilikuwa ndoto yetu, sasa tunaamini Watanzania watapata nafasi ya kuweza kupata fursa ya kufanya maamuzi sahihi kwa kukimbilia na kujiunga na CCJ ili kuunganisha nguvu.
"CCJ haitawaangusha Watanzania kwani ni chama ambacho sera, shabaha na madhumuni yake ni kuwakomboa na kuwapa nguvu za kiuchumi, kumiliki rasilimali zao na mambo yote ya msingi."
CCJ iliwasilisha maombi kwenye ofisi ya Msajili wa Vyama tangu Januari 20, hatua ambayo imekuwa ikiiumiza kichwa CCM hadi kufikia kutoa tamko la kutahadharisha wanachama wake wasije kuingia mkenge kwenda kwenye chama hicho.
Hata hivyo, kauli hizo za kuhaha za CCM hazikuwa zikitosha kutimiza kile wanachokidhamiria katika kuzima moto wa CCJ kwani Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, John Chilligati ambaye alisema kamwe chama hicho hakitaweza kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Lakini, Muabhi alisema CCJ ni chama makini na kinachoundwa na watu makini, hivyo kuzuia usajili wake ni kunyima fursa Watanzania haki yao ya msingi ya kujumuika.
"Tuliamini msajili angesajili CCJ, tulishaweka siku ya mwisho ambayo ni Alhamisi hii kuona kama kutakuwa na chochote kuhusu kupata usajili wetu wa muda, lakini sasa tumethibitishiwa," alifafanua Muabhi.
Alisema kila kitu walichokuwa wameelekezwa na msajili walishatimiza ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho yote ya msingi na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika.
"Kwa hiyo msajili ametupa barua hiyo ya utambulisho akisema kuwa tumekidhi mahitaji ya msingi tuliyoelekezwa, hivyo sisi tunafurahia hatua hii,"aliongeza.
CCJ ujio wake unaangaliwa na wadadisi wa mambo ya kisiasa kama tishio kwa CCM na Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutajwa kuhusisha vigogo wa chama hicho tawala ambao wanataka kujitenga na kugombea urais katika uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.
Tayari Spika wa Bunge Samuel Sitta, aliwahi kusema kwamba, haoni tatizo la kusajiliwa CCJ huku pia akisema hawezi kuzuia watu kumuhusisha na chama hicho kama mgombea hapo Oktoba.
CCJ imekuwa ikitikisa nchi tangu taarifa zake kuchapishwa kwenye vyombo vya habari, kwani kuna majina makubwa yanatajwa akiwemo Spika Sitta, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, John Malecela, lakini wote wamekanusha.

No comments: