Wednesday, March 24, 2010

ANKAL


Mwasisi wa habari za jamii mtandaoni (social media) nchini Bw. Muhidin Issa Michuzi ameondoka leo Jumatano kuelekea London, Uingereza, kuhudhuria kongamano la pili la Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora 2 conference) kwa mwaliko maalumu akiwa kama blogger.
Bw. Michuzi, ambaye ametoa mchango mkubwa katika kupromoti habari za jamii mtandaoni kupitia blog yake maarufu ndani na nje ya nchi iitwayo
issamichuzi.blogspot.com, amealikwa huko mkutanoni na ubalozi wetu Uingereza ili kutoa mada inayohusu umuhimu wa habari za jamii mtandaoni katika kujenga daraja kwa walio ndani na nje ya nchi.
Akiongea nasi leo kabla ya kukwaa pipa la shirika la ndege la Emirates, Bw. Michuzi ambaye pia ni maarufu kwa majina kama Mzee wa Libeneke, Mdau na Ankal, amesema amefarijika sana kuona kumbe kuna wanaotambua mchango mkubwa unaoletwa na vyombo vya habari za jamii mtandano, hasa blogs.
Amesema anajisikia mwenye furaha sana kuona azma yake ya kuifanya tasnia hii ya kupashana habari kwa njia ya intaneti kwa waandishi wa hapa nyumbani unatambulika na kukubalika na kupewa heshima stahili kama ilivyo kwa vyombo vya kawaida kama vile magazeti, redio na luninga.
Bw. Michuzi, anayeweka rekodi ya kuwa bloga wa kwanza nchini kualikwa kama bloga kwenye mkutano muhimu kama huo, anaushukuru ubalozi wetu Uingereza chini ya Balozi Mh. Mwanaidi Maajar ambaye naye anakuwa miongoni mwa wazalendo wa kwanza kuutambua hadharani mchango wa wanahabari za jamii mtandaoni kwa kutoa mwaliko huo.
"Nilijua iko siku wanahabari za jamii mtandaoni tutatambulika na mwaliko huu hakika umekuja wakati muafaka kwani msisimkmo na mwitikio wa jamii kuikubali njia hii ya mawasiliano hapa nyumbani umekuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.
"siku hizi habari za jamii mtandaoni zinachukua kiti cha mbele katika kusomwa na wenye kuwa na intaneti kutokana sio tu na habari kuwa za uhakika, zisizochujwa na za haraka bali pia kwa kule wasomaji kupata fursa ya kuchangia habari waionayo tofauti na ilivyo kwa magazeti, redio na luninga.
"dunia imezidi kuwa kijiji kimoja kidogo kwa teknohama hii ambayo hata Rais Jakaya kikwete yuko mstari wa mbele kutaka iendelezwe mijini na vijijini ili kuwezesha wananchi wawe na habari za uhakika, za haraka na zenye kutoa fursa ya wasomaji kuchangia maoni" alisema Bw. Michuzi.
Blog ya
issamichuzi.blogspot.com ilianza rasmi Septembe 8, mwaka 2005 katika jiji la Helsinki, Finland, ambako alikwenda kuhudhuria mkutano wa Helsinki Conference akiwa kama mwandishi na mpiga picha wa gazeti la Daily News.
Alikuwa ni bloga wa siku nyingi aliyekuwa anaishi Marekani wakati huo, Bw. Ndesanjo Macha, aliyemshawishi Bw. Michuzi kufungua blog yake na kuwa bloga wa kwanza wa Tanzania kuupasha ulimwengu ya kila linalojiri nchini, kazi ambayo ameifanya kwa ustadi mkubwa kiasi ni hivi majuzi tu ameweza kufikisha wasomaji milioni 8, kati ya hao asilimia 30 wakiwa ni wasomaji wa hapa hapa Tanzania.
Bw. Michuzi ameweka wazi kwamba amefurahi na kusisismkwa sio kwa sababu anakwenda ulaya, kwani ameshatembelea karibu miji mikubwa yote duniani, ukiondoa Australia na New Zealand, ila amefarijika kwa sababu hatimaye blog zimeanza kutambuliwa rasmi.
Anatoa masikitiko yake kwamba pamoja na fanaka hiyo, lakini bado hapa nyumbani jamii, hasa ya mahafidhina (conservatives) wasiotaka mabadiliko wamekuwa wazito kukubali kwamba vyombo vya habari za jamii mtandaoni vimeshapata nguvu sawa na vyombo vya kawaida kutokana na wingi wa wasomaji na hata kupelekea kujitokeza kwa wadhamini wanaotangaza biashara zao humo.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Michuzi amesema anatamani sana kuanzisha umoja wa wanahabari za jamii mtandaoni ili kutetea na kulinda maslahi yao pamoja na kuindeleza tasnia hii ambayo inakua kwa kasi za ajabu.
Kwa mahesbu ya haraka haraka hivi sasa kuna blog zinazotumia lugha ya kiswahili zipatazo 200 ambapo pia blog takriban 10 zinaanzishwa kila siku, na kuifanya Tanzania kuw nchi zinazoendelea katika tasnia ya habari kwa njia ya mtandao.

No comments: